Thursday, June 26, 2014

Sista aliyeuawa na majambazi kuagwa leo Dar es salaam


Dar es Salaam.
 Sista wa Kanisa Katoliki, Clencensia Kapuli aliyeuawa na majambazi na kuporwa kiasi kikubwa cha fedha ambacho bado hakijafahamika, anatarajiwa kuagwa leo katika Parokia ya Mtakatifu Gaudence Makoka, Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwenyeheri Anuwarite, Carlos Mgumba alisema ibada ya kuaga mwili wa marehemu itaanza saa sita mchana shuleni hapo, kabla ya mwili kusafirishwa kwenda Mbeya kwa maziko.
“Nashindwa kujizuia kila nikifikiria jinsi walivyomuua kikatili, sista, alikuwa mpole na mnyenyekevu…Wametumia nguvu kubwa kama shida yao ilikuwa ni fedha wangeweza hata kuchukua bila kutumia silaha, wametuachia pigo kubwa kwa shule yetu, wamemwonea tu,” alisema huku akitokwa na machozi. Mgumba alisema katika miaka miwili na nusu aliyofanya naye kazi, Sista Kapuli alisaidia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya shule kutokana na utendaji kazi wake uliotawaliwa na uaminifu.
“Nakumbuka siku hiyo tulikuwa pamoja asubuhi kwa mipango ya malipo ya mishahara ambayo kwa kawaida tunalipa moja kwa moja kwenye akaunti za walimu, saa sita hivi mchana aliniaga anakwenda benki kuchukua fedha za (petty cash) matumizi madogo ya shule,” alisema.
Alisema akiwa anaendelea na kazi zake, ndipo alipopigiwa simu na kujulishwa kuhusu tukio hilo la mauaji lililotokea eneo la Riverside, Ubungo, Dar es Salaam hukuna dereva Mark Mwarabu kukatwa kidole gumba kwa risasi.
Rais wa serikali ya wanafunzi wa sekondari hiyo, James Sweya alisema marehemu alikuwa karibu naye kwa sababu, yeye anasomea mchepuo wa biashara hivyo alikuwa akimsaidia kumpa mwongozo wa mambo ya uhasibu.
Mwanafunzi mwingine, Evelyn Kiwenge alisema Sista Kapuli alikuwa mwenye upendo wa aina yake msaada kwa maisha ya wanafunzi wengi katika sekondari hiyo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema juzi kuwa tayari kimeundwa kikosi kazi ili kufuatilia tukio hilo na akiahidi kwamba atahakikisha wote waliohusika wanasakwa na kutiwa mbaroni.
Alisema majambazi hayo yaliua na kupora Sh20 milioni lakini hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa majambazi hayo yalipora Sh10 milioni.
Sista Kapuli aliuawa akiwa ameongozana na wenzake, Sista Brigita Mbaga na dereva Mwarabu aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux walikuwa wakitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City kuchukua fedha.
Baada ya kufika Ubungo kwa lengo la kulipa deni la chakula katika duka la Thomas Francis, ndipo walitokea majambazi wawili wakiwa na pikipiki ambayo haikusomeka namba mmoja wao akiwa na bunduki aina ya SMG na kumpiga risasi ya kidole gumba cha mkono wa kulia Mwarabu kisha kumgeukia Sista Kapuli na kumuua kisha kuondoka na fedha zilizokuwa kwenye pochi.

Mkutano mkuu CUF, Lipumba Seif Kidedea wengine wapigwa chini

Mkutano mkuu CUF, Vijimambo, Siasa, Upinzani Tanzania
Viongozi wakuu wa CUF wakionyesha mshikamano baada ya kuchaguliwa kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Wa pili kulia ni msimamizi wa uchaguzi huo Awadh Ali Said
 Mkutano Mkuu wa CUF Taifa umemchagua tena Katibu Mkuu wa Chama hicho kuendelea na wadhifa huo kwa kupata kura 675, sawa na asilimia 99.5 ya kura zilizopigwa.
Mkutano huo pia umemchagua Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa kwa kupata kura 659 sawa na asilimia 95.5 na kumshinda mpinzani wake Chifu Lutalosa Yemba aliyepata kura 30 sawa na asilimia 4 nukta 3.

