Monday, February 3, 2014

Balozi Maajar Mwenyekiti mpya Vodacom

Balozi Mwanaidi Sinare Maajar





BODI ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Vodacom Tanzania, imemteua Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, kuwa Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo akichukua nafasi ya Peter Kisumo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Vodacom inaeleza Balozi Maajar amekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za kisheria, kibiashara, kidiplomasia na kuwekeza katika jamii na kuwa na msukumo tosha kwa vijana wengi wa sasa na wanaochipukia nchini.
Mbali na mafanikio hayo, Balozi Maajar ni kati ya waasisi wa kampuni ya uwakili iliyoanzishwa kwa umoja kati ya Maajar, Rwechungura, Nguluma na Makani ambayo ni zao la Kampuni ya Rex Attorneys, inayoongoza katika masuala ya kisheria nchini.
Kwa sasa yupo Rex ambapo anahodhi nafasi ya Mkuu wa Utekelezaji wa Sheria za Maliasili ambapo inajumuisha nishati, madini, mafuta na gesi.
Pia ni Mwenyekiti wa Tanzania Mozambique Centre for Foreign Relations and the International Consultant for the D Group, kituo kinachotoa ushauri kuhusu masuala ya uhusiano wa kimataifa, nafasi ambayo amekabidhiwa baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Andy Chande.
Balozi Maajar amemaliza wajibu wake kama Balozi wa Tanzania nchini Marekani na balozi asiye mkazi wa Mexico Machi mwaka jana.

No comments:

Post a Comment