IDADI ya Tembo nchini imepungua kutoka 38,975 mwaka 2009 hadi kufikia 15,174 mwaka huu.
Hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya sensa yaliyofanyika Oktoba na Novemba mwaka jana katika mbuga za hifadhi za Selous-Mikumi na Ruaha-Ruangwa.
Hayo yalielezwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu wakati akizungumzia matokeo ya sensa ya idadi ya tembo katika mfumo wa ikolojia jijini Dar es Salaam.
Akitoa mchanganuo wa idadi ya tembo waliokufa katika mapori hayo ya hifadhi ya taifa, Waziri Nyalandu alisema katika pori la Selous-Mikumi kuna tembo 13,084 na Ruaha-Ruangwa 20,090 huku akieleza kuwa takwimu hizi zinaonyesha kupungua kwa idadi ya tembo katika mapori hayo ikilinganishwa na sensa iliyofanyika awali.
Alisema kupungua kwa idadi hiyo ya tembo kunathibitishwa na idadi ya mizoga ya tembo iliyohesabiwa wakati wa zoezi la sensa ambapo 6,516 na 3,496 ilihesabiwa katika mifumo ya ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha-Ruangwa.
Alibainisha kuwa katika zoezi hilo wizara ilitumia vigezo vya uwiano wa mizoga na tembo hai waliohesabiwa ‘Carcass Ratio’ kubaini vyanzo vya vifo hivyo.
Alisema katika hali ya kawaida, uwiano wa asilimia 7-8 unaashiria vifo vya asili vya ugonjwa na uzee, huku zaidi ya asilimia hiyo inaashiria vifo visivyo vya asili.
Nyalandu alisema sensa iliyofanyika mwaka jana inaonyesha uwiano wa asilimia 30 kwa mfumo wa ikolojia wa Selous–Mikumi na asilimia 14.6 kwa Ruaha-Ruangwa.
“Kwa mujibu wa matokeo hayo, idadi kubwa ya vifo vya tembo vimetokana na vifo visivyo vya asili na kwamba asilimia 95 na 85 ya mizoga iliyoonekana katika mifumo ya ikolojia ya Selous–Mikumi na Ruaha–Ruangwa ni zaidi ya miezi 18 iliyopita,” alisema Nyalandu.
Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa juhudi za makusudi zilizofanywa na serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria na operesheni maalumu za hivi karibuni, zimesaidia kupunguza kasi ya ujangili kwa kiasi kikubwa.
Nyalandu alisema kukamatwa kwa meno ya tembo yenye uzito wa kilogramu 32,987 ndani na nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 2008 hadi Septemba 2013, ni ishara tosha kwamba ujangili ni sababu kubwa ya kuisha kwa tembo hao.
Alisema juhudi mbalimbali zinachukuliwa na wizara yake ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi wa wanyama hai, kuanzisha Idara ya Wanyamapori inayojitegemea na kupitia upya sheria za uhifadhi ili kuruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa kijeshi kwa watumishi wa sekta ya wanyamapori.
Nyalandu alisema hata hivyo kutokana na matatizo yaliyotokea katika Operesheni Tokomeza Ujangili na kusababisha mawaziri wanne kung’olewa, serikali itaanzisha tena operesheni hiyo hivi karibuni ili kuhakikisha ujangili unakwisha kabisa.
Sensa hiyo pia imetumia kiasi cha dola za Kimarekani 160,000 ikiwa ni fedha za serikali na wafadhili kutoka Shirika la Misaada ya Kiufundi la Ujerumani (GIZ) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kupitia mradi wa TANAPA wa Spanet.
Katika hatua nyingine, Richard Temu (36), askari wa wanyamapori, amevunjika miguu wakati wa mapambano na majangili kwenye pori la akiba la Ugala lililopo Wilaya ya Sikonge.
Askari huyo amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Tiba za Mifupa (MOI) kwa ajili ya matibabu zaidi na Naibu Waziri Nyalandu alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali jana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Temu alisema wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na majangili kutumia silaha za kivita, SMG wanapovamia mapori ya hifadhi.
No comments:
Post a Comment