Aidha mkutano huo umemchagua Mhe. Juma Duni Haji kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho kwa kupata kura 662 sawa na asilimia 99.25.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumpa tena ridhaa ya kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wakati wa Kampeni. Mapema akizungumza katika kampeni za kuomba kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif amesema siri ya mafanikio yake kisiasa ni kutokana na kujiamini kwake kuwa kiongozi, kuwa mkweli na kuwa na dhamira njema kwa wananchi.
Akijibu hoja za wajumbe wa mkutano huo Maalim Seif amewataka viongozi wa chama hicho kutotangaza kuhudhuria kwa viongozi wa kitaifa kwenye mikutano ya hadhara hadi pale wenyewe watakapothibitisha kuhudhuria, ili kuepusha wananchi kutoamini utendaji wa viongozi hao.

Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Juma Duni Haji amesema iwapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo atashirikiana na viongozi wengine wa kitaifa pamoja na wananchi kuhakikisha kuwa chama kinapata maendeleo zaidi.
Chifu Yemba amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kutetea demokrasia ya kweli ndani ya chama na taifa kwa ujumla. Chifu Yemba ambaye ni mwanasayansi kitaaluma, pia ni Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Prof. Lipumba amesema akichaguliwa atahakikisha anatembelea nchi nzima kuimarisha chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Aidha amesema atafanya juhudi za ziada kuona kuwa Tanzania inakuwa na Muungano wa kuheshimiana baina ya pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).

Amesema wanawake watapewa nafasi ndani ya kamati tendaji ya chama kuondosha dhana ya mfumo dume unaodaiwa kuwepo katika ngazi za juu za uongozi.
Mgombea mwengine wa nasafi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa M’bezi Adam Bakar, amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kubakia wagombea wawili wa nafasi ya Mwenyekiti. Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa muda wa kuongoza uchaguzi huo uliosimamiwa na mwanasheria Awadh Ali Said.

WEREMA NUSURA AMPIGE KAFULILA JUZI BUNGENI

mawaziri 8e512
Na MABANTANYAU FAMILY
Kama siyo kuzuiwa na mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana angezua tafrani bungeni kutokana na kitendo chake cha kutaka kumpiga Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila.
Sakata hilo lilitokea jana asubuhi baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kuahirisha kikao cha Bunge hadi jioni, ikiwa ni muda mfupi baada ya Werema na Kafulila kurushiana maneno bungeni. Jaji Werema alichukia baada ya Kafulila kumwita mwizi, akijibu mapigo baada ya mbunge huyo kuitwa tumbili na mwanasheria huyo.
Waliomzuia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Abdulla Juma Saadallah.
Mawaziri hao walimsindikiza Werema hadi nje ya Ukumbi wa Bunge na kutoweka.
Ilivyokuwa
Hali ilianza kuchafuka wakati Jaji Werema alipokuwa akijibu mwongozo uliombwa na Kafulila kuhusu fedha za akaunti ya Escrow.
Katika mwongozo huo, Kafulila alisema Wizara ya Nishati na Madini kupitia Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo alizungumza uongo mara mbili bungeni kuhusiana na fedha za akaunti ya Escrow.
"Alisema uongo mbele ya Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maeneo mawili, kwamba uamuzi wa kutoa fedha za Escrow kwa IPTL ulikuwa wa Mahakama na Serikali isingeweza kwenda kinyume..." alisema.
Alisema katika hukumu hiyo ya Septemba mwaka jana, hakuna mstari hata mmoja unaosema kuwa fedha za Escrow wapewe Kampuni ya IPTL.
"Profesa Muhongo aliliambia Bunge kuwa Serikali ililipa fedha hizo ili kuondokana na kesi hiyo lakini ninazo nyaraka za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuteua kampuni mbili za uwakili kwenda kuiwakilisha katika kesi nchini Uingereza," alisema Kafulila.
Alisema kwamba aliomba mwongozo sababu huo umekuwa mwendelezo wa kuzungumza uongo bungeni... "Naibu Waziri (Nishati na Madini - Stephen Masele), alizungumza uongo bungeni tukaambiwa kuwa wamekutana katika sherehe za kuzaliwa yakaisha, haiwezekani, Bunge ni sehemu ya kuisimamia Serikali.

