Tuesday, February 18, 2014

KIFICHO AWA MWENYEKITI WA MUDA WA BUNGE LA KATIBA


Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Ameir Pandu Kificho  (pichani) amechaguliwa leo kuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katibam mjini Dodoma.

CCM YAWAPA ONYO WANAOJITANGAZIA URAIS KABLA YA WAKATI


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye akionesha kitabu cha maadili yanayotakiwa kufuatwa na wanaCCM alipokuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu onyo walilopewa makada wa CCM wanaodaiwa kutangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda kuwadia. Makada hao waliohojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ya chama hicho ni; Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa,  Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Januari Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, Wiliiam Ngeleja  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira. Makada hao watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 12. (PICHA NA RICHARD MWAIKENDA)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kati ya tarehe 13/02/2014  na tarehe 18/02/2014 kumekuwa na mfululizo wa vikao kadhaa vya Chama kitaifa vilivyoshughulikia suala la maadili ndani ya Chama.
Vikao hivyo ni pamoja na Kamati Ndogo ya Udhibiti tarehe 13-14/02/2014, Tume ya Udhibiti na Nidhamu 18/02/2014 na Kamati Kuu tarehe 18/02/2013.
Waliohojiwa katika mfululizo wa vikao hivi ni wafuatao:-
1. Ndg. Frederick Sumaye
2. Ndugu Edward Lowasa
3. Ndugu Bernard Membe
4. Ndugu Stephen Wassira
5. Ndugu January Makamba
6. Ndugu William Ngeleja
Baada ya kuwahoji ilithibitika kuwa baadhi ya tuhuma dhidi yao ni za kweli na hivyo kupendekeza adhabu.  Mapendekezo hayo yalipelekwa kwenye Tume ya Udhibiti na Nidhamu na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu kwa wahusika.
Kwa ujumla waliohojiwa wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo:-
1. Walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
2. Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.  Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo.


Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya ONYO KALI na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi.
Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni:-
“Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.”
Kamati Kuu imeitaka pia Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe) kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja Kanuni za Chama.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.

Imetolewa na:-


Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI,
18/02/2014

Monday, February 17, 2014

RAIS KIKWETE AZINDUA SERA YA MTANDAO WA VIKUNDI VYA MAADILI NA UCHUMI TZ (MVIMAUTA)


 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na vijana baada  ya kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)  iliyoasisiwa na   Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission  International  na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam  Jumamosi, Februari 15, 2014
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akinyanyua juu kitabu baada ya kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)  akiwa na mwasisi wake  Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission  International  na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam  Jumamosi, Februari 15, 2014
 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakati wa  kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)  iliyoasisiwa na   Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission  International  na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam  Jumamosi, Februari 15, 2014.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na msanii wa vichekesho ambaye  pia ni mhubiri  na mwimbaji wa nyimbo za injili Emmanuel Mgaya maarufu kama Masanja Mkandamizaji  baada ya kuzindua Sera ya Mtandao wa Vikundi vya Maadili na Uchumi Tanzania (MVIMAUTA)  akiwa na mwasisi wake  Askofu Mkuu Sylvester Gamanywa, Mwangalizi Mkuu wa Kitaifa, wa WAPO Mission  International  na Mwasisi wa Maono ya Harakati za Maadili kwa Kizazi Kipya katika ukumbi wa BCIC Mbezi Beach jijini Dar es salaam  Jumamosi jana. Picha na IKULU

DODOMA YAFURIKA, WAJUMBE WAWASILI VYUMBA VYAADIMIKA

dodomapix_64492.png
Na Elizabeth Edward na Hebel Chidawali, Mwananchi
Dar es Salaam/Dodoma.Wakati Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwasili mjini Dodoma, Ofisi ya Bunge imetangaza kuandaa utaratibu wa malazi kwa wajumbe hao katika hoteli mbalimbali mjini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, jumla ya hoteli 27 zimeainishwa kuwapokea wajumbe hao 640 ambao wanatarajiwa kuwapo mjini Dodoma kwa muda wa miezi mitatu.
Pamoja na utaratibu wa malazi, taarifa hiyo pia iliagiza wajumbe hao kuwasili wakiwa na nakala halisi za vitambulisho vitakavyotumika kwa ajili ya usajili.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa usajili utafanyika leo na kesho kwenye Ofisi za Bunge, ambapo zoezi hilo litajumuisha ujazaji wa fomu, upigaji picha za vitambulisho sambamba na kukabidhiwa vitendea kazi.
Baada ya zoezi hilo Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi watakutana na wajumbe kwa ajili ya kutoa maelekezo ya awali yanayohusiana na utaratibu wa ukaaji, jiografia ya viwanja vya Bunge na huduma za utawala.
Kikao cha kwanza cha mkutano huo kitafanyika Jumanne ijayo, ambapo pamoja na masuala mengine kitahusisha uchaguzi wa mwenyekiti wa muda atakayesimamia upitishwaji wa kanuni na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge hilo.
Wiki iliyopita Ikulu ilitangaza majina ya wajumbe 201, yaliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushiriki katika uchambuzi wa Rasimu ya Pili ya Katiba na kutengeneza Katiba Mpya.
Mbali ya wajumbe wa Bunge la Katiba, pia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wako Dodoma wakiendelea na vikao vyao.
Mji wafurika wageni
Kutokana na kuwapo kwa ugeni huo, Mji wa Dodoma umefurika wageni wakiwamo wajumbe wa Bunge la Katiba na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) huku, maeneo mengi yakionekana kufanyiwa usafi.
Hata hivyo, wageni wengi walionekana kuingia jana na baadhi ya watumishi wa hoteli hizo walikiri kuwasajili baadhi ya wageni, ambao wapo katika orodha hiyo.
Gazeti hili jana lilishuhudia kukiwa na maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mapokezi hayo, huku baadhi ya maeneo yakiendelea kukarabatiwa ikiwamo kupaka rangi.
Moja kati ya maeneo ambayo wageni wengi wamepangwa kufikia ni Hoteli ya New Dodoma ambayo imepangiwa vyumba 87.
Katika eneo la hoteli hiyo, jana kulikuwa kukifanyika usafi wa hali ya juu ikiwemo kupata rangi, kusafisha maji kwenye bwawa la kuogelea, kupulizia dawa baadhi ya maeneo na katika bustani ikiwamo kufagia paa la juu upande wa vibanda.
Hoteli nyingine ambayo kulikuwa na usafi katika kumbi zake pamoja na mandhari ya nje ni Fifty Six

