Sunday, January 19, 2014

MCHINA AKAMATWA NA MENO YA TEMBO UWANJA WA NDEGE DAR ES SALAAM


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA
MATUKIO YA UJANGILI WA CHUI NA TEMBO 
Jumamosi, tarehe 18 Januari 2014, majira ya saa 12:45 jioni katika eneo la Yombo Vituka, Jijini Dar Es Salaam, askari wa wanyamapori wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Mashariki walifanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa wa ujangili kwa jina Mwajuma Hamis. Mwajuma alikutwa akiwa na nyara za Serikali ambazo ni ngozi mbili za chui ndani ya nyumba anamoishi kinyume cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Mtuhumiwa huyo amekabidhiwa kwa Polisi kwa hatua zaidi za kisheria na amefunguliwa jalada na. CHA/RB/564/2014.

Pia, siku ya Ijumaa, tarehe 17 Januari 2014, jioni kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, askari wa KDU kanda ya Mashariki walimkamata raia wa China aliyefahamika kwa jina la LING TIAN mwenye hati ya Kusafiria na. G28214172. Bwana Tian alikutwa akiwa na bangili 2 na mkufu 1 wenye golori 11 zilizotengenezwa kutoka meno ya tembo. Mtuhumiwa amefikishwa Polisi na kufunguliwa jalada na. JNIA/IR/16/2013 kwa hatua zaidi za kisheria. Mtuhumiwa huyo, ambaye kwa sasa yuko rumande, alikuwa anatokea Msumbiji kwenda China.

Serikali haitalala hadi majangili wote wanapatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Ilani inatolewa kuwa Tanzania si kichaka cha kupitishia meno ya tembo au magendo ya aina yoyote. Wizara inawahakikishia wananchi kuwa imejizatiti vilivyo kupambana na vitendo vya ujangili katika mapori yote, maeneo yote ya mipaka ya nchi yetu na kwenye viwanja vyote vya ndege pamoja na bandari zote.

Wizara inatoa pongezi kwa raia wote ambao wanaisaidia kuwabaini waalifu. Tunatambua kuwa wengi wa wahalifu ni raia walio miongoni mwetu. Tunawaomba wananchi waendelee kutoa kwa Wizara habari zinazohusu ujangili ili tuendelee kuwabana na hatimaye kuusambaratisha mtandao wa ujangili ili tusalimishe maliasili zetu na kuokoa uchumi wa nchi.

Imetolewa na:
Chikambi K. Rumisha
Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii

No comments:

Post a Comment