Tuesday, June 24, 2014

Kuhusu Umeme Kukatika Nchi Nzima hii ndio Taarifa Kamili.



TBS YAKAMATA SHEHENA YA NGUO ZA NDANI

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekamata shehena ya marobota ya nguo za ndani za mitumba ambazo thamani yake haijajulikana kwa kuwa zimechangaywa na nguo za watoto.
Mkaguzi wa TBS, Donald Manyama alisema wamefanikiwa kukamata nguo hizo juzi bandarini zikiwa kwenye kontena mbili ambapo walilazimika kuongozana na wahusika ambao ni Kampuni ya Dema ili kuufanyia ukaguzi zaidi mzigo huo. (J M)
“Katika ukaguzi wetu , tumebaini kwamba marobota haya yanaonekana kama ni nguo za watoto lakini ndani kuna nguo nyingi za ndani za kike na za kiume za wakubwa na watoto za mitumba ambazo zimepigwa marufuku kuingizwa au kuuzwa nchini,” alisema.
Akiwa katika ghala za kampuni hiyo eneo la Mwenge, Dar es Salaam, Manyama alisema kazi ya kuzichambua na kuzitenganisha inaendelea ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Mfanyabiashara Mussa Kassim wa Kampuni ya Dema katika utetezi wake amedai  kusikitishwa kwake na hali hiyo hasa kwa kuwa wao waliagiza nguo za watoto na siyo za ndani kama ilivyotokea.
“Mitumba hii sisi tunaiagiza kutoka Ujerumani. Hatukuagiza nguo za ndani kwa kuwa siyo kusudio letu wakati Serikali imepiga marufuku. Nafikiri zimechangaywa kwa bahati mbaya,” alisema Kassim.

SUAREZ ADAIWA KUMNG'ATA MCHEZAJI KAMA VAMPIRE

Picha za video zimeonesha mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez akimng'ata beki wa Italy Giorgio Chiellini. Mwamuzi hakuona kitendo hicho lakini huenda hatua zitachukuliwa baadaye

Saturday, June 21, 2014

Uganda yasema haitishwi na vikwazo kutoka Marekani


Gazeti la Red Cross lilichapisha majina ya watu wanaoshukiwa kuwa wapenzi wa jinsia moja baada ya sheria kupitishwa
Katibu mkuu wizara ya mambo ya nje wa Uganda, Balozi James Mugume, amesema kuwa Uganda haitishwi na vikwazo ilivyowekewa na Marekani kama hatua ya kupinga sheria yake kali kuhusu mapenzi ya jinsia moja.
Mwandishi wa BBC mjini Kampala, Isaac Mumena anasema kuwa Balozi Mugume ameelezea kuwa serikali ya Uganda hata hivyo itafanya mazungumzo na Marekani ili kufafanua hatua waliyochukua.
Amesisitiza kuwa
wataieleza Marekani sheria hiyo inapinga tabia ambayo sio ya kiafrika na maadili ambayo hayakubaliki katika jamii nyingi za kiafrika.
Serikali imesisitiza kuwa vikwazo hivyo havitakuwa na athari kubwa kwa nchi hiyo na pia imekanusha madai ya mashirika ya kijamii kuwa tayari sheria hiyo imechochea ongezeko la dhuluma dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Vikwazo vyenyewe ni pamoja na kufutilia mbali msaada wa kijeshi, kuwapiga mrufuu baadhi ya maafisa wa serikali kusafiri nje na kupiga tanji mali zao.
Maandamano kupinga mapenzi ya jinsia mopja na kumpongeza Rais Museveni kuwa kupitisha sheria hiyo
Kadhalika msemaji wa serikali Ofwono Opondo amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa wananchi wa Uganda wanafahamu kuwa hawatategemea tena msaada wa nchi za Magharibi
Sheria hiyo iliyotiwa saini na Rais Yoweri Museveni mwezi Februari inasema kuwa wanaopatikana na hatia mara mbili ya kuhusika na mapenzi ya jinsia moja watafungwa maisha jela.
Sheria hiyo pia inaharamisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja pamoja na kuwataka wananchi kuwashitaki watu wanaohusika na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa maafisa wakuu.
Ikulu ya White house imelaani sheria hiyo ikisema kuwa inakwenda kinyume na uhusiano kati ya nchi hizo ikitoa wito wa sheria hiyo kufutuliwa mbali. 
Waziri wa mambo ya nje John Kerry, amefananisha sheria hiyo na sheria za utawala wa zamani wa kinazzi nchini Ujerumani.

