MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, amesema kuwa kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya Operesheni Tokomeza Ujangili hazijulikani zilipo.
Alisema kuwa hatua hiyo imesababisha askari zaidi ya 2,000 waliounda kikosi maalumu kwa ajili ya operesheni hiyo ambayo imesitishwa kwa muda kuanza kudai posho zao.
Lembeli aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati kamati hiyo ilipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) kwa ajili ya kujionea namna hifadhi hiyo ilivyofanikiwa kudhibiti uharibifu wa mazingira na kutunza bioanuai ya eneo la ukanda wa hifadhi ya nusu maili.
Alisema kuwa hadi sasa kiasi cha sh bilioni 1.5 za posho hizo hakijalipwa kwa askari hao.
Lembeli alisema katika operesheni hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwaka 2013 na baadaye kusitishwa Novemba mosi, serikali ilikuwa imetenga zaidi ya sh bilioni 3.5, lakini inashangaza kuambiwa kuwa askari bado wanadai posho zao.
Alisema baada ya operesheni hiyo kusitishwa kutokana na ripoti ya kamati yake iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana bungeni, askari hao bado walikuwa wakiendelea na kazi huku wakisubiri kuanza kwa awamu ya pili ya operesheni hiyo.
“Serikali ilitenga zaidi ya sh bilioni 3.5 zitumike katika Operesheni Tokomeza, inashangaza sana kuambiwa kuwa askari wale wanaendelea kusotea posho zao hadi sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa Lembeli, kusitishwa kwa operesheni hakukumaanisha kwamba ndiyo ukomo wake, kwani askari waliendelea kulinda usalama wa maeneo yale, na kwamba katika kazi hiyo ambayo wameifanya kwa moyo mmoja hadi sasa, walitakiwa kulipwa stahili zao.
Askari walioshiriki operesheni hiyo ni wanajeshi 480 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), polisi 440, wamo pia askari 440 kutoka Kikosi dhidi ya Ujangili (KDU), askari wa wanyamapori kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Usalama wa Taifa.
Wengine ni askari 99 kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na askari wanyamapori 51 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Alisema ili kuondoa sintofahamu hiyo, kamati inashauri kufanyika kwa ukaguzi wa fedha hizo pamoja na serikali kutoa ufafanuzi wa kiasi kilichobaki kwa kueleza sababu za ucheleweshaji wa malipo ya askari hao wakati bajeti hiyo tayari ilikwishapitishwa.
Wakati huo huo, kamati hiyo imekutana na kushauriana na Menejimenti ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) kuhusu viwango vya tozo za utalii kwenye mlima huo.
Waliitaka serikali kulipa fursa shirika hilo kupanga viwango vya tozo za viingilio vya utalii nchini ili kuvifanya viendane na hali halisi ya utalii duniani badala ya utaratibu wa sasa ambao hauipi nafasi Tanapa kupanga viwango hivyo.
“Haya mambo tatizo hapa ni siasa, serikali inatakiwa kuangalia tozo zake na kuacha hadithi ya kunufaisha wafanyabiashara ambao hata hivyo hawalipi kodi.
“Hifadhi ikipewa mamlaka kamili ya kujiendesha lazima nchi ipate faida, lakini kwa staili hii tusipowatetea hawa Tanapa, shirika hili litakufa kama lilivyokufa Shirika la Ndege nchini (ATCL),” alisema.
Ushauri wa Kamati ya Lembeli, unafananishwa na taarifa za serikali ambazo zinaonyesha kwamba kwa sasa mlima Kilimanjaro unaonekana kuzidiwa na idadi ya watalii.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mlima Kilimanjaro kwa mwaka ulikuwa ukipokea wageni 13,000, lakini hivi sasa watalii wanaopanda mlima huo ni zaidi ya 50,000 huku wapagazi wakidaiwa kuwa zaidi ya 200,000 kwa mwaka.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi, alisema shirika hilo limeweka mikakati ya kuona njia mbadala ya kupunguza idadi ya watu wanaopanda mlima ambapo tayari wameshaanza kuwasiliana na vyama vya wafanyabiashara ya uongozaji wa utalii kuhusu mpango huo.
Kuhusu eneo la hifadhi ya nusu maili, Kijazi alisema Tanapa imeandaa mpango utakaohakikisha ukanda huo unasimamiwa na kupunguza uharibifu wa mazingira kikamilifu ambapo rasimu ya muongozo huo imeshaandikwa.
No comments:
Post a Comment