MEMBE: TULIKAANGWA, TULIULIZWA MASWALI MAGUMU URAIS 2015

jpg_28028.jpg
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka nje ya ukumbi wa mahojiano na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula kuhusu mbio za urais 2015.
Akizungumza jana mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, Membe alisema kamati hiyo inauliza maswali magumu kuhusu wanayoyafanya pamoja yanayofanywa na mashabiki wao.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amesema aliulizwa maswali mazito na Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula kuhusu mbio za urais 2015.
Akizungumza jana mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, Membe alisema kamati hiyo inauliza maswali magumu kuhusu wanayoyafanya pamoja yanayofanywa na mashabiki wao.
"Kamati inauliza maswali mazito na magumu yanayohusiana na uvunjaji wa maadili ya uongozi wa chama chetu... Kamati ya maadili imejipanga vizuri sana wala msidanganyike, wanauliza maswali mazito," alisema Membe.
Membe aliongeza kusema aliulizwa mambo makubwa matatu, kubwa likiwa ni kuibuka ghafla kwa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila wakati chama hicho kinapokaribia kwenye uchaguzi wa Rais.
"Kuna mambo makubwa matatu ambayo kamati ya maadili imeyauliza. Kubwa kabisa ni uzukaji ghafla wa makundi makubwa ambayo yanazaliwa kila wakati wanapodhani mtu fulani anafaa kuwa kiongozi."
Alisema na kuongeza: "Suala la pili nililoulizwa ni tunafanyaje kukifanya chama chetu kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani kwenye uchaguzi?"
Suala la tatu ambalo wajumbe wa kamati hiyo wanauliza ni suala la fedha, kama msingi wa ushindi na kuhoji inakuwaje mtu atumie mamilioni au mabilioni ya shilingi kununua uongozi?
Membe alisema hayo ndiyo maeneo matatu ambayo kamati hiyo ya maadili imekuwa ikiyauliza na kusema kuna uwezekano mkubwa wa wanachama zaidi kuitwa kuhojiwa.
Alisema alitumia fursa hiyo kukishauri chama mambo kadha wa kadha ikiwamo CCM kufanya mchakato wa kumteua mgombea au wagombea urais mwaka huu ili waweze kujulikana kabla ya Desemba.
Kamati hiyo ya ndogo ya Maadili ya CCM iliyoanza kikao chake Alhamisi iliyopita, imewahoji makada sita wa chama hicho ambao wamekuwa wakitajwa kuanza kutangaza nia za kuwania kupendekezwa kupeperusha bendera yake kwenye kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Tayari kamati hiyo imeshawahoji Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye kwa kile kilichokuwa kikielezwa kuwa wanakivuruga chama kwa kuonyesha nia ya kuwania urais kabla ya muda ulioruhusiwa na chama hicho.
Pia kikao hicho kimewahoji Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

ARSENAL YAICHAPA LIVERPOOL 2-1

afc_c48cb.jpg
Washika bunduki kutoka jiji la London maarufu kama ''The Gunners'' jana waliitandika timu ya Liverpool jumla ya magoli 2-1 katika mchezo wa kombe la FA na kujihakikishia kutinga hatua ya robo fainali za kombe hilo, Arsenal ilipigwa jumla ya magoli 5-1 mara ya mwisho ilivyokutana na timu hiyo katika mtanange wa ligi kuu ya Uingereza; hivyo jana ililipa kisasi na kuwatoa Liverpool katika kinyang'anyiro cha kombe hilo.
Goli la kwanza la Arsenal lilifungwa na Oxlade-Chamberlain katika dakika ya 16 ya mwanzo wa mchezowakati goli la pili likifungwa na Lukas Podolski na baadae timu ya Liverpool ilipata goli kwa njia ya Penati kupitia kiungo wake Steven Gerrard.
Japokuwa Mwamuzi wa mchezo huo '' Howard Webb'' ambaye atachezesha baadhi ya michezo ya kombe la dunia mwaka huu; alionekana tupowapa Liverpool penati ya wazi baada ya mshambuliaji wake Luis Suarez kuchezewa rafu mbaya ndani ya dimba la Arsenal na Oxlade-Chamberlain wa timu hiyo.
Arsenal itavaana na timu ya Everton katika hatua ya robo fainal ya kombe hilo la FA.

