Picha ya pamoja kabla ya kuondoka kijijini hapo
Mwanamke Aida Nakawala(25) aliyejifungua watoto wanne kwa mkupuo usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Wazazi ya Meta kwa ajili ya hifadhi ya chumba cha joto kwa watoto na huduma muhimu kwa mzazi amewasili kijijini kwao Chiwanda na kupokelewa na mamia ya wakazi wa hapo.
Mapokezi hayo yaliyofanyika jana, mara baada ya kuwasili nyumbani kwake kijijini hapo akitokea katika Hospitali ya Wazazi ya Meta alikokuwa akipatiwa matibabu, ambapo Wakazi hao walionekana kushangazwa na kitendo cha mama huyo kujifungua watoto wanne kwa mkupuo tena kwa njia ya kawaida.
Baadhi ya majirani waliokuwepo Nyumbani kwa Mwanamke huyo wakiongozwa na Serikali ya Kijiji, walisema wapo tayari kumpa msaada mama huyo shujaa wa hali na mali.
Hata hivyo wakati Wananchi wakionesha furaha na mishangao Serikali ya Kijiji pia imejipanga kuhakikisha inaisaidia Familia hiyo ambayo haina uwezo kimaisha kutokana na baba wa Familia Webson Simkanga(28) kutegemea kilimo cha Mahindi huku akiwa na jumla ya watoto Sita, kutunza watoto hao kwa kupanga mikakati mbali mbali ya muda mfupi na muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari waliofanikisha Safari ya Mama huyo kutoka Hospitali ya Wazazi Meta hadi kijijini kwao umbali wa Kilomita zaidi ya 130, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chiwanda, Ignas Sinkara aliwapongeza waandishi hao kwa moyo walioonesha na kuwaomba kuendelea kujitolea hivyo hivyo katika majukumu mengine.
Alisema moja ya michango iliyopatikana imesaidia huduma za mama alipokuwa Hospitali, kukarabati Nyumba atakayoishi baada ya kujifungua pamoja na kusaidia shughuli za Shamba kutokana na wazazi wote wawili kutakiwa kusaidiana katika kuwahudumia watoto hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mpumpi anapotokea Mama huyo, Winstoni Mtali, alisema mbali na juhudi zilizopangwa na serikali ya kijiji pamoja na wasamaria wema walionesha kuguswa na mama huyo tangu alipojifungua bado misaada zaidi inahitajika kutokana na mzigo huo kuwa mkubwa kwa Wanakijiji.
Alisema bado mazingira ya nyumbani kwa mwanamke huyo na kijiji kwa ujumla siyo rafiki kwa malezi ya watoto hao kutokana na nyumba yao kutokuwa katika mazingira mazuri hivyo kuhitajika michango ya hali na mali kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hiyo ambayo inahitaji kusakafiwa, kupigwa dali, madirisha na kusakafia kuta ili watoto wasidhurike na vumbi la ndani
Waandishi waliojitolea kufanikisha safari ya Mwanamke huyo hadi kijijini kwao ni pamoja na Venance Matinya(JamboLeo), Ezekiel Kamanga(Bomba Fm Redio), Joseph Mwaisango ambaye ni mmoja wa wakurugenzi wa mtandao wa kijamii wa Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment