Sao Paulo, Brazil. Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Sepp Blatter amesema madai ya rushwa katika kuipa Qatar uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za 2022 yamechochewa na hisia za ubaguzi wa rangi.
Blatter alisema haya alipokuwa akijibu madai wanayorushiwa baadhi ya wanakamati wa Fifa waliohusika na uamuzi huo, wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa.
"Kuna kimbunga kimeelekezewa Fifa tangu iichague Qatar. Inasikitisha sana kwamba yote yamechochewa na hisia za ubaguzi hasa wa rangi," Blatter.
Blatter alisema hayo mjini Sao Paulo, Brazil alipokuwa akizungumza na maofisa kutoka Afrika.
Aliahidi kuwa Fifa itakabiliana na chochote kinachobeba hata chembe ya kibaguzi.
Hata hivyo, Fifa imeamua kufanya uchunguzi wake na imesema taarifa ya uchunguzi itatolewa kati ya Septemba na Oktoba.
Katika kikao chao cha Sao Paulo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) nalo lilitoa cheche zake kwa vyombo vya habari vya kimataifa hasa magazeti ya Uingereza likisema ndiyo yaliyoanza kampeni hiyo dhidi ya Qatar na ya kuchafua jina la shirikisho hilo.
Wametaja suala hilo kuwa ni kampeni iliyojaa chuki na udhalilishaji. Wametishia kuyafungulia kesi magazeti husika.
Mwendesha mashtaka wa zamani wa Marekani, Michael Garcia anayeongoza kitengo cha uchunguzi cha Kamati ya Maadili, ndiye anayechunguza kashfa hiyo.
amekuwa akichunguza utaratibu na vipi nchi zinavyochaguliwa kuandaa kombe hilo na atatoa ripoti yake hapo Julai.
Qatar ilishinda Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani hapo Desemba 2010 ilipochaguliwa na Fifa kama mwenyeji wa Kombe la Dunia 2022.
Qatar imekana vikali kuhusika na vitendo vyo vyote vya rushwa na kusema kuwa ilishinda kihalali
No comments:
Post a Comment