NGUZA VIKING 'BABU SEYA' NA PAPII KOCHA WAPIGA SHOW SIKU YA MAGEREZA

Wanamuziki wa Bendi ya Wafungwa, Nguza Viking ‘‪‎Babu‬ ‪‎Seya‬’ (kulia) na mwanaye Johnson Nguza ‘‪‎Papii‬ Kocha‬’ (wa pili kulia) wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani, wakitumbuiza na wenzao katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika katika Chuo cha Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam jana.

DALADALA ZA GONGANA NA KUUWA WATU 19 NA WENGINE MAJERUHI DAR LEO.

TAHADARI PICHA ZINA TISHA
 Habari zilizo tufikia ni kwamba ajali hii mbaya imetokea eneo la Makongo. Coaster mbili zimegongana watu 20 wamefariki hapo hapo. 
Moja wapo ya Daladala aina ya Coster iliyo husika katika ajali hiyo
 R.I.P

Tunatoa pole kwa familia zote zilizo fikwa na msiba huu. Habari zaidi tutawaletea tutakapo zipata mara moja uysichoke kuwa  nasi.

LOWASSA ATANGAZA ‘UAMUZI MGUMU’ SANA KUWAHI KUUCHUKUA

lowassa 9c884
Na MABANTANYAU FAMILY
Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa ametangaza kuanza kwa hatua za kuyarejesha kwenye Mamlaka za Serikali za Vijiji mashamba 21 ya wawekezaji yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 10,000, ambayo hayajaendelezwa.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lomooti, Kata ya Lolkisale wilayani humo alipokwenda kutembelea boma la kisasa la mfugaji Isaya Lembekure, Lowassa alisema haiwezekani wananchi wa Monduli kukosa ardhi wakati, kuna ardhi yao iliyohodhiwa na wachache bila kuendelezwa.
"Monduli tumechoka na uuzwaji wa ardhi. Kila mahali ni matatizo ya uuzwaji wa ardhi. Sasa tunatangaza kuanza mchakato wa kuyarejesha mashamba yote ya wawekezaji ambayo hayajaendelezwa. Tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuyarejesha," alisema Lowassa.
Tamko hilo la Lowassa, lilipokewa kwa shangwe na wananchi wa Wilaya ya Monduli na limekuja wakati migogoro ya ardhi baina ya wawekezaji na wananchi na wakulima na wafugaji imeshamiri nchini.
Licha ya kutoa agizo hilo, Lowassa ameendelea kukemea uuzajiwa wa ardhi wilayani humo, unaofanywa kinyume cha taratibu na Serikali.
"Kuanzia sasa kiongozi wa kijiji atakayebainika kuhusika kuuza ardhi kinyemela, ang'olewe kupitia mikutano ya vijiji," alisema Lowassa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Twalib Mbasha alisema tayari halmashauri hiyo imeanza maandalizi ya kuyarejesha mashamba hayo kwa kuwataka wahusika wa mashamba hayo kujieleza kwa nini hawajayaendeleza hadi leo.
"Halmashauri inakusudia kuyafuta mashamba yote yasiyoendelezwa na yaliyotelekezwa, hii ni kutokana na kushindwa kufuata masharti ya ardhi kama ilivyoanishwa na sheria ya Ardhi namba 4,999 fungu la 44 na fungu la 48. Nimetoa siku 90 watu hawa wajieleze," alisema Mbasha.
Aliyataja mashamba yanayotarajiwa kurejeshwa kwenye mamlaka za Serikali za Vijiji kuwa ni Meru Enterprises namba 10, ACU LTD namba 2390, TANFORM LTD 47, TANFORM 44 na Melembuki Kitesho Mollel namba 974 katika Kijiji cha Lolkisale.
Mashamba mengine ni The Monduli Parents Sec School, Musa Mamuya namba 2278 lipo Makuyuni, David Pello 2275, Hillary Gadi namba 2474, Khalifan Said Masoud 2276, Masoud Said Masoud 2277 yapo Kijiji cha Mswakini Juu.
Alitaja pia yaliyopo katika kijiji hicho ni ya Lucas Petro Kambei namba 2597 na Rungwa game Safari Ltd namba 2765.
Alisema mashamba mengine ni Omary Daudi Mshana 1571, Saidi Rashid Lena namba 2549 yaliyopo Kijiji cha Naitolia, wakati mashamba mengine ni ya T.R Msuya namba 3, Esimingori Estate Ranch namba 7/2, Saburi Estate Ltd namba 7, Musa Y. Mamuya yaliyopo Makuyuni.