MAPACHA WALIOUNGANA KUMALIZA KIDATO CHA NNE MWAKA HUU



Mapacha wawili walioungana kiwiliwili, Maria Mwakikuti (kushoto) na Consolata Mwakikuti (kulia) wakila chakula katika hafla ya kuwapongeza kwa kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010 katika hospitali ya misheni Ikonda Makete 

Aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Getrude Mpaka akiwapa zawadi ya vitabu mapacha wawili walioungana kiwiliwili, Maria Mwakikuti (kushoto) na Consolata Mwakikuti (kulia) baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba mwaka 2010 
WENGI wamesikia historia ya wale mapacha walioungana kiwiliwili; baada ya kimya chao cha muda mrefu wengi watapenda kujua wako wapi na wanafanya nini?

Wanafunzi hao Maria Mwakikuti na Consolata Mwakikuti wanasoma shule ya sekondari ya Nyota ya Asubuhi iliyopo Kidabaga, wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Uongozi wa shule umeweka masharti magumu kidogo ili kukutana nao, lakini mtandao huu unaendelea kuwasiliana na uongozi wa shule hiyo ili watanzania waweze kujua maendeleo yao.

Kwa wasiofahamu mapacha hao, ni wenyeji wa wilaya ya Makete mkoani Njombe; wilayani humo wanaishi katika kijiji cha Ikonda, hapo ndipo walipozaliwa na kumalizia elimu yao ya msingi.

Walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja walisema wanataka kuwa wataalamu wa kompyuta.

Miaka mitatu sasa imepita toka wawakilishi wa mtandao huu wakutane nao katika hafla ya kuwapongeza baada ya kufaulu vizuri mitihani yao ya darasa la saba.

Wapo kidato cha nne katika shule hiyo ya Nyota ya Asubuhi; walijiunga na shule hiyo baada ya walezi wao kukataa wasijiunge na shule ya sekondari ya Jangwani walikokuwa wamepangiwa baada ya matokeo yao kutoka

Hivi sasa wana miaka 17. wanaukaribia utu uzima, kwa vyovyote watakuwa na mengi ya kuzungumza kuhusu maisha yao ya sasa, elimu yao, changamoto wanazopata na matarajio yao ya baadaye.

Sunday, February 16, 2014

CHADEMA YATISHIA KUSUSIA BUNGE

chadema-mnyika1_c4b47.jpg
Zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba mjini Dodoma, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitasusia bunge hilo, iwapo mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba hayatazingatiwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati alipokuwa akitoa taarifa ya Mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho uliofanyika juzi, kuzungumzia Bunge la Katiba, uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga na uamuzi kuhusu madiwani wake mkoani Arusha.
Mbowe alisema Chadema wanakwenda kushiriki bunge hilo wakiwa na masikitiko kwa kuwa uteuzi wa wajumbe 201 uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete haukuwa na nia njema kwa taifa, kwani asilimia 80 ya walioteuliwa ni wanachama wa CCM. "Tunakwenda Dodoma lakini hatutakubali Bunge limilikiwe na wachache na hatutasita kurudi kwa wananchi tutakapoona mapendekezo ya Jaji Warioba hayatekelezwi," alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa Chadema hawaendi bungeni kugoma ila wananchi wasishangae watakapoona wanatoka ndani ya Ukumbi wa Bunge hilo, kwa kuwa lengo la uteuzi wa wajumbe lilikuwa ni kutaka kupata wabunge wengi watakao unga mkono CCM.
"Kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano, CCM tayari wana wajumbe karibu asilimia 80, katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wana wajumbe karibu asilimia 68, kwa hiyo wanaweza wakakidhi vigezo vya mshindi kupatikana kwa theluthi mbili ya kura zilizopigwa kufanya uamuzi kwa niaba ya Bunge la Katiba," alisema Mbowe.
Hata hivyo, alisema Chadema hakitajali maoni yatakayotolewa na CCM ikiwa yatazingatia maoni yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba.
"Tutafanya kazi na wajumbe wote walioteuliwa na Rais, hatutawabagua kwasababu wametokea vyama gani, hapana, ila tunachokitahadharisha ni kwamba wajumbe wote wataweka masuala ya taifa mbele na hawataendekezwa na itikadi za vyama vyao.

Uvumilivu una mwisho Tumekubaliana kuacha unyonge! Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete awaambia Wajumbe

Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) katika jengo la White House mjini Dodoma leo, akiwa meza kuu na Makamu wa Rais wa CCM visiwani na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein, na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana. (picha: Ikulu)
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) katika jengo la White House mjini Dodoma leo, akiwa meza kuu na Makamu wa Rais wa CCM visiwani na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein, na Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana. (picha: Ikulu)

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amewataka wanachama wake kuacha unyonge na kujibu mapigo ya wapinzani hasa wale ambao wanaendesha siasa za vurugu katika kampeni za chaguzi mbalimbali nchini.

Rais Kikwete amesema kuwa uvumilivu una ukomo, na kwamba sasa wanachama wa CCM hawana budi kuacha unyonge, kutokana na siasa hizo za vurugu zinazoendeshwa na vyama vya upinzani.

