JACK PATRICK MATESO SAA 48, DADA YAKE AMLILIA, ASEMA ALIMUONYA
HABARI ya kufungia mwaka 2013 na kufungua pazia la mwaka mpya wa 2014 ni madai ya mwanamitindo kiwango Bongo, Jacqueline Patrick kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Macau nchini China akiwa na mzigo wa madawa ya kulevya aina ya heroin lakini Risasi Mchanganyiko linaangaza mapya zaidi juu ya sakata hilo.
Macho na masikio ya Wabongo wengi kwa sasa ni juu ya mwenendo wa madai hayo, wakati gazeti hili likiendelea kupekenyua limenasa mpya kuwa, Jack yupo kwenye mateso makali kutoka kwa askari wapelelezi nchini humo wanaotaka kujua mtandao unaomuunganisha katika mchezo huo.
SAUTI KUTOKA CHINA
Chanzo chetu makini kilichopo China ambacho kinapiga kitabu kilieleza kuwa, katika kufuatilia ishu hiyo, juzi Jumatatu, Desemba 30, 2013, alikutana na kizingiti cha kushindwa kuonana na Jack katika mahabusu aliyowekwa kwa maelezo kwamba, uchunguzi bado unaendelea.
Raia huyo wa Tanzania aliyedai ana ukaribu na Jack, kwa sharti la kutochorwa jina lake gazetini, alisema mengi kuhusiana na mateso anayopata mrembo huyo hivi sasa.
“Ni kweli Jack amekamatwa hapa Macau. Hilo halina ubishi kabisa. Sheria za huku zinatofautiana kati ya jimbo na jimbo. Nilifika mahabusu aliko kwa lengo la kutaka kumwona lakini nilikataliwa. Nimeambiwa hawezi kuonana na mtu yeyote hadi Machi, mwakani (mwaka huu). Bado wanaendelea na uchunguzi kwanza.
“Unajua wanajaribu kufichaficha mambo ili polisi waweze kufanya upelelezi wao vizuri lakini nimepenyezewa taarifa kuwa ataingizwa chumba cha mateso ili abanwe na kutaja mtandao wake. Wanajua yeye wameshamkamata, lakini wanataka kufahamu mzigo alitumwa na nani, ameutoa nchi gani na unakwenda nchi gani?
“Lengo la kufanya hivyo ni kukomesha mtandao mzima wa madawa ya kulevya. Si ajabu akawa kwenye mateso kwa kipindi chote hicho kama hatakuwa mkweli lakini kwa sasa ataingizwa kwenye kikosi cha kwanza.
“Hapo atakalishwa kwenye chumba cha mateso kwa siku mbili mfululizo (akimaanisha saa 48). Ni mateso makali sana. Wataalam wanajua wanafanyaje ili mtuhumiwa aweze kuzungumza ukweli kwa muda mfupi. Sasa hapo ikishindikana ndipo anaweza kuhamishiwa kwenye kikosi kingine,” alipasha mtoa habari wetu na kuongeza:
“Ni kama huko Bongo tu. Unaposikia chumba cha mateso ya wapelelezi maana yake shughuli yake siyo ndogo. Mimi namuonea huruma sana Jack, lakini najiuliza, hivi ni kwa nini huwa hawajifunzi kupitia wenzao?
“Si juzi tu wengine (Agnes Gerald ‘Masogange’ na Melisa Edward) wamekamatwa kwa madawa hayohayo na walisota kwa muda mrefu? Kwa nini hawasikii jamani? Namuhurumia sana kwakweli.”
KUMBE DADA YAKE ALIMUONYA
Habari kutoka kwa mtu wa karibu na dada wa Jack zinasema kuwa, wakati akitaka kusafiri akitokea Bongo, alimweleza dada yake juu ya mpango wake huo, akamuonya lakini modo huyo alikataa.
“Alimfuata dada yake na kumweleza mchongo mzima kuwa alitaka kwenda na mzigo China, dada yake akamwambia aachane na hizo biashara, akakataa. Jack alifikia hatua akamwambia dada yake kuwa hana mtoto, hana mume wala ndugu anayemtegea kwa hiyo yupo tayari kwa lolote kwani hakuwa na cha kupoteza.
