Na Saleh Ally
Tayari Yanga imekubaliana na kuingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Mholanzi, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm.
Kazi hiyo ilipangwa kumalizika leo asubuhi na kocha huyo ana mambo mengi sana ya kuburudisha.
Pamoja na kuwa na miaka 64, lakini ni mchapakazi na amekuwa gumzo alipokuwa na kikosi cha Berekum Chelsea ya Ghana.
Akiwa na timu hiyo msimu wa 2012-13, alizitoa jasho na kuzipa wakati mgumu pia timu vigogo kama Al Ahly, TP Mazembe na Zamalek.
Sasa ndiyo wakati wake na Yanga wamempa kazi ya kuhakikisha kikosi chao kinafanya kazi ya uhakika katika Ligi ya Mabingwa na mtihani mkubwa ni watakapokutana na Al Ahly kama watavuka kizingiti laini cha Wacomoro.
Gazeti la Championi lilikuwa chombo cha kwanza nchini cha habari kuandika kuhusu uamuzi wa Yanga kujitupia kwa van der Pluijm.
Sasa tayari yuko na leo alikuwa apelekwe Zanzibar, lakini huenda akapumzika kujiandaa na safari ya Uturuki.
Pamoja na mambo mengi lakini kocha huyo ana mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake.
Utulivu:
Yanga imeamua kufanya kwa utulivu suala la kocha, awali lilikuwa likipelekwa mbio na kambi ya Uturuki, ikitaka kocha awahi kambi hiyo.
Lakini sasa uongozi wake umekubali hata kama kocha mpya hatakwenda Uturuki, lakini inataka ipate ‘mtu’ wa uhakika wa kuziba nafasi ya Brandts na ambaye atakuwa na uwezo kweli.
Mvuto:
Mvuto wa van der Pluijm kwa Yanga umetokana na mafanikio yake kwa Berekum Chelsea ambayo ilifanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.
Ilikuwa Kundi B na timu za Al Ahly, TP Mazembe na Zamalek ambao ni vigogo waliowahi kuchukua ubingwa Afrika zaidi ya mara moja, lakini Berekum Chelsea ikaonyesha inaweza.
Hicho ndiyo kitu cha kwanza kilichoivutia Yanga kwa kuwa inahitaji kocha wa kuifikisha mbali kwenye Ligi ya Mabingwa ikizingatiwa katika mechi ya pili tu (kama itawang’oa Wacomoro), itakutana na Al Ahly ambao ndiyo mabingwa.
Kingine kinachoonyesha kuwavuta Yanga ni umri wa kocha huyo, miaka 64 ni sawa na mzazi hasa, lakini makocha wengi wenye umri huo wamekuwa wakali, wanajali zaidi kazi na wasiokuwa na mzaha hata kidogo.
Mazingira:
Kwa mazingira ya nchi za Kiafrika, van Pluijm hawezi kuwa na hofu hata kidogo kwa kuwa ameishi katika bara hili kwa zaidi ya miaka 10.
Miaka yote hiyo ameishi nchini Ghana ambako ameoa mrembo wa Kiafrika wa nchi hiyo.
Uwanja:
Mholanzi huyo ni mtu wa misimamo sana, amewahi kususia mazoezi kutokana na ubovu wa uwanja. Kama Yanga itaingia mkataba naye, basi ina wakati mgumu kuhakikisha inamaliza tatizo hilo.
Kabla ya kuondoka kwa Brandts, kilio chake kilikuwa uwanja usiokuwa na kiwango na magoli madogo, maana yake van Pluijm lazima atalizungumzia, kama halitatekelezwa kama ilivyokuwa kwa Brandts, basi kuna tatizo linaweza kutokea.
Misimamo:
Van der Pluijm ni mtu mwenye misimamo kweli, kama akikubaliana na Yanga na kuanza kazi, maana yake wachezaji wajiandae.
Anatoa ushirikiano mkubwa kwa wachezaji, lakini ni mkali na asiyehofia jina la staa yeyote.
Vyombo vya habari vya Ghana vilimbandika jina la Kiboko ya Vigogo kwa sababu mbili, kwanza kuzipa wakati mgumu timu kongwe za Ghana kama Asante Kotoko lakini kuwaweka benchi wachezaji nyota walioonekana kuvimba vichwa na timu ya Berekum Chelsea ikaendelea ‘kukamua’.
