OFISI za Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, jana ziligeuka uwanja wa masumbwi baada ya Mstahiki Meya, Henry Matata na madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuchapana makonde.
Vurugu hizo zilizoanza majira ya saa 4:45 asubuhi na kudumu kwa takribani dakika 25, zilitokana na mgogoro wa siku nyingi kati ya Meya Matata na madiwani wa CHADEMA.
Madiwani wa CHADEMA walifika katika ofisi ya mkurugenzi kutaka kupata nakala ya barua ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyeamuru madiwani watatu waliofukuzwa na Meya Matata warudishwe madarakani, jambo ambalo mkurugenzi hataki kulifanya hadi sasa.
Madiwani hao wakiwemo wa CCM na CUF, pia walifika makao makuu ya wilaya kuhudhuria kikao maalumu cha bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015, kilichopangwa kufanyika jana.
Katika kushinikiza kupata barua hiyo, Diwani wa CHADEMA, Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera, alimfungia ndani Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Alhaji Zuberi Mbyana.
Mkurugenzi Mbyana alifungiwa ndani wakati alipokuwa akijadiliana na madiwani wengine wa CHADEMA, kuhusu madai ya taarifa za Waziri Mkuu, Pinda kuwarudisha madarakani madiwani watatu waliofukuzwa na Matata.
Matata ambaye amekuwa na mvutano mkubwa na CHADEMA, huku akilindwa na serikali, aliwatimua madiwani hao Desemba 10 mwaka juzi kwa madai ya kutohudhuria vikao vya Baraza la Madiwani vitatu mfululizo bila idhini yake.
Madiwani waliofukuzwa na Matata na kata zao kwenye mabano ni Dani Kahungu (Kirumba), Marietha Chenyenge (Ilemela), pamoja na Abubakar Kapera wa Nyamanoro, wote wa CHADEMA.
Hali ilivyokuwa
Wakati majadiliano hayo yakiendelea baina ya Mbyana na madiwani hao ndani ya ofisi ya mkurugenzi, Kapera alidaiwa kufunga geti la mlango kwa kufuli, jambo lililoibua vurugu kubwa.
Baada ya kuibuka ghasia hizo, Meya Matata akiwa amevalia joho lake la umeya, akiwa na mabaunsa wake wawili waliokuwa wamevalia suti na miwani nyeusi, alifika na kumrukia kichwa kisha kumtwanga ngumi, hali iliyozua tafrani kubwa.
Huku askari mgambo wa manispaa hiyo wakijaribu kuingilia kutuliza vurugu hizo, Kapera alisikika akilalamika kwa sauti akisema: “Hivi wewe Matata kwanini umenipiga? Sheria gani inayokuruhusu kunipiga? Hebu niachieni nimuonyeshe huyu Matata!”
Wakati Kapera akisema hayo, askari mgambo na baadhi ya watumishi wa Manispaa ya Ilemela, walikuwa katika wakati mgumu wa kuzuia hali hiyo, ambapo Matata naye alisikika akisema kwa sauti: “Nitakupiga tu, wewe ni bwana mdogo. Nimekupiga ndiyo, kwani utanifanya nini wewe? Eeeh nimekupiga na nitaendelea kukupiga.”
Huku sekeseke hilo likiendelea, Diwani wa Kata ya Ilemela, Chenyenge, alisikika akisema kwa sauti ya juu: “Hivi kwanini diwani wetu apigwe? Huyu Matata ni nani na analindwa na nani kwenye nchi hii? Tuko tayari halmashauri hii ifutwe, maana haina faida kwa wana
nchi na inatumia rasilimali za wananchi bure. Tunataka ifutwe hii halmashauri, ifutwee, ifutweeee.” Baadaye alifika Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ilemela, Amina Masenza kutuliza hali hiyo na kuagiza aliyemfungia mkurugenzi na madiwani aufungue mara moja.
Wakati DC huyo akitoa amri hiyo na kuondoka eneo hilo kurudi ofisini kwake, Matata alizuia mlango huo usifunguliwe.
“Hakuna mlango kufunguliwa hapa. RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza) amesema anakuja, usifunguliwe huo mlango, RPC anakuja,” alisema. Lakini baadaye mlango ulifunguliwa.
Baada ya ghasia
Baada ya kufunguliwa, Mkurugenzi Mbyana alitoka haraka haraka huku akicheka, kisha kuomba apelekewe chai ofisini kwake.
“Nileteeni chai huku,” alisikika akisema huku akielekea ofisi ya mkuu wa wilaya chini ya ulinzi wa mgambo.
