Maliasili na Utalii Yawasimamisha Kazi 21 Kwa Tuhuma za Ujangili
WIZARA ya Maliasili na Utalii, imewasimamisha kazi watumishi wake 21 kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia ujangili wa nyara za Serikali. Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Polisi mkoani Singida, kumkamata ofisa wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kwa tuhuma za kupatikana na silaha mbili na nyara za Serikali, kinyume cha sheria.
Akitangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema Serikali inasikitishwa na vitendo viovu vinavyofanywa na watumishi wake na haitavivumilia. “Tumesikitishwa na kitendo cha ofisa wanyamapori wilayani Singida kukamatwa na bunduki mbili na ndege aina ya Heroe 12 nyumbani kwake, hatua tuliyochukua ni kumsimamisha kazi na kufikishwa mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Wizara baada ya kufanya uchunguzi, imegundua kuwa kuna watumishi wanaoshirikiana na mtandao wa ujangili, hivyo imewasimamisha kazi watumishi 21 wa Idara ya Wanyamapori na tutachukua hatua zaidi.”
Alisema kati ya watumishi hao, 11 wanatoka katika Kikosi cha Kuzuia Ujangili mkoani Arusha, wanne wanatoka Mkoa wa Rukwa katika Pori la Akiba la Lwafu, mmoja Kikosi cha Bunda, watatu Pori la Akiba la Maswa, mmoja Selous, na mwingine mapori ya Lupika, Lumesule na Lusangu.
Akifafanua kuhusu uhaba wa watumishi katika Idara ya Wanyamapori, Nyalandu alisema kwa zaidi ya miaka 10 wizara hiyo haikuwa ikiajiri watumishi hali inayosababisha kukosa watumishi wenye ujuzi.
“Tunajipanga kuajiri watumishi wengine wenye ujuzi na kuangalia maendeleo ya teknolojia hasa kwa kujifunza kwa wenzetu Afrika Kusini,” alisema.
Kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, alisema Serikali imeunda tume ya kimahakama itakayowahoji askari waliohusika na kurudisha taarifa. Hata hivyo alisema wako mbioni kuendelea nayo.
“Rais Jakaya Kikwete ameunda tume ya kimahakama na itatoa taarifa, ila sisi hatutalala, tutahakikisha kuwa tunapambana na ujangili ili kulinda nyara za Taifa,” alisema Nyalandu.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wizara yake kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kuwakamata wahalifu.
“Jitihada hizi siyo zetu wenyewe, tunashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama. Tunawaomba wananchi washirikiane kulinda na kutoa taariza zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu. Tunawaomba watumishi wetu wafanye kazi kwa moyo na uaminifu,” alisema Nyalandu.
Mamlaka ya wanyamapori
Akiwa katika pori la akiba la Selous hivi karibuni, Nyalandu alieleza mkakati wa Serikali wa kuanzisha mamlaka ya wanyamapori ili kuwapa mamlaka watendaji wa sekta hiyo katika kutunza maliasili
Akiwa katika pori la akiba la Selous hivi karibuni, Nyalandu alieleza mkakati wa Serikali wa kuanzisha mamlaka ya wanyamapori ili kuwapa mamlaka watendaji wa sekta hiyo katika kutunza maliasili
No comments:
Post a Comment