Wachezaji wageni:
Amekuwa na msimamo wa kutaka wachezaji wa kigeni wanaoonyesha uwezo mkubwa kuthibitisha tofauti yao na wenyeji.
Hivyo, Emmanuel Okwi, Mbuyu Twite, Hamisi Kiiza na Didier Kavumbagu wanalazimika kufanya kazi kweli na si kubahatisha, la sivyo kibarua kitakuwa kigumu ikizingatiwa msimu ujao ni wachezaji watatu tu.
Mfumo:
Uchezaji wa timu anazozifundisha ni kasi sana, anataka washambulie pamoja na kurudi pamoja, lakini amekuwa akisisitiza kikosi chenye walinzi warefu au wenye uwezo mkubwa wa kupiga vichwa.
Mchezaji akiwa mvivu, huenda akawa na wakati mgumu wa kupata namba katika kikosi chake.
Ndiyo maana mazoezi yake ya mwanzo wa msimu kama timu ataanza nayo, yanakuwa makali sana kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa fiti kweli.
Van Nistelrooy:
Alimuibua mshambuliaji nyota wa Uholanzi, Ruud van Nistelrooy akiwa na umri wa miaka 17 tu na kumpa nafasi ya kucheza katika kikosi cha FC Den Bosch cha nchini kwao Uholanzi.
Van Pluijm aliitumikia FC Den Bosch kwa miaka 28 akiwa mchezaji na baadaye kocha. Akiwa kipa alicheza mechi 338 kwa misimu 18 kabla ya maumivu ya goti kumlazimisha kupumzika soka.
Aprili 1995, aliingia mkataba wa miaka miwili kuinoa SBV Excelsior hadi Desemba kabla ya kumuachia nafasi hiyo msaidizi wake John Metgod.
Mwaka 1999 alitua nchini Ghana na kujiunga na Ashanti Gold SC na kusaini mkataba wa mwaka, baadaye alitua nchini Ethiopia na kuanza kuinoa Saint George.
Sasa amekuwa akifanya kazi ya kuinoa timu ya vijana ya Feyenoord Ghana inayopata msaada kutoka katika klabu ya Feyenoord ya Rotterdam nchini Uholanzi.
Ngumi mkononi:
Oktoba, mwaka jana, akiwa na kikosi cha mabingwa wa Ghana wakati huo cha Medeama Sporting Club, van Der Pluijm alisaini mkataba wa miaka miwili, lakini hakudumu hata robo ya mkataba huo.
Kwani siku chache baada ya Makamu wa Rais wa Madeama, Albert Commey, kumtangaza kuwa kocha mkuu, akiwa ameiongoza timu hiyo katika mechi saba tu, van Der Pluijm alitangaza kuachia ngazi.
Uongozi wa Madeama ulikubali na kuficha, lakini ukweli baadaye uligundulika kuwa kocha huyo Mholanzi alizozana na msaidizi wake akavurumisha ngumi.
Katika mahojiano yake na mtandao wa Caf na vyombo vingine vya habari, Mholanzi huyo amekuwa akisisitiza kutotaka kulizungumzia suala hilo kwa madai ni sawa na kuongeza maadui bila sababu za msingi.
Kutokana na hali hiyo, alionyesha kuchukizwa na mwenendo wa mambo kwa kuwa kila alichokuwa akieleza kibadilishwe hakikufanyika, pia msaidizi wake pamoja na kwamba alipendekeza kuchukuliwa kwa Mholanzi huyo kama bosi wake, alikuwa mbeya sana.
Pamoja na hivyo, kikosi chake cha Madeama hakikufanya vizuri kabisa, kwani alianza na mechi ya Kombe la Super Cup dhidi ya Asante Kotoko na kuchapwa bao 3-0. Aliiongoza timu kwa jumla ya mechi saba, badala ya kubeba jumla ya pointi 21, timu yake ilipata pointi nane tu!
Katika mechi hizo saba, kikosi chake kilishinda mechi moja tu, sare tano na kupoteza mechi moja.
Wakati anaondoka alikiacha kikiwa katika nafasi ya tisa kwenye ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara wakati huo, Asante Kotoko.
No comments:
Post a Comment