Alipofika ofisi ya mkuu wa wilaya, mkurugenzi huyo alibeba sahani ya chai yenye vitafunwa, kisha kutoka na kuelekea kwenye ofisi ya meya ambapo Matata alikuwa amekaa baada ya vurugu.
Baadaye mkurugenzi huyo alitoweka maeneo hayo ya ofisi za halmashauri, na madiwani watano wakiongozwa na Meya Matata waliingia ukumbini na kupitisha bajeti ya sh bilioni 35.8, ambapo zaidi ya asilimia 65 ya bajeti ni matumizi, huku asilimia 28 pekee ya fedha hizo, ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, kikao hicho cha kujadili na kupitisha bajeti kilifanyika ndani ya dakika 20 kikawa kimemalizika na hakuna diwani aliyehoji chochote katika bajeti hiyo.
Wakiwa maeneo ya ofisi za halmashauri hiyo, diwani Kapera, katibu na dereva wa mbunge wa Ilemela, walikamatwa na polisi kisha kupelekwa katika Kituo cha Polisi Kirumba kwa mahojiano zaidi, na baadaye waliachiwa kwa dhamana.
Akizungumzia vurugu hizo baada ya kumalizika kikao cha kupitisha bajeti, Meya Matata alikiri kumrukia na kumpiga ngumi diwani Kapera na kujisifu kwamba anajua kupigana na yupo tayari kumkodia gari waende wakapigane eneo la wazi wakiwa wawili tu.
Matata anayedaiwa kuiongoza halmashauri hiyo kwa kulindwa na Serikali ya CCM, aliapa kuwafukuza madiwani wote wanane wa CHADEMA, iwapo hawatahudhuria vikao vingine viwili siku zijazo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamwe hawatarudi nyuma kupigania haki yao na wananchi kwa ujumla na kwamba msimamo wao hadi sasa hawamtambui Matata kama Meya wa Ilemela na wataendelea kususia vikao.
Mbunge huyo alihoji iwapo madiwani walifukuzwa kwa kufuata sheria za nchi tangu Desemba 10, 2012, iweje serikali imeshindwa kutangaza uchaguzi mdogo katika kata hizo.
“Tulishabaini kinachofanyika hapa ni Serikali ya CCM kutanguliza maslahi ya kisiasa na si maslahi na haki za wananchi,” alisema.
Diwani wa Kirumba, Dani Kahungu, alisema kikao cha bajeti kilichofanyika ni batili kwani haikutimia akidi ya wajumbe ambayo ni theluthi mbili ya madiwani wote 14 wa manispaa hiyo, hivyo fedha za walipakodi zimetumika vibaya.
Diwani Kapera alithibitisha kupigwa na Matata katika vurugu hizo na kuongeza kwamba wamechoka kunyanyaswa na serikali, kwani wana taarifa za kurejeshwa kwao uongozini na Waziri Mkuu, Pinda.
Mwanzo wa mgogoro ulivyo
Vurugu hizo ni mwendelezo wa mgogoro uliopo tangu Novemba 9, 2012, baada ya Matata na naibu wake, Swila Dede (CCM), kuchaguliwa na madiwani sita kushika nyadhifa hizo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika chini ya Mkurugenzi Mbyana, ukihudhuriwa na DC Masenza, madiwani wote wa CHADEMA ambao idadi yao ni wanane, hawakuhudhuria kwa madai kwamba haukufuata wala kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi.
Licha ya Manispaa ya Ilemela kuwa na madiwani 14, siku hiyo ya uchaguzi madiwani wanne wa CCM, mmoja wa CUF ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu, Mkiwa Kimwanga pamoja na Matata aliyefukuzwa uanachama ndani ya CHADEMA, ndiyo waliopiga kura ya kuchagua meya na naibu wake.
Matata alishafungua kesi mahakamani kupinga kufukuzwa uanachama, lakini hukumu yake haijatolewa.
Katika hilo, madiwani wa CHADEMA pamoja na chama chao, wameendelea kutomtambua Matata kama meya kwa madai kwamba idadi ya wajumbe ambayo inatakiwa iwe theluthi mbili (2/3) ya madiwani 14 haikutimia.
Mgogoro huo ulisababisha Mbunge wa Ilemela, Kiwia adai kutishiwa kuuawa na Meya Matata mbele ya mkuu wa wilaya na askari polisi wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani ambalo lilivurugika pia.
No comments:
Post a Comment