Aliyasema hayo jana mjini hapa wakati akifungua kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kitakachokutana kwa siku mbili chini ya uenyekiti wake, ambacho ajenda kuu ni kuzungumzia Bunge Maalumu la Katiba.
“Tumelizungumzia hili katika Kamati Kuu, tumekubaliana kuacha unyonge (makofi). Ndiyo
 watu wamelisema hili katika Kamati Kuu, tumesema jamani tumekubaliana kuacha unyonge,”
“Wacha wakaseme (waandishi wa habari), ndio tumekubaliana kuacha unyonge. Kabisa. Hata kama leo katika taarifa za habari, zisiwekwe habari nyingine, msikike ninyi tu. Uvumilivu una ukomo wake.”
alisema Rais Kikwete ambaye wakati anafungua kikao hicho waandishi wa habari walikuwamo.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema wamefikia hatua hiyo kwa sababu yanayotokea yanasikitisha sana na akatoa mfano wa matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani katika kampeni katika maeneo ya Igunga mkoani Tabora na Kahama mkoani Shinyanga.
“Maana tunashindana na wenzetu wagomvi maana wao ugomvi ndio sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa. Maana pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Acheni unyonge (makofi).
“Nasema kwa kweli kwa sababu yanayotokea yanasikitisha. Pale Igunga kijana yule wamemmwagia tindikali, pale Kahama kijana wamemtoa macho kwa bisibisi. Tuache unyonge,”
alisisitiza Rais Kikwete huku akishinikizwa kwa shangwe za CCM Oyee, Mapinduzi Daima.

Ingawa Rais Kikwete hakutaja chama, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekuwa kikihusishwa na vurugu za uchaguzi katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Igunga na Kahama katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika hivi karibuni na pia katika chaguzi ndogo za ubunge.

Akizungumzia uchaguzi mdogo wa kata 27 zilizofanyika hivi karibuni na CCM kuzoa kata 23, Rais Kikwete aliwapongeza wanaCCM kwa ushindi huo, lakini akawapa changamoto ya kuhakikisha wanarejesha kata hizo nne zilizokwenda kwa vyama vya upinzani.
“Huu ni ushindi mkubwa sana, ushindi mnono. Ni vizuri kutumia nafasi hii kujipongeza na kuwapongeza wenzetu kwa kazi nzuri, kazi nzuri waliyoifanya ya kujenga chama,”
“Lakini tukumbushane kwamba kata nne hatukuzipata, hivyo tuna kazi ya kuzikomboa, sisi wakati wote nia yetu ni kushinda, kushindwa haiwezekani.”
alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Aidha, alizungumzia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, akisema hadi sasa hali ni shwari, hakuna migawanyiko wala misukosuko kama ilivyokuwa kwa Jimbo la Arumeru Mashariki ambalo alisema tangu mwanzo hadi mwisho, hali haikuwa shwari.

Alisema hadi sasa wana uhakika wa ushindi katika jimbo hilo, lakini akawataka wanaCCM kujiandaa vyema kwa kila hali na kuhakikisha ushindi unapatikana katika jimbo lililoachwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa. Mwanawe Geoffrey ndiye mgombea wa CCM.

Pia aliwataka wanachama na viongozi wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, nao kujiandaa kwa uchaguzi mdogo kwa sababu tayari Spika wa Bunge, ametoa taarifa serikalini kuhusu kuwa wazi kwa jimbo hilo kutokana na kifo cha mbunge wake, Said Bwanamdogo.
“Msikae tu kusubiri na kuendelea kuomboleza, kwa sababu Serikali haiombolezi, wao wanachotaka ni uchaguzi ujazwe, shughuli ziendelee. Maana watu wanaweza kusema hata orobaini bado. Kule Arumeru tuliambiwa tumbo bado halijapasuka. Kwani kwa Mgimwa orobaini tayari, mbona mchakato umeanza.
“Ninyi fanyeni mchakato, orobaini yetu mnaweza kufanya wakati mambo mengine yakiendelea. Tujiandae mapema ili kuhakikisha tunashinda,”
alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na kuwapongeza viongozi wa mkoa na wilaya waliofanikisha ushindi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki ambako mgombea wao, Mahmoud Thabit Kombo alishinda.

Alisema CCM ilibidi kumtosa aliyekuwa mbunge wao, Mansour Yussuf Himid, kwa sababu alikuwa akivaa magwanda ya chama hicho, lakini alikuwa akipinga sera na taratibu za chama hicho tawala.
“Kila akifungua mdomo wake anaitukana CCM, kila akifungua mdomo anapingana na sera za CCM. Tukasema inatosha, bora kuwa na mpinzani huko nje kuliko huyu, ndio maana niliwahi kusema katika NEC moja hapa kuwa sijui mtu anasema nitahama CCM, nikasema nendeni sasa hivi,”
alisema Kikwete.

FUNDI SAMWELI ATHIBITISHA KUACHANA NA MKEWE MWANAMUZIKI SARAHA










Producer wa wimbo mpya wa Ben Pol, ‘Unanichora’, Fundi Samwel ambaye ni raia wa Sweden, amethibitisha kuachana na mke wake, Saraha.

Mtayarishaji huyo amesema sababu kubwa ya kuachana ni ubusy waliokuwa nao uliosababishwa na muziki na hivyo kuwafanya wasiwe karibu kwa kipindi kirefu.

