BASI mmoja lanusurika kuwaka moto na daladala moja yateketea yote kwa moto wakati wanafunzi wa masomo ya kuunga vyuma katika gereji bubu eneo la uwanja wa Samora mjini Iringa wakijifunza kuunga ngao ya daladala hiyo yenye namba za usajili T189 AWN .
Tukio hilo limetokea leo majira ya 2.15 mchana wakati vijana wawili wanaojifunza kuunga wakiendelea na mafunzo ya kuunga ngao ya daladala hilo.
Akizungumzia ajali hiyo mmoja kati ya wafanyakazi wa gereji hiyo Filibert Mwihava alisema kuwa chanzo cha daladala hilo kuwaka moto ni vijana wawili ambao wanajifunza ufundi wa kuunga vyuma katika eneo hilo kufanya kazi hiyo bila kuzingatia kanuni ya kazi hiyo.
Kwani alisema vijana hao walikuwa wakiunga ngao ya nyuma ya daladala hilo jirani na tenki la mafuta na kutokana na cheche zilizokuwa zikitoka zilisababisha moto kuibuka kwa kasi .
Hata hivyo alisema mbali ya kuwa na kifaa cha kuzimia moto bado walishindwa kukitumia kifaa hicho kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ya kukitumia.
Mwihava alisema kutokana na moto huo kushika daladala hilo linalofanya safari zake kati ya Tumaini na Zizi la Ng'ombe mjini Iringa hakuna mtu aliyezulika zaidi ya basi lenye namba za usajili T 457 AMQ kutetekea upande wa mbele kabla ya kuokolewa .
Pia alishukuru kikosi cha zimamoto na uokoaji mjini Iringa ambao walifika kwa wakati na kufanikiwa kuzima moto huo ambao ungeweza kusababisha madhara makubwa katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na ofisi maduka ya watu waliojenga kuzunguka uwanja wa Samora kuteketea..
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kiongozi wa askari wa zimamoto ambao walifika eneo hilo John Zacharia alisema kuwa kuwa chanzo cha moto huo ni uzembe wa ofisi hiyo.
Kwani alisema hata kifaa cha zimamoto walichokuwa nacho kilikuwa hakifanyi kazi kutokana na kuharibika muda mrefu.
Huku kifaa cha kuzimia moto kilichokuwemo katika daladala hilo ni kifaa ambacho kidogo zaidi na maalum kwa gari dogo ambacho pia kilikuwa hakifanyi kazi.
Zacharia aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuzingatia sheria za zimamoto ya kuwa na vifaa vya kuzimia moto badala ya kudanganya na kuona kama wanaonewa pale wanapolazimishwa kuwa na vifaa hivyo.
|
No comments:
Post a Comment