Monday, February 17, 2014

MEMBE: TULIKAANGWA, TULIULIZWA MASWALI MAGUMU URAIS 2015

jpg_28028.jpg
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka nje ya ukumbi wa mahojiano na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula kuhusu mbio za urais 2015.
Akizungumza jana mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, Membe alisema kamati hiyo inauliza maswali magumu kuhusu wanayoyafanya pamoja yanayofanywa na mashabiki wao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amesema aliulizwa maswali mazito na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula kuhusu mbio za urais 2015.
Akizungumza jana mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, Membe alisema kamati hiyo inauliza maswali magumu kuhusu wanayoyafanya pamoja yanayofanywa na mashabiki wao.
"Kamati inauliza maswali mazito na magumu yanayohusiana na uvunjaji wa maadili ya uongozi wa chama chetu... Kamati ya maadili imejipanga vizuri sana wala msidanganyike, wanauliza maswali mazito," alisema Membe.
Membe aliongeza kusema aliulizwa mambo makubwa matatu, kubwa likiwa ni kuibuka ghafla kwa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila wakati chama hicho kinapokaribia kwenye uchaguzi wa Rais.
"Kuna mambo makubwa matatu ambayo kamati ya maadili imeyauliza. Kubwa kabisa ni uzukaji ghafla wa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila wakati wanapodhani mtu fulani anafaa kuwa kiongozi."
Alisema na kuongeza: "Suala la pili nililoulizwa ni tunafanyaje kukifanya chama chetu kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani kwenye uchaguzi?"
Suala la tatu ambalo wajumbe wa kamati hiyo wanauliza ni suala la fedha, kama msingi wa ushindi na kuhoji inakuwaje mtu atumie mamilioni au mabilioni ya shilingi kununua uongozi?
Membe alisema hayo ndiyo maeneo matatu ambayo kamati hiyo ya maadili imekuwa ikiyauliza na kusema kuna uwezekano mkubwa wa wanachama zaidi kuitwa kuhojiwa.
Alisema alitumia fursa hiyo kukishauri chama mambo kadha wa kadha ikiwamo CCM kufanya mchakato wa kumteua mgombea au wagombea urais mwaka huu ili waweze kujulikana kabla ya Desemba.
Kamati hiyo ya ndogo ya Maadili ya CCM iliyoanza kikao chake Alhamisi iliyopita, imewahoji makada sita wa chama hicho ambao wamekuwa wakitajwa kuanza kutangaza nia za kuwania kupendekezwa kupeperusha bendera yake kwenye kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Tayari kamati hiyo imeshawahoji Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa wanakivuruga chama kwa kuonyesha nia ya kuwania urais kabla ya muda ulioruhusiwa na chama hicho.
Pia kikao hicho kimewahoji Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

No comments:

Post a Comment