Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Sheikh Ahmed Jongo alipowasili kufungua kongamano la viongozi wa dini lililokuwa likijadili ‘Rasilimali za Gesi, Mafuta na Madini kwa Amani na Maendeleo ya Watanzania’ jijini Dar es Salaam jana.
Rais Jakaya Kikwete amefunga mjadala wa wafanyabiashara wazawa wanaotaka kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa sekta ya gesi akisema Shirika la Maendeleo la Petroli(TPDC) linajitosheleza kuwasaidia Watanzania wanufaike na rasilimali hiyo. Katika kipindi cha miaka miwili, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameshikilia kuwa hakuna Watanzania wenye uwezo wa utafutaji, uchimbaji na uzalishaji, jambo ambalo linapingwa vikali na wafanyabiashara wazawa.
Akizungumza jana wakati wa Kongamano la Viongozi wa Dini kuhusu rasilimali ya gesi, mafuta na madini kwa ajili ya amani na maendeleo ya taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema hakuna kampuni nchini yenye dhamana ya kupata mikopo kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hiyo.
“Kampuni za kigeni zenye mitaji mikubwa zinafanikiwa kupata mikopo kwa kuwa zina dhamana inayowasaidia kupata mikopo kwenye mabenki,” alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema kama kuna kampuni za Watanzania zinatakiwa kushirikiana na wawekezaji watapaswa kufuata taratibu zilizowekwa.
Rais Kikwete alisema uwekezaji kwenye sekta ya mafuta ni kama mchezo wa kamari kwani mtu anaweza kuwekeza fedha nyingi katika utafutaji wa gesi na asipate kitu.
“Ni kampuni gani Tanzania ambayo itakuwa tayari kucheza kamari?” alihoji Rais Kikwete.
Alisema ndio maana Serikali imeona ni vizuri iandae mpango wa kuiwezesha TPDC kuingia kwenye shughuli za gesi badala ya kuwa kutoa leseni tu.
“Tunataka siku moja TPDC iwe na uwezo wa kuwauzia hisa Watanzania iwe kama kampuni kubwa za Statoil(Norway) na Petro Plus(Brazil) zinazoendeshwa na Serikali zao,” alisema.
Rais Kikwete alisema baada ya kuliwezesha shirika hilo, Watanzania watanufaika kwa kiwango kikubwa tofauti na kutoa kipaumbele kwa kampuni binafsi za Watanzania.
Washiriki watoa maoni tofauti
Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima alipinga kongamano hilo kufanyika sasa kwani alieleza lilipaswa kufanyika miaka mitano iliyopita na sio sasa wakati ambapo shughuli za uchimbaji wa gesi zinakaribia kuanza.
Akizungumza wakati wa akisoma salamu za viongozi wa Dini ya Kikristo katika kongamano hilo, Dk Kitima alisema kongamano kama hilo haliwezi kubadili chochote na kinachofanyika ni kwa wawekezaji kujifagilia njia wakati wanaelekea katika kuanza kutekeleza miradi waliyowekeza.
“Hapa ninachoweza kusema ni kuwa wafadhili hao wametoa fedha, wamefadhili kongamano hili ili wakianza shughuli zao wasisumbuliwe,” alisema na kuongeza kuwa kinachofanyika sasa hakitoi taswira nzuri kwani jamii imelishwa sumu kuwa haiwezi kufanya lolote bila kuombaomba.
Akionekana kujibu hoja hiyo, Askofu Stephen Munga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), aliomba kuweka sawa dhana hiyo kwa kusema kuwa sio sahihi kuwa mkutano huo umefadhiliwa na matajiri wa gesi na mafuta.
“Kongamano tumeandaa wenyewe baada ya baadhi ya maaskofu wa KKKT kufika ofisini kwa Waziri wa Nishati na Madini, Muhongo kuzungumza nae kuhusiana na uharibifu wa mazingira na akataka pia tuzungumzie suala la gesi, ndio tukaona kuna haja ya kufanya kitu kama hiki ambacho kinafanyika sasa,” alisema.
Naye Sheikh Aboubakary Zuberi alisema ni vizuri watu ambao wanaishi katika maeneo ambako rasilimali zinapatikana ni vizuri wakanufaika nazo badala ya kuwa kama ilivyo sasa jambo ambalo haliwezi kuleta matokeo mazuri siku za mbeleni.
Alisema nchini kuna mgawanyiko mkubwa wa mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment