Sunday, February 16, 2014

CHADEMA YATISHIA KUSUSIA BUNGE

chadema-mnyika1_c4b47.jpg
Zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba mjini Dodoma, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitasusia bunge hilo, iwapo mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba hayatazingatiwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati alipokuwa akitoa taarifa ya Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika juzi, kuzungumzia Bunge la Katiba, uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga na uamuzi kuhusu madiwani wake mkoani Arusha.
Mbowe alisema Chadema wanakwenda kushiriki bunge hilo wakiwa na masikitiko kwa kuwa uteuzi wa wajumbe 201 uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete haukuwa na nia njema kwa taifa, kwani asilimia 80 ya walioteuliwa ni wanachama wa CCM. "Tunakwenda Dodoma lakini hatutakubali Bunge limilikiwe na wachache na hatutasita kurudi kwa wananchi tutakapoona mapendekezo ya Jaji Warioba hayatekelezwi," alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa Chadema hawaendi bungeni kugoma ila wananchi wasishangae watakapoona wanatoka ndani ya Ukumbi wa Bunge hilo, kwa kuwa lengo la uteuzi wa wajumbe lilikuwa ni kutaka kupata wabunge wengi watakao unga mkono CCM.
"Kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, CCM tayari wana wajumbe karibu asilimia 80, katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wana wajumbe karibu asilimia 68, kwa hiyo wanaweza wakakidhi vigezo vya mshindi kupatikana kwa theluthi mbili ya kura zilizopigwa kufanya uamuzi kwa niaba ya Bunge la Katiba," alisema Mbowe.
Hata hivyo, alisema Chadema hakitajali maoni yatakayotolewa na CCM ikiwa yatazingatia maoni yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba.
"Tutafanya kazi na wajumbe wote walioteuliwa na Rais, hatutawabagua kwasababu wametokea vyama gani, hapana, ila tunachokitahadharisha ni kwamba wajumbe wote wataweka masuala ya taifa mbele na hawataendekezwa na itikadi za vyama vyao.

No comments:

Post a Comment