Monday, August 18, 2014

KWA MUONEKANO TU NCHI YA DUBAI IMEKATAA MTU HUYU KUINGIA NCHINI HUMO

Uso wake Rolf Bushholz ulivyo na maumbile kama pembe
Mwanaume mmoja kutoka Ujerumani anayeshikilia rekodi ya dunia ya kuwa mtu aliyetoboa zaidi mwili wake, Rolf Buchholz amekatazwa kuingia Dubai.
Rolf Buchholz, ametoboa mwili wake mara 453 ikiwemo usoni mwake na ana pembe mbili juu ya paja la uso wake.
Rolf Bushholz aliyenyimwa ruhusa ya kuingia Dubai.
Mjerumani huyo mwenye umri wa miaka 53 alikuwa ameratibiwa kuandaa onyesho katika klabu moja mjini humo.
Bwana Buchholz alieleza BBC kuwa maafisa wakuu katika uwanja wa ndege walihofia huenda alikuwa ni '' mchawi'' .
Mtaalamu huyu wa tarakilishi alitambulika na kitabu cha rekodi za dunia cha Guiness, kama mwanaume aliyetoboa mwili wake zaidi duniani mwaka wa 2012.
Rolf Bushholz katika moja ya maonyesho yake
Alieleza wanahabari wa Press News Agency kuwa hapo awali alikuwa amekubalika lakini baadaye akarejeshwa kabla ya kufika eneo la maafisa wa usafiri ndipo akarejeshwa katika ndege iliyokuwa ikielekea mjini Instabul Uturuki.
Onyesho lake katika mgahawa maarufu wa Irque le Soir ulioko katika hoteli ya Fairmont Hotel Dubai lilifutiliwa mbali.
Mdomo wake uso wake Rolf Bushholz ulivyotogwa
Maafisa wa mgahawa huo wa Fairmont Dubai wamesema kuwa walifanya chochote kadri ya uwezo wao kumuingiza Buchholz nchini Dubai lakini hawakufua dafu.
Bwana Rolf amesema kuwa mizigo yake bado iko Dubai na aliapa kwenye mtandao wa kijamii kuwa hatarudi tena katika milki za Kiarabu.
Polisi na Maafisa wa usafiri wa ndege nchini Dubai hawajazungumzia swala hilo.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY

KITUO CHA WAGONJWA WA EBOLA CHAVAMIWA NA MALI KUPORWA

Wafanyakazi wa afya wabeba maiti ya mgonjwa wa Ebola, Monrovia, Liberia Agosti 12, 2014
Waandamanaji nchini Liberia walishambulia na kupora mali kwenye kituo kimoja kilichowekewa karantini kwa wagonjwa wa Ebola katika mji mkuu wa Monrovia.
Maafisa wanasema shambulizi lilitokea Jumamosi jioni kwenye kituo kilichopo katika mji jirani wa West Point. Wanasema kundi moja la wakazi wenye silaha, wengi wao wanaume waliokuwa na virungu, walivunja jengo na kuiba vifaa kutoka kituo cha afya ambavyo huenda vimeathiriwa na virusi vya Ebola.
Shirika la habari la Ufaransa-AFP, linawakariri wafanyakazi wa afya wa Liberia wakisema kwamba wagonjwa 20 ambao wote walifanyiwa uchunguzi na kugunduliwa wana virusi vya Ebola, pengine walikimbia baada ya shambulizi au walilazimishwa kuondoka na jamaa zao.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY

LIPUMBA AELEZA WANACHOKITAKA UKAWA

Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia kuhudhuria vikao.
Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai kuwa Bunge lilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba, hasa katika suala la muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama tawala, CCM kiliingiza suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye rasimu hiyo badala ya serikali tatu.
Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na wajumbe kutoka CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201 kutoka taasisi mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo huenda usifanikiwe kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka uamuzi upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.
Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa Lipumba alisema wana uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao wajumbe 14 kutoka kundi la 201 ambao ndiyo tegemeo lao.
"Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha, tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21," alisema.
"Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini tunajua misimamo yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini tunawafuatilia kwa karibu."
Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa mkono na wabunge na wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea mamlaka ya Zanzibar.
"Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la Wawakilishi, katika malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF na CCM yalikuwa yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka CCM Zanzibar ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake nini? Mamlaka ni Serikali," alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
"Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano."
Aitetea Tume ya Jaji Warioba
Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na rasimu iheshimiwe kwa kuwa imefanya kazi kubwa.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY

