Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia kuhudhuria vikao.
Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai kuwa Bunge lilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba, hasa katika suala la muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama tawala, CCM kiliingiza suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye rasimu hiyo badala ya serikali tatu.
Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na wajumbe kutoka CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201 kutoka taasisi mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo huenda usifanikiwe kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka uamuzi upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.
Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa Lipumba alisema wana uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao wajumbe 14 kutoka kundi la 201 ambao ndiyo tegemeo lao.
"Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha, tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21," alisema.
"Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini tunajua misimamo yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini tunawafuatilia kwa karibu."
Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa mkono na wabunge na wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea mamlaka ya Zanzibar.
"Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la Wawakilishi, katika malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF na CCM yalikuwa yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka CCM Zanzibar ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake nini? Mamlaka ni Serikali," alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
"Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano."
Aitetea Tume ya Jaji Warioba
Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na rasimu iheshimiwe kwa kuwa imefanya kazi kubwa.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY
No comments:
Post a Comment