WANAMGAMBO WAHIMIZWA KUJITOLEA KATIKA MAPIGANO MAKALI HUKO IRAQ

Jeshi la Mehdi mjini Najaf
Maelfu ya wanamgambo wa Kishia waliobeba silaha, wamefanya mhadhara mjini Baghdad na miji mengine ya Iraq ili kuonesha nguvu zao dhidi ya wapiganaji wa Kisunni ambao wameteka maeneo makubwa kaskazini mwa Iraq.
Wafuasi hao wa kiongozi wa Kishia mwenye msimamo mkali, Moqtada al-Sadr, piya walipinga wanajeshi wa Marekani kurudi Iraq kupambana na wapiganaji.
Kikosi cha Moqtada al-Sad kiliwahi kupigana na Marekani nchini Iraq kwa miaka kadha. Katika mhadhara uliofanywa Kirkuk, mwakilishi wa Moqtada al-Sad, Raad al Sakhri, alihutubia wafuasi wa jeshi lao liitwalo Mehdi:
"Tunawahimiza muwe tayari kujitolea mhanga kuilinda nchi yetu tunayoipenda!" Wapiganaji wa Kisunni wanaopambana na jeshi la serikali kaskazini mwa Iraq wanasema wameuteka mji wa Al-Qaim, karibu na mpaka wa Syria, kutoka mikono ya serikali.
Al-Qaim ni mji muhimu katika kuvuka mpaka ambao unaweza kuwaruhusu wapiganaji wa kundi la ISIS kupitisha silaha nzito, kutoka maeneo ya Syria wanayodhibiti, hadi Iraq.
Kundi hilo piya limesema kuwa limeuteka mji wa Rawa.
Na limeeleza kuwa mapambano makali yanaendelea kwenye kinu kikubwa kabisa cha kusafisha mafuta nchini Iraq, Baiji, na wamedungua helikopta mbili za serikal

UINGEREZA YAONDOLEWA BRAZIL HAPO JANA.

140619212028 uruguay england 512x288 bbc nocredit b52d9
Na MABANTANYAU FAMILY
Uingereza wameondolewa kutoka kombe la dunia la mwaka huu huko Brazil baada ya raundi ya kwanza, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1958.
Uingereza ilibanduliwa baada ya Italia kupoteza mechi yao dhidi ya Costa Rica 1-0 huko Recife katika kundi D.