“Kama angemsikiliza dada yake (jina linahifadhiwa) haya yote yasingemkuta na asingeingia kwenye mateso ya namna hii,” alisema mtoa habari wetu huku akiendelea kusisitiza jina lake lisionekane mahali popote kwenye ukurasa huu.
ABEBESHWA MZIGO, ALIPWA MALIPO YA AWALI
Ilizidi kusemekana kuwa, alipokaribia kuondoka Bongo, Jack alimwambia dada yake kwamba anakwenda kambini (kituo cha kuingiza mzigo tumboni) ambapo aliporejea kwa dada’ake alimuonesha dola za Kimarekani 21,000 (zaidi ya shilingi milioni 33) ambazo ni malipo ya awali huku akimwambia alishabebeshwa nusu ya mzigo.
Hata hivyo, habari zinasema Jack alimwambia dada yake huyo kuwa hakuwa akijisikia kusafiri lakini kwa kuwa anatafuta maisha aliamua kuondoka baada ya mzigo kukamilika wote siku iliyofuata.
INA MAANISHA NINI?
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Jack aliondoka na unga hapahapa Bongo kwenda Thailand kupitia Nairobi, Kenya na baadaye Macau, China ambako alinaswa.
MASTAA WAFUNGUKA
Watu wamekuwa na mitazamo tofauti kulingana na ishu hiyo lakini Risasi Mchanganyiko lilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya mastaa wa Bongo ambao wameeleza maoni yao kuhusiana na sakata hilo la Jack.
Katika mahojiano na waandishi wetu, tulitaka kusikia kutoka kwao namna wanavyolinganisha tabia ya kujihusisha na biashara za kusafirisha madawa ya kulevya na vitendo vya umalaya ambapo wametoa maoni tofauti.
JACQUELINE WOLPER:
“Mh! Mwenzangu, bora uwe na mabuzi (wanaume wenye mkwanja) 40 kuliko kufanya biashara ya madawa ya kulevya. Nawaomba mastaa wenzangu wasikubali kubebeshwa madawa kwa kudanganywa eti na dola 30,000, kamwe haiwezi kubadili mfumo wa maisha yako.”
REHEMA CHALAMILA ‘RAY C’:
“Madawa ya kulevya hayakubaliki, yalinitenda sana haya madude! Kabisa tulinde vizazi vijavyo kwa kupiga vita madawa ya kulevya. Fanya yote lakini siyo madawa ya kulevya.”
SHAMSA FORD:
“Nasema hivi, bora umalaya japo pia si mzuri kuliko kudili na biashara ya madawa ya kulevya. Nawaomba waachane na vitu hivyo kwani vinatumaliza kisanii... lakini nasisitiza kutulia na bwana mmoja ni vizuri sana kuliko kurukaruka.”
JOKATE MWEGELO:
“Hakuna aliye mkamilifu lakini kama kitu ni kiovu ni kiovu tu hata kama mimi na wewe tunakifanya, kimsingi hakuna bora na anayesema kuna ubora basi hajitambui. Vyote vinadhalilisha utu na thamani ya mwanamke. Mwili si wa kuchezewa.”
BLANDINA CHAGULA ‘JOHARI’:
“Tukitumia majina yetu vizuri, hakuna atakayejihusisha na yote hayo... tujitume kufanya kazi, umalaya unaweza kuwa bora kuliko kufanya biashara ya madawa ya kulevya kama utabanwa kuchagua maovu hayo. Maisha ya Ughaibuni yatatumaliza kwani tunaiga kwa kukurupuka bila kuelewa.”
TUMETOKEA HAPA
Jack anatuhumiwa kukamatwa na madawa ya kulevya Desemba 19, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Macau, China akitokea jijini Bangkok, Thailand akiwa safarini kwenda Guangzhou nchini China.
Ilielezwa kuwa unga aliokutwa nao una uzito wa kilo 1.1 ndani ya kete 57 huku thamani yake ikitajwa kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 223.
Bado yupo mikononi mwa polisi wa China wakati upelelezi wa awali ukiendelea ambao utafikia tamati Machi, mwaka huu kabla ya kuingia hatua nyingine.
No comments:
Post a Comment