“Mimi na Saraha tuliachana, kilikuwa kitu kibaya kwangu na kwake pia ndio maana nilikuwa kimya kidogo mwaka huu sababu unajua moyo ulivunjika sana na mood lazima ipotee,” Fundi Samwel amemuambia Sam Misago kwenye kipindi cha Power Jams cha East Africa Radio.

“Unajua kukaa na kufanya muziki lazima utumie muda sana na unatumia akili sana, na hata yeye alifanya kazi nzuri hapa, alikuwa busy sana, namimi nilikuwa busy ya studio. Unajua anakuta foleni kila siku halafu wewe unapiga kazi kama masaa 15 hivi and then unachoka sasa huwezo kuongea vizuri. Hata Saraha alichoka, unajua tulishindwa kuongea vizuri na kitu kiliendelea. And then tulipofika Sweden, unajua upendo uliisha tu, uliisha kabisa,” aliongeza.

Samwel ambaye tayari amerejea kwao nchini Sweden amesema yupo Tanzania kwa wiki mbili kutengeneza nyimbo kadhaa

KASHFA YA NGONO CBE...HUYU NDIO PROFESA ALIYETIMULIWA KAZI KWA KUJIHUSISHA NA NGONO NA WANAFUNZI


Profesa Emanuel Mjema
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), tawi la Dar es salaam, kimemfukuza kazi mhadhiri wa chuo hicho anayedaiwa kuhusika na vitendo vya ukiukaji wa maadili ikiwamo kufanya ngono. Mhadhiri huyo ambaye jina halikutajwa alinaswa na kamera za kisasa za kurekodi matukio za CCTV zilizofungwa kwenye vyumba vya madarasa ili kudhibiti nidhamu,miongoni mwa wanafunzi na wahadhiri.
Kamera hizo zimefungwa kwenye vyumba vya madarasa 20 ili kudhibiti vitendo vya ngono baina ya walimu na wanafunzi, wizi wa mitihani na matendo mengine yanayovunja sheria.

Hayo yalibainishwa jana jijini na mkuu wa chuo hicho, Profesa Emanuel Mjema (pichani), alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene.   

Profesa Mjema, alisema, walifikia maamuzi ya kuweka kamera hizo za kisasa ndani ya madarasa Aprili mwaka jana baada ya kujiridhisha na taarifa za kuwapo matukio ya ukosefu wa maadili miongoni mwa wahadhiri ikiwa ni pamoja na kutoa alama za juu kwa baadhi ya wanafunzi wa kike baada ya vitendo vya ngono. 

“Nilipoingia chuoni hapa Januari mwaka jana, nilisikia kuwa kuna baadhi ya wahadhiri wamekosa maadili, wanatoa alama za juu kwa wanafunzi wa kike kwa masharti hata kama hawajafaulu kwa kiwango hicho. Nikaona vyema tuweke vifaa hivyo ili kudhibiti vitendo hivyo,” alifafanua Profesa Mjema.
 
Alieleza kuwa baada ya kuweka kamera hizo 20 kwa kila darasa kuwa na kamera moja, walifanikiwa kumnasa mwalimu mmoja kwa kitendo cha kukiuka maadili yake ya kazi na kumfukuza kazi.
Alisema kuwa, kamera hizo pia, zinasaidia kuwadhibiti wanafunzi wenye tabia ya kuiba mitihani, kwani mikakati iliyopo hata wakufunzi na wanafunzi hawajui anayetunga mitihani ili mradi ipo ndani ya silabasi ya chuo. 

Kamera hizo zinadaiwa kuwa na uwezo wa kumvuta karibu mwanafunzi aliyeko darasani na kujua anachokiandika, pia mhadhiri iwapo anachokifundisha ni cha ukweli au anadanganya kwa hiyo zinatumiwa wakati wote kwenye vipindi na mitihani.

Alisema, chuo kimeajiri walinzi kwa ajili ya kuwadhibiti wanafunzi ambao wanavaa nguo ambazo hazina maadili mazuri na pia hukagua vitambulisho wanapofika getini, lengo likiwa ni kukifanya chuo hicho kubakia katika heshima yake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mbene, alipongeza jitihada hizo zilizofanywa na chuo hicho, huku akikemea vikali tabia inayofanywa na baadhi ya wahadhiri hao, akiongeza kuwa, ni lazima mwanafunzi apewe madaraja ya matokeo ya mitihani kutokana na ufaulu na uwezo wake.  
Pia, aliahidi kushughulikia suala la uvamizi wa eneo la chuo hicho pamoja na maombi ya kuongezewa madarasa ikiwa ni pamoja na kupewa majengo ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa (NFRA).