Uingereza ilikuwa imeshindwa na Uruguay na Italia katika mechi zilizotangulia.
Uingereza ilihitaji Italia kushinda mechi yao ili wapate matumaini ya kuendelea lakini Costa Rica walipoishinda Italia, matumaini yao yakapotea pia.
Kikosi cha Uingereza kiliitazama mechi hiyo kutoka katika makazi yao, hotelini huko Rio.
Aliyekuwa mlinzi katika kikosi hicho, Rio Ferdinand anaamini kuwa kukosa uzoefu kulichangia pakubwa katika kuondolewa kwa timu hiyo mapema hivyo.
Ushindi wa Costa Rica umeiondoa Uingereza
Hata hivyo anadhani kuwa mchuano huo ni muhimu kwani utasaidia kukuza wachezaji wao wachanga.
"labda Uingereza ilikua bado changa katika hali tofauti .
Mfano, katika mchuano dhidi ya Uruguay, waliposawazisha 1-1, walikua na nafasi ya kupata angaa alama moja na hilo lingekua bora" alisema Ferdinand.
Mkufunzi Roy Hodgson, alichagua kikosi kilichokua na wachezaji wachanga na alitumai watanawiri kutoka kwa kundi lao gumu.
Kwa natharia, Costa Rica ndio iliyotarajiwa kulazwa mabao mengi ikilinganishwa na majina makubwa katika kandanda Hata hivyo, Costa Rica ndio wamekuwa wa kwanza kuingia katika raundi ya pili.
Uingereza imebanduliwa nje ya kombe la dunia Brazil.
Hata ingawa walishindwa katika mechi yao ya kwanza na timu ya Italy 2-1, mechi yao ya Alhamisi dhidi ya Uruguay ilionekana kuwapa matumaini.
Uruguay walikuwa wamepoteza mechi yao ya kwanza dhidi ya Costa Rica.
Hata hivyo, mabao mawili ya Luis Suarez yaliipatia Uruguay ushindi wa 2-1, tukio lililowaacha wachezaji wa Uingereza kutegemea matokeo ya michuano mingine,
Baada ya kushindwa Hodgson alisisitiza kuwa hataacha kuwa mkufunzi wa Uingereza, naye Greg Dyke, mkuu wa shirikisho la soka la Uingereza (FA), akimhakikishia Hogson kuwa kibarua chake hakijaota nyasi.
Uingereza watamaliza kampeni yao dhidi ya Costa Rica siku ya Jumanne

Thursday, June 12, 2014

BRAZIL 2014: WELBECK AZUA HOFU KATIKA TIMU YA ENGLAND

danny_31db2.jpg
Timu ya England imepata mshituko baada ya nyota wake, Danny Welbeck kuumia juzi wakati wa mazoezi kujiandaa kwa mchezo wao wa kwanza wa Fainali za Kombe la Dunia Jumamosi dhidi ya Italia.
Inasadikiwa, mshambuliaji huyo wa Manchester United mwenye miaka 23, ana tatizo la misuli ya nyuma ya mguu aliyoumia katika mazoezi ya England kwenye kambi ya jeshi ya Urca juzi.
Na kama ataondolewa kikosini, itaongeza nafasi kwa winga wa Liverpool, Raheem Sterling kucheza dhidi ya Waitaliano katika mchezo huo mjini Manaus.
Welbeck amefunga mabao manane katika michezo 20 aliyocheza akiwa chini ya kocha wa England, Roy Hodgson.
Kukosekana kwa Welbeck kutakuwa tatizo la msingi kwa Hodgson, ambaye amekuwa shabiki mkubwa wa mchezaji huyo kijana.
Sterling ni mchezaji muhimu katika mchezo huo wa Jumamosi kutokana na kazi kubwa aliyoonyesha mazoezini, lakini Hodgson amekuwa akitaka kumtumia nyuma ya Daniel Sturridge kwa pamoja wakisaidiwa na Wayne Rooney katika upande wa kushoto.
"Wakati wote unapotaka kuchagua wachezaji wa kuanza au wa kutowatumia lazima uwe na sababu ya msingi," alisema Hodgson