MAUWAJI YA ALBINO YAENDELEA HUKO TABORA

kamanda-suzan-kaganda_300_179_cad4c.jpg
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, 
Suzan Kaganda
MATUKIO ya kukata viungo vya walemavu wa ngozi (albino), yameendelea mkoani hapa, ambapo juzi mlemavu wa pili katika muda usiozidi wiki mbili, amekatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho kusikojulikana.
Suzana Mungi (35) ambaye ni mlemavu wa ngozi na mkazi wa Kijiji cha Buhelele kata ya Nsimbo wilayani Igunga, amekatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho kusikojulikana.
Katika tukio hilo lililofanyika juzi, mume wa Suzana, Mapambo Mashili ameuawa kikatili kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.
Hivi karibuni mtoto Upendo Sengerema (15), mkazi wa Kijiji cha Usinge, Kata ya Uganza Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, alikatwa mkono na wahalifu ambao walikimbia nao. Mpaka sasa Upendo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani hapa.
Akizungumzia tukio hilo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, alisema kitendo hicho ni cha kinyama, ambacho hakiwezi kuvumiliwa na mtu yeyote.
Alisema watu wote watakaobainika kufanya unyama huo, watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo visivyokuwa vya kistaarabu.
Aidha, aliwataka wakuu wa wilaya zote mkoani hapa, kutambua maeneo yote ambayo wanaishi walemavu wa ngozi na kuwa karibu nao kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wao kila siku katika maeneo wanayoishi.
Dau la RC Mkuu wa huyo wa Mkoa, ametangaza dau la Sh 500,000 kwa mwananchi yeyote atakayetoa taarifa za kupatikana kwa wahalifu wanaojihusisha na matukio hayo.
Pia, Mwassa aliliagiza Jeshi la Polisi mkoani Tabora, kuhakikisha waliofanya matukio hayo, wanakamatwa na kutiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzana Kaganda, aliwataka wakazi wa Mkoa wa Tabora, kuachana na imani za kishirikina na kueleza kuwa atahakikisha wahusika wanakamatwa.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY

JK AITISHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA CCM

Rais Jakaya Kikwete
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kitakachofanyika Dodoma kesho.
Habari za uhakika zilizopatikana Dar es Salaam jana, zinasema moja ya ajenda kubwa inayoweza kutawala kikao hicho ni mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba ambalo limesusiwa na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kwa muda sasa Ukawa wamekuwa wakimtaka Rais Kikwete aliahirishe Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma, kwa kile wanachodai kutotendewa haki.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM kililiambia MTANZANIA kuwa kikao hicho cha siku moja kitajadili masuala mbalimbali likiwamo kufuatilia mwenendo wa makada wa chama hicho ambao katika siku za hivi karibuni kwa namna moja au nyingine wanadaiwa kutangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
"Nakwambia hakuna mjumbe hata mmoja anayejua nini kinakwenda kujadiliwa, Rais Kikwete amekwenda na siri nzito moyoni...tusubiri tuone nini kitatokea Dodoma.
"Hata hivyo, ajenda kubwa itakuwa uamuzi mpya juu ya hatima ya sasa ya Bunge Maalumu la Katiba ambalo mwenendo wake umekuwa ukilalamikiwa na wengi," kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya CCM Makao Makuu.
Chanzo hicho kilisema kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM kilichoanza juzi mjini Dodoma kufuatilia mwenendo wa makada sita waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa kuanza kampeni za kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati. Kikao hicho kitatoa taswira na mwelekeo mpya ndani ya CCM.
Uamuzi wa Rais Kikwete kuitisha CC unatokana na uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi Julai 16 mwaka huu ambayo ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais.
Kutokana na hali hiyo, CC iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada hao.
Julai 17 mwaka huu, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema endapo Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho inayotarajiwa kukutana Agosti mwaka huu ikibaini kama makada hao walikiuka mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa watapoteza sifa ya kugombea.
Pamoja na adhabu nyingine, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya siasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mienendo yao ya siasa ikifuatiliwa.
Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
Nape alisema CC ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonyesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais.
"Baada ya kutafakari kwa kina, kamati kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili wasipoteze nia ya kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo," alisema Nape.
Alisema kama itabainika makada hao hawakutekeleza masharti ya adhabu zao kama zilivyotolewa na CC, kuna hatari ya kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
"Kila mmoja anafuatiliwa mwenendo wake; kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo.
Kama watakuwa hawajatekeleza adhabu zao kamati itapeleka mapendekezo CC waweze kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa makosa yao na taratibu za chama," alisema Nape.
Alisema ni muhimu kwa wanachama wote kukumbuka chama ni pamoja na katiba, kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga jambo ambalo halivumiliki.
Alisema nia ya CCM ni kusimamia na kuhakikisha chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu hasa katika kuelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Hoja ya kuendelea kufuatiliwa kwa makada hao ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, PhilipMangula, aliyesema amefungua jalada kwa ajili ya makada hao.
Suala jingine alilowasilisha Mangula ni ripoti ya ziara yake aliyoifanya katika mikoa ya Tabora na Kigoma na Tanga.
Februari 18 mwaka huu, CCM kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za nidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
Uamuzi huo ulibarikiwa na Kamati Kuu iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
MTANZANIA lilimtafuta Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye hakupatikana kwenye simu yake ya kiganjani na muda wote ilikuwa imezimwa.
Hata hivyo, ofisa wa CCM Idara ya Uenezi alipoulizwa kuhusu kikao hicho cha CC alisema hana taarifa zozote kuhusiana na kikao hicho.
"Mimi sina lolote ninalolijua kwa sasa labla kwa kuwa nipo kwenye mapumziko acha nifuatilie taarifa zaidi. Lakini ninachojua hakuna kikao chochote kwa sasa," alisema ofisa huyo.
CHANZO:MABANTANYAU FAMILY