Friday, February 14, 2014

HISTORIA FUPI YA SIKU YA WAPENDANAO AU VALENTINE'S DAY

images_1_da39a.jpgimages_2_d7b4a.jpg
Na mabantanyau family
Februari 14 wapendanao duniani huitumia siku hii kusherehekea na wapendwa wao wakijumuika kula na kunywa. Mjengwa blog tunakuletea historia fupi ya siku hii ya wapendanao aka Valentine's day
Asili ya siku ya wapendanao "Valentine's Day" ni St Valentine, mhubiri wa kikristo aliyekuwa akiishi karibu na mji wa Roma katika karne ya tatu wakati wa utawala wa Claudis II.
Claudis alitaka awe na jeshi kubwa akategemea vijana wangejitolea na kujiunga na jeshi lake.
Lakini vijana wengi hawakupenda vita kwakuwa hawakutaka kuziacha familia zao na watoto wao.
Claudis akafikiria akaona hawa vijana kuwakomesha waingie jeshini ni kupiga marufuku watu kuoana.Kuanzia hapo akapiga marufuku watu kuoana akitegemea vijana hawatajali sasa kujiunga na jeshi kwasababu ya familia zao.
Askofu Valentine naye kwa siri akawa anawafungisha ndoa vijana hao kwa siri.
Claudius aliposikia habari hizo aliamuru Valentine akamatwe na akahukumiwa adhabu ya kifo cha kunyongwa.
Wakati akiwa jela akisubiri siku yake ya kunyongwa Valentine alikuwa akitembelewa na vijana waliokuwa wakimpelekea maua kuonyesha wako pamoja nae.
Mmoja wa vijana waliokuwa wakienda kumtembelea ni mtoto wa mkuu wa gereza ambaye aliruhusiwa kuingia mpaka kwenye selo la Valentine "kupiga naye stori".
Inasemekana kwamba Valentine aliangukia katika mapenzi na binti huyo wa mkuu wa gereza wakati anasubiria kunyongwa.
Inasemekana kwamba muda mchache kabla hajanyongwa Valentine aliomba kalamu na karatasi na kuandika meseji yake ya kuaga akiweka sahihi "From Your Valentine" ( kutoka kwa Valentine wako )
Valentine akanyongwa tarehe 14 februari mwaka 269 AD.
Baada ya kunyongwa kwa Valentine, vijana wa Roma walianza kumuiga Valentine na kuwaandikia na kuwatumia wanawake waliowapenda salamu za mapenzi.
Tangia siku hiyo tarehe hiyo ikaanza kuhusishwa urafiki, upendo na mahaba duniani huku ikihusishwa zaidi na mambo ya mapenzi.
Siku hiyo imezidi kuwa maarufu kila miaka inavyoenda huku huku makampuni yakiigeuza siku hiyo kuwa ya biashara zaidi kwa kufanya kila kitu maalumu kwa siku ya wapendanao kionekane kuwa inabidi kiwe chekundu kuanzia kadi za salamu, maua, mpaka nguo wavaazo wapendanao inabidi ziwe nyekundu.
Kuna watu wengi pia ambao hawasherehekei siku hii kwa kuhoji umuhimu wa kuonyesha kumjali umpendaye katika siku moja tu ya mwaka badala ya siku zote 365.
HAPPY VALENTINE'S

Thursday, February 13, 2014

ARSENAL, MAN U NGOMA DROO

Mshambuliaji wa Arsenal, Olivier Giroud akijaribu kuipa ushindi Arsenal bila mafanikio.
Kipa wa Arsenal Wojciech Szczesny akiondoa mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji wa Man U, Robin Van Persie.
Antonio Valencia wa Manchester United akiokoa hatari golini kwake kwa kichwa

WATU 39 WAUAWA NA BOKO HARAM-NIGERIA

Serikali ya jimbo la Borno lililoko Kaskazini mwa Nigeria, inasema kuwa watu 39 wameuawa katika shambulizi lililofanywa katika mji wa Konduga.Wanawake na watoto ni miongoni mwa watu waliouawa .
Wanamgambo kadhaa waliokuwa wamejihami kwa bunduki waliingia mji wa Konduga kwa kutumia magari makubwa makubwa.
Watu wengi wameukimbia mji wa Konduga, uliopo kilometa zipatazo ishirini na tano kutoka Maiduguri mji mkuu wa jimbo la Borno Maiduguri.
Wanamgambo wa Kiislam wa Boko Haram, wanaofahamika kwa kuendesha harakati zao katika maeneo hayo wamelaumiwa kwa shambulio hilo.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, wanajeshi wa serikali walioko mjini humo, walishindwa kuwathibiti waasi hao hali iliyowalazimu kutoroka.
Watu wapigwa risasi kiholela
Wanamgambo hao wa Kiislamu, waliwapiga risasi watu hamsini na kuteketeza nyumba kadhaa na pia kuna ripoti kuwa waliwateka nyara wasichana wapatao ishirini kutoka kwa chuo kimoja, kilichoko katika eneo hilo.
Wakiongea wakati walipofanya kikao na gavana wa jimbo hilo, raia hao waliokuwa na wasi wasi, walihoji kwa nini maafisa wa ulinzi walichukua muda mrefu kufika eneo hilo baada ya shambulio hilo.
Wanajeshi Nigeria wakishika doria Konduga
Mji huo ulishambuliwa agosti mwaka uliopita na zaidi ya watu arubaini kuuawa, wakati walipokuwa wakielekea msikitini kwa sala za alfajiri.
Katika miezi ya hivi karibuni kumekuwa na mashambulio kadhaa katika maeneo ya mashambani, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo, yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu mia moja.
Mwezi uliopita rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, aliwafuta kazi maafisa wote wakuu wa jeshi, akiwatuhumu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ili kuzuia mashambulio hayo.
Kundi la Boko Haram linaonekana kuwa na wakati zaidi wa kufanya mashambulio katika maeneo kadhaa nchini Nigeria, mashambulio ambayo jeshi la nchi hiyo limekisiwa kushindwa kuyazuia.

