Saturday, February 8, 2014

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Yatangaza Uwepo wa Homa ya dengue

Wizara ya Afya Yatangaza Uwepo wa Homa ya dengue
Wizara ya Afya Yatangaza Uwepo wa Homa ya dengue

Na Mwandishi Wetu
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya dengue yaani “dengue fever” nchini Tanzania. Ugonjwa huu umethibitishwa baada ya sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliohisiwa kuwa na ugonjwa huu jijini Dar es salaam kupelekwa kwenye maabara ya Taifa Dar es salaam na kukutwa na virusi vya homa ya dengue mnamo mwishoni mwa mwezi wa Januari.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja kwa vyombo vya habari leo, alisema hadi sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 21 na hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha. 
Akifafanua zaidi alisema homa ya dengue ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu wa aina ya Aedes na dalili za ugonjwa huu ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. “Dalili hizi huanza kujitokeza kuanzia kati siku ya 3 na 14 tangu mtu alipoambukizwa kirusi cha homa ya dengue. Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo basi wananchi wanaombwa wakati wakipata homa kuhakikisha wanapima ili kugundua kama wana vimelea vya malaria ua la ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema Mwamwaja.
Alisema mbu hao hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu au hata ndani ya nyumba. Viluwiluwi vya mbu hawa huweza kuishi katika mazingara ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu. Mbu hawa huwa na tabia ya kuuma wakati wa mchana.
“…Ugonjwa huu hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine. Homa ya dengue inaweza kutibika kama mgonjwa atapelekwa hospitali mapema na kupatiwa matibabu ya haraka. Hakuna tiba maalumu ya ugonjwa wala chanjo bali mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa, kupungukiwa maji au damu. Endapo mgonjwa atachelewa kupatiwa matibabu, mgonjwa anaweza kupoteza maisha,” alisema Mwamwaja.
Aidha akizungumzia namna ya kujikinga na ugonjwa huo, alisema wananchi wanatakiwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo, kuondoa vitu vyote vinavyoweza kuweka mazalio ya mbu kama vile, vifuu vya nazi, makopo, magurudumu ya magari yaliyotupwa hovyo na kfyeka vichaka vilivyo karibu na makazi ya watu.
Njia nyingine ni pamoja na kuhakikisha maua yandayopandwa kwenye makopo au ndoo hayaruhusu maji kutuama, kufunika mashimo ya maji taka kwa mfuniko imara, kusafisha gata za paa la nyumba ili kutoruhusu maji kutuama, kujikinga na kuumwa na mbu na pia kutumia dawa za kufukuza mbu “mosquito repellants”.
Wananchi wanashauriwa kuvaa nguo ndefu kujikinga na kuumwa na mbu, kutumia vyandarua vyenye viuatilifu (hata kwa wale wanaolala majira ya mchana) na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi.
Hata hivyo alisema tayari Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanza kuchukua hatua kukabiliana na homa ya dengue, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya tahadhari ya ugonjwa kwa Waganga Wakuu wote wa Mikoa na Wilaya kwa Tanzania Bara kupitia Makatibu Tawala na Wakurugenzi na kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo kupitia kwa Wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na maeneo ya mipakani.
Aidha alisema uchunguzi wa ugonjwa huo utafanyika kwenye Mikoa na Wilaya zitakazoonekana kuwa na ongezeko la wagonjwa wenye homa. Wizara inatumia vipeperushi katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa. 
Hatua zingine ni pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya na mipakani wa namna ya kutambua na kujikinga dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu pamoja na uchukuaji wa sampuli iwapo mgonjwa atapatikana, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa, ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa dengue uliopo kwenye vituo maalumu ‘Sentinel Surveillance Sites’.

Mara ya kwanza kugundulika kuwepo kwa ugonjwa huu nchini ilikuwa ni Juni 2010 mkoani Dar es salaam ambapo idadi ya watu waliothibika kuwa na ugonjwa ilikuwa 40, pia kati ya mwezi Mei hadi Julai 2013, wagonjwa 172 walithibitishwa kuwa na ugonjwa huu. Hakuna mgonjwa yeyote aliyepoteza maisha. 
Wizara inasisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini. Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huu.

No comments:

Post a Comment