Kamanda wa Polisi mkoani Tabora,
Suzan Kaganda
MATUKIO ya kukata viungo vya walemavu wa ngozi (albino), yameendelea mkoani hapa, ambapo juzi mlemavu wa pili katika muda usiozidi wiki mbili, amekatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho kusikojulikana.
Suzana Mungi (35) ambaye ni mlemavu wa ngozi na mkazi wa Kijiji cha Buhelele kata ya Nsimbo wilayani Igunga, amekatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho kusikojulikana.
Katika tukio hilo lililofanyika juzi, mume wa Suzana, Mapambo Mashili ameuawa kikatili kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.
Hivi karibuni mtoto Upendo Sengerema (15), mkazi wa Kijiji cha Usinge, Kata ya Uganza Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, alikatwa mkono na wahalifu ambao walikimbia nao. Mpaka sasa Upendo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani hapa.
Akizungumzia tukio hilo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, alisema kitendo hicho ni cha kinyama, ambacho hakiwezi kuvumiliwa na mtu yeyote.
Alisema watu wote watakaobainika kufanya unyama huo, watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo visivyokuwa vya kistaarabu.
Aidha, aliwataka wakuu wa wilaya zote mkoani hapa, kutambua maeneo yote ambayo wanaishi walemavu wa ngozi na kuwa karibu nao kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wao kila siku katika maeneo wanayoishi.
Dau la RC Mkuu wa huyo wa Mkoa, ametangaza dau la Sh 500,000 kwa mwananchi yeyote atakayetoa taarifa za kupatikana kwa wahalifu wanaojihusisha na matukio hayo.
Pia, Mwassa aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Tabora, kuhakikisha waliofanya matukio hayo, wanakamatwa na kutiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Tabora, kuachana na imani za kishirikina na kueleza kuwa atahakikisha wahusika wanakamatwa.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY
No comments:
Post a Comment