Habari Njema Kwa Wana-Yanga Wote Kuhusu Mchezaji Emmanuel Okwi

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limemuidhinisha mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi kuchezea klabu ya Yanga ya Dar es Salaam. Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa ameiambia BIN ZUBEIRY muda huu kwamba, FIFA imewaandikia barua ikiwaambia Okwi ni halali kuchezea Yanga SC. “Suala la Okwi limekwisha, ila siwezi kuzungumza zaidi kwa sasa naingia kwenye kikao, tutatuma taarifa kwa vyombo vya habari baadaye,”alisema Mwesigwa.  

Ruksa; Okwi katikati akiwa na wachezaji wenzake wa Yanga, Juma Kaseja kulia na Hamisi Kiiza kushoto. FIFA imemruhusu kuchezea Yanga.

Januari 22 mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilisimamisha usajili wa Mganda huyo Yanga ili kwanza upatikane ufafanuzi kutoka FIFA juu ya uhalali wake kucheza timu hiyo ya Jangwani akiwa anatambulika kama mchezaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia.
Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji ya TFF iliyokutana Januari 22, mwaka huu kupitia masuala mbalimbali, ilisema imesimamisha usajili huo baada ya kubaini kuwa Okwi aliruhusiwa kuichezea SC Villa ya Uganda kwa kibali maalumu kutoka FIFA. Okwi ambaye aliingia kwenye mgogoro na klabu yake ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliruhusiwa na FIFA kuchezea SC Villa kwa kibali maalumu (provisional permit) cha miezi sita ili kulinda kiwango chake wakati suala lake dhidi ya Etoile du Sahel likishughulikiwa na shirikisho hilo la kimataifa. Kulikuwa kuna kesi tatu FIFA kuhusiana na suala la mchezaji huyo, Okwi ameishitaki klabu hiyo FIFA kwa kutomlipa mshahara, Etoile du Sahel imemshitaki mchezaji huyo kwa utoro. Nayo Simba imeishitaki Etoile du Sahel kwa kushindwa kuilipa ada ya mauzo ya mchezaji huyo ambayo ni dola za Marekani 300,000. Hivyo, TFF iliiandikia FIFA kutaka kujua iwapo mchezaji huyo anaweza kucheza Ligi nchini Tanzania wakati Etoile du Sahel ikiwa imefungua kesi katika shirikisho hilo la kimataifa ikidai Okwi bado ni mchezaji wake na majibu yamewasili TFF Mganda huyo akihalalishwa kuendelea na kazi Yanga

Wednesday, February 12, 2014

Thamani ya Chupa ya Plastic ilivyotoa ajira kwa Vijana Kadhaa Nchini Tanzania


Vijana wamegeuza makazi hapa kwenye eneo la Kukusanyia Chupa chafu za Plastic kwaajili ya Kuziuza Kiwandani,Picha hii imepigwa Ilala Jijini Dsm.Hili ni Sehemu tu ya eneo linalotumika na Vijana walioamua Kujiajiri kuokota Chupa za Plastic mitaa mbalimbali ya Jiji la Dsm na kuzipeleka Kiwandani tena kwaajili ya kuzalisha Chupa Zingine Mpya.Chupa hizi wanaziridisha kiwandani kwa Malipo,Wanapima Kilo ya Mzigo na wanaelewana Bei.Tunafuatilia Kujua Kilo moja ya Mfuko wa chupa za Plastic unauzwa Shilingi ngapi

Mchezaji Emmanuel Okwi alichokiandika kwa Mashabiki Wake


 
Mchezaji wa Kimataifa Emmanuel Okwi amesimamishwa kucheza Soka kwa Muda Kutokana na matatizo ya Uhamisho wake kutoka Simba kwenda Tunisia,Pia Kutoka Tunisia kuja yanga.Hivyo TFF ipo kwenye utaratibu wa Kuhakikisha Mchezaji huyo anapata haki zake na anarejea kwenye Soka kama kawaida yake.

AGIZO LA KUREJESHA MAGARI YA TOYOTA

prius22_b3ff7.jpg
Kampuni ya kutengeza magari ya Toyota nchini Japan, imeagiza kurejeshwa kwa magari milioni 1.9 aina ya Prius katika kiwanda cha magari hayo nchini Japan.
Hii ni kutokana na hitilafu ya kimitambo ambayo inaweza kusababisha gari hilo kukwama.
Gari la Prius ni moja ya magari yenye muundo unaonyesha ubunifu wa hali ya juu wa kampuni ya Toyota.
Gari hilo linaweza kutumia petroli na betri huku likitoa kiwango kidogo sana cha moshi kuliko magari ya kaiwada.
Sasa kampuni hiyo imetambua hitilafu ya programu ya gari hilo ambayo inaweza kusababisha vifaa vya elektroniki vya gari hilo kukwama.
Magari mengi yenye hitilafu hiyo yako nchini Japan na Amerika ya Kaskazini na Toyota inasema kuwa haijapokea taarifa zozote za ajali au majeraha kutokana na hitilafu hiyo

Tuesday, February 11, 2014

RAY, CHUCHU HANS PENZI LAO HALINA KIFICHO TENA



Ray na Chuchu wakijiachia. 

MAMBO hadharani! Penzi ‘hoti’ la mastaa mahiri wa filamu za Kibongo, Chuchu Hans na Vincent Kigosi ‘Ray’ kwa sasa limekuwa kama la njiwa kwani mara nyingi kila sehemu wapo pamoja na hakuna kificho tena.

Chanzo chetu makini kilieleza kuwa mastaa hao wamekuwa wakionekana pamoja mara nyingi na hivi sasa inadaiwa kuwa wanaishi pamoja huku wakiwa na mtoto wa Chuchu aitwaye Danzel.
Mpashaji wetu huyo alizidi kudai kuwa kutokana na mapenzi hayo kukolea siku hadi siku, juzikati baadhi ya ndugu wa mastaa hao walianza vikao vya chini kwa chini ili kuhakikisha mwaka huu wasanii hao wanafunga ndoa lakini haijajulikana kama watafungia kanisani au msikitini kwa kuwa wana dini tofauti.
“Yaani sasa hivi hakuna siri hata chembe, ni fulu kujiachia. Mara nyingi wapo pamoja kila sehemu yaani kama njiwa,” kilisema chanzo chetu.


Chanzo hicho kilizidi kudai kwamba mara nyingi Ray na Chuchu wanapenda kwenda kuogelea na kujiachia kama mke na mume kwenye hoteli moja maarufu (jina linahifadhiwa) iliyoko maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar huku wakijifotoa picha za kumbukumbu.

Baada ya kujazwa ‘info’ hizo na kumwagiwa picha za mastaa hao, gazeti hili lilimtafuta Chuchu kisha kumuuliza kuhusiana na penzi lake na Ray kuwa ‘shatashata’ ambapo alifunguka kuwa kama kuna mtu anawaona wakiwa pamoja ni kwa sababu hivi sasa eti wanaandaa ‘sinema’ yao wawili.
Alipotafutwa Ray ili kuulizwa kuhusiana na ishu hiyo, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa muda wa nusu saa.

WAIRAN WAKAMATWA WAKIINGIZA MADAWA YA KULEVYA TANZANIA



WIKI iliyopita Jeshi la Polisi Kikosi Kazi cha Wanamaji Tanzania, walikamata shehena ya madawa ya kulevya ‘unga’ wenye thamani ya mabilioni ya shilingi zikiwa ndani ya meli. 

Wairan wakipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.
Taarifa za uhakika zinadai kuwa meli hiyo ambayo ni mali ya Kampuni ya Almansoor SA ya Iran ilikamatwa Jumanne iliyopita katikati ya bandari za Zanzibar na Dar es Salaam.
Meli hiyo ilikamatwa baada ya askari waliokuwa doria kuilitilia shaka na kufuatilia kwa karibu ili kujua ilikuwa imebeba nini.
Vyanzo vilivyokuwa katika eneo la tukio vinasema kuwa meli hiyo ilikuwa na watu 12 na baada ya kupekuliwa ndipo walikuta kilo 201 za madawa ya kulevya aina ya heroine.


Wairan wakiwa kizimbani.
Watu waliokamatwa katika meli hiyo ni Mohamed Hassan (30), Abdul Nabii (30), Fahiz Muhamad (34) na Rahi Baksh (30), wote raia wa Pakistani.
Wengine ni Abdulsamad Badreuse (47), Hazra Azat (60),
Nahimu Musa (25), Khalid Ally (35), Kher Murad (38), Said Mohamed (34), Murad Gwaharam (38) na Ayub Hot (50) ambaye ni nahodha wa meli, wote raia wa Iran.
Meli hiyo ilikuwa na mtazamo wa kivuvi na lengo la wahusika ilikuwa wasishtukiwe kirahisi.
“Ilikuwa si rahisi kuigundua kama uwezo wako wa kufikiri ni mdogo lakini askari wetu wana akili sana na ndiyo maana meli ile ilihisiwa mara moja,” alisema mtoa habari mmoja kutoka jeshi la polisi.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Tanzania, ACP Mboje Kanga alisema ilikuwa ni kazi kubwa kuibaini meli hiyo ilikuwa imebeba nini lakini kwa kutumia mbinu za kiintelijensia waliweza kuitilia shaka na kuipeleka bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Uwazi, unga huo ulikuwa utue katika maeneo ya Ilala jijini Dar ambapo baadaye ungesambazwa kila kona ya nchi ya Tanzania.
“Ndugu waandishi, Ilala kuna maeneo ambayo ni maarufu sana kwa biashara kama hiyo, ule unga ulikuwa upelekwe Ilala halafu upelekwe nchi nzima,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kudibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa akizungumza na gazeti hili kuhusu madawa hayo, alisema kama yangefanikiwa kutua Dar na kusambazwa nchini watu milioni 3 mpaka 4 wangetumia, hasa vijana.
Kamanda Nzowa alisema meli hiyo ilitiliwa shaka kutokana na kutokuwa na utambulisho wa nchi husika, yaani bendera kama meli zingine.
Akasema baada ya upekuzi waligundua zaidi ya kilo 201 za heroin zenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 9.
“Mpaka sasa upelelezi unaendelea ili kubaini mwenyeji wao ambaye angewapokea Dar es Salaam ni nani maana kwa vyovyote yupo, tukimbaini amekwisha,” alisema Nzo