MAJAMBAZI YATEKA KITUO CHA POLISI NA KUUA

chagonja_5602f.gif
Mkuranga na Dar. Hili linawezekana kuwa ni tukio la kwanza na la aina yake. Majambazi wanaokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu, juzi walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo na kujeruhi mgambo mwingine na kisha kupora bunduki tano na risasi 60 usiku wa kuamkia juzi.
Polisi aliyeuawa ni Konstebo Joseph Ngonyani na majeruhi Venance Francis na Mariamu Mkamba ambao walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya Mkuranga kwa matibabu.
Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, majambazi hayo yalikuwa na taarifa kwamba kituo hicho kina silaha za moto na kuweka mpango wa kukivamia usiku baada ya kupiga hesabu na kujiridhisha kwamba polisi kutoka Kibiti, wilayani Rufiji au Mkuranga wasingeweza kufika hapo kabla ya wao kutekeleza azma yao...(E.L)..
Mkazi wa Kimanzichana, Mohamedi Muba alisema wananchi wenzake walimwambia kuwa majambazi hayo yalifika kituoni hapo saa saba usiku na kuvamia kituo hicho wakitaka funguo za kufungulia stoo zilipohifadhiwa silaha.
"Kituo cha Kimanzichana kipo mbali sana na vituo vingine vya Kibiti na Mkuranga, ni kama kilometa 30 hadi 35, hivyo kwa wakati huo wa usiku wa manane ingekuwa vigumu kuwahi kutoa msaada," alisema mkazi mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mkazi huyo alisema baada ya kubishana na askari huyo aliyekuwa na ufunguo, majambazi hayo yalitumia nguvu kumlazimisha kutoa funguo.
Huku mzozo huo ukiendelea, majambazi wengine walikuwa wakiwashambulia askari mgambo kwa mapanga na walipoona askari amegoma kutoa funguo walimpiga risasi na kuzichukua kisha kufungua na kuchukua silaha na kutokomea kusikojulikana.
Alisema majambazi hayo yalionekana kujipanga na kuwa na taarifa zote kuhusu hali ya ulinzi katika kituo hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema ameagizwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja kwamba ndiye atakayelizungumzia suala hilo.
"Kwa sasa nipo chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ninashughulikia mwili wa askari aliyeuawa, Makao Makuu watalizungumzia zaidi," alisema Kamanda Matei.
Chagonja alonga
Akizungumzia tukio hilo jana, Chagonja alisema majambazi hayo yalitumia bunduki na mapanga kumuua askari huyo na kuwajeruhi mgambo hao na kutokomea na bunduki mbili aina ya Sub Mashine Gun (SMG), mali ya Jeshi la Polisi na bunduki tatu aina ya shortgun, mali ya raia ambazo zilikuwa kituoni hapo zikisubiri kupelekwa kwenye ghala kuu la silaha.
"Polisi inalaani vikali kitendo hicho na imeanzisha msako mkali na itahakikisha inayatia mbaroni majambazi hayo," alisema Chagonja.
Aliwaomba wananchi wenye taarifa za wahalifu hao kujitokeza au kupiga simu ili waweze kuyakamata na kuyafikisha mahakamani na kupata silaha hizo. Alitoa namba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Ernest Mangu na ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ambazo ni 0754 785 557 na 0715 009 953 kwa ajili ya kutoa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa watu wenye silaha au wanaotiliwa shaka kuhusiana na tukio hilo.
"Kwa sasa wananchi wawe watulivu, waendelee na shughuli zao lakini wafahamu muda wote polisi hatutalala, tutayasaka usiku na mchana na tutahakikisha tunayatia mbaroni," alisema.
Kimanzichana na Mkuranga
Habari za majambazi hayo kuvamia kituo hicho zilisambaa haraka mapema asubuhi kutokana na msako mkali ulioanza kufanywa muda mfupi baada ya tukio hilo.
Madereva wanaotumia barabara ya Dar es Salaam - Kilwa walisema magari yote yalisimamishwa katika vizuizi na kupekuliwa.
"Kila gari lililopita katika Kijiji cha Kimanzichana lilifanyiwa upekuzi ili kutafuta silaha hizo, ukikutwa na mkaa au mbao kazi unayo," alisema dereva wa daladala, Hussein Ali.
Alisema kutokana na msako huo, madereva wengi walisitisha safari na dereva mmoja alisikika akimweleza mwenzake aliyekuwa akielekea huko... "Usiende Mkuranga leo kuna msako mkali, usipokutwa na mkaa au mbao gari lako hata likiwa na tatizo dogo tu utakamatwa

KINDUMBWENDUMBWE CHALIA!! BRAZIL 2014 MTOTO HAPATI USINGIZI

br_58f05.jpg
Wenyeji Brazil watapambana na Croatia katika mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia usiku wa leo saa Tano saa za Afrika Mashariki.
Brazil wanatarajia kuanza na kikosi kile kile kilichoichapa Spain katika fainali ya Kombe la mabara -Confederation- mwaka jana.
Hii inamaanisha Oscar huenda akaanza licha ya 'form' yake kupungua hivi karibuni, na licha ya vyombo vya habari vya Brazil kumpendekeza Willian.
Croatia hawatakuwa na Mario Mandzukic anayetumikia adhabu, hivyo Nikica Jelavic au Eduardo huenda wakaanza

