UMOJA wa Ulaya umezindua ripoti ya kwanza ya juhudi za kupambana na rushwa, huku ikionesha rushwa ipo kila mahali. Ripoti hiyo inabainisha hali katika nchi anuai na kutoa ushauri wa namna ya kupambana na rushwa.
Msemo wa ‘Rushwa ni adui wa haki’ umezoeleka zaidi katika nchi zinazoendelea. Lakini hata kwenye nchi zilizoendelea, rushwa bado ni tatizo sugu. Akizindua ripoti hiyo, Kamishna wa Mambo ya Ndani wa Umoja huo, Cecilia Malmström, alionesha ukubwa wa tatizo hilo katika mataifa ya Ulaya.
“Ripoti hii inaonyesha wazi kwamba kiwango cha rushwa kinatofautiana kati ya nchi moja na nyingine lakini inaonyesha pia kuwa rushwa inaathiri nchi zote mwanachama. Hakuna sehemu isiyo na rushwa Ulaya,” alisema Malmström.
Inakadiriwa kwamba kila mwaka rushwa inaugharimu uchumi wa Umoja wa Ulaya kiasi cha Euro billioni 120. Kiasi hicho ni sawa na bajeti ya Umoja wa Ulaya kwa mwaka mzima. Ripoti iliyozinduliwa imefanya tathmini ya hali ya rushwa katika nchi mwanachama lakini haikuishia hapo tu bali imetoa pia ushauri wa hatua za kuchukuliwa ili kutokomeza rushwa. “Sheria zilizopo hazitiliwi mkazo na vile vile bado hakuna nia ya kweli ya kutokomeza rushwa.”
Kila mwaka, shirika la kimataifa la kupambana na rushwa Transparency International, linatoa orodha ya nchi zinazofanya vizuri katika kupambana na rushwa. Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinaonekaa kuwa kielelezo bora.
Kwa mfano Denmark inayoongoza kwenye orodha hiyo. Ujerumani imeshika nafasi ya 12. Lakini zipo pia nchi zilizogubikwa na rushwa. Ugiriki kwa mfano iko kwenye nafasi ya 80 na hivyo, kwa mujibu wa orodha ya Transparency International, nchi za Kiafrika kama Ghana na Rwanda zimefanikiwa kudhibiti rushwa kuliko Ugiriki.
Miongoni mwa maeneo ambapo rushwa imesambaa Ulaya ni katika michango kwa vyama vya siasa. Nchini Ujerumani kwa mfano, chama cha siasa lazima kiweke wazi jina la mtu au kampuni inayotoa mchango wa zaidi ya Euro 50.000. Michango iliyo chini ya kiwango hicho inaweza kutolewa kisirisiri. Kwa chama cha kisiasa kupokea mchango si sawa na kupokea rushwa lakini msemaji mmoja wa Transparency Internatioal anaelezea hatari iliyopo.
“Fedha za michango zinatoa upenyo kwa chama kupitisha maamuzi si kwa manufaa ya umma bali kwa kuwanufaisha waliotoa mchango na kwetu hii ni sawa na rushwa,” msemaji Ronny Patz ameiambia DW.
Transparency International imekosoa kuwa ripoti ya Umoja wa Ulaya haijagusia tatizo la rushwa katika taasisi za Umoja huo. Hivyo shirika hilo litachapisha ripoti yake Aprili mwaka huu na kuelezea tatizo la rushwa ndani ya taasisi za Umoja wa Ulaya. Hata hivyo, Transparency International imeeleza kuwa mafanikio ya ripoti hii yataonekana katika siku za usoni.
“Swali kubwa ni iwapo nchi mwanachama zitafuata ushauri uliyotolewa katika ripoti juu ya namna ya kupambana na rushwa,” amesema Patz.
Zaidi ya asilimia hamsini ya raia wa Umoja wa Ulaya wamesema kwamba wanahisi rushwa inazidi kuongezeka katika nchi wanayoishi. Ripoti mpya ya Umoja wa Ulaya itakayotolewa mwaka 2016 itaonyesha iwapo Umoja huo umefanikiwa kupiga hatua na kupambana na adui adui huyu wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment