Friday, April 18, 2014

MASOGANGE, NIKISEMA UNAJIUZA UTAKATAA?



AGNES Jerald, binti anayetumika sana kunengua na pozi katika video za nyimbo za wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya, amejipatia umaarufu mkubwa sana baada ya kufanya kazi na mkali wa Morogoro, Belle 9 katika kibao chake cha Masogange.

Limegeuka kuwa jina lake na mwenyewe analitumia kikamilifu katika harakati za kimjini. Lakini aligeuka kuwa kipusa zaidi baada ya kukamatwa katika Uwanja waNdege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg mwaka jana, akiwa na shehena kubwa ambayo Tanzania ilijulikana kama madawa ya kulevya, lakini Afrika Kusini wakasema ni malighafi inayoweza kutumika kutengeneza mihadarati.


Masogange ni msichana ambaye Mwenyezi Mungu amemjaalia uzuri wa asili wa Kiafrika. Ana sura nzuri ambayo bado hajaanza kuikoboa kwa mikorogo na mwili unaoendana na umbo lake maridhawa.

Sifa moja kubwa ya uzuri wa msichana huyu, ni maumbile yake ya nyuma, amejazia kiasi ambacho ni wanaume wachache, tena walio waadilifu kwelikweli, wanaoweza kupishana naye na wasigeuke nyuma kuhakikisha walichokiona!

Baada ya kuachiwa kutoka mahabusu nchini Afrika Kusini ambako alishindwa kesi ya kukutwa na shehena ile ya madawa ya kulevya, Masogange alijikuta akiwa gumzo kubwa jijini Dar es Salaam, kiasi kwamba pamoja na kuachiliwa, bado ilimchukua muda mrefu kurudi nyumbani.

Akiwa huko kwa Madiba, binti huyu alikuwa akiweka picha zake kila mara katika mitandao ya kijamii inayopatikana katika Internet, hasa Instagram. Ni utamaduni mpya kwa wasichana wa Kibongo siku hizi, wengi wanapenda kutupia picha zao humo na watu ambao huwaona, huwasifia kama wamependeza au huwaponda kama wamechukiza.

Lakini katika hali isiyotarajiwa kabisa, wiki kadhaa zilizopita, Masogange aliweka picha yake huko, ikionyesha sehemu kubwa ya mwili wake, ikiwa imepakwa hina.

Aliipaka kwa staili ambayo mtu akiitazama haraka haraka anaweza kudhani ni Tattoo, ile michoro inayochorwa kwa sindano mwilini ambayo hapo awali tulianza kuiona kwa wasanii wa Kimarekani.

Lakini kitu kibaya katika picha hiyo ni kwamba Masogange amepiga picha mguu wake akiwa amepaka hina hiyo hadi juu kabisa pajani.

Baadaye akapiga picha nyingine akiwa amevaa kimini, lakini kikionyesha sehemu ya paja hilo lililopakwa urembo huo ambao pia hutumiwa na wanawake wa Kiislamu wakati wa ndoa!

Ni picha ambayo mwanaume yeyote mkware akiiona, anavuta hisia za mahitaji ya kimapenzi. Na nieleweke, siyo Masogange tu anayetupia picha za aina hii, wasichana wengi hufanya hivi na baadhi yao, baada ya kuziweka, huweka pia na namba zao za simu, ukiwa na shida nao uwatafute!

Sitaki kuamini moja kwa moja kwamba msichana huyu ambaye amepata umaarufu bila ya kutarajiwa anajiuza, lakini ni vigumu sana kwa picha zile kuacha kusadiki jambo hili kama mtu mmoja atajitokeza na kutoa madai kama hayo.

Inakuaje mtoto wa kike, mwenye jina, tena na uzuri wako bomba kabisa wa asili, unapiga picha za namna ile na kuziweka hadharani? Nafikiri siyo sawa, zipo picha zinazopaswa kuendelea kubakia chumbani.

Kwa jinsi mambo yanavyotokea, unapata kabisa hisia kwamba kumbe dada zetu wanatafuta umaarufu kwa nguvu kwa malengo binafsi, yasiyo ya kimaadili na yenye kuchefua.

Wakishapata majina na bahati nzuri kuanza kufuatiliwa na vyombo vya habari, vikitanguliwa na magazeti, wanaanza makeke!

Kwa kutambua kwamba sura zao zinafahamika, badala ya kujistahi, ndiyo kwanza utashangaa kuona wanavaa mavazi yenye utata, kumbe tunaanza kuelewa kuwa wanafanya hivi ili kujitangaza, kama wanavyosema mabingwa wa uchumi, biashara matangazo.

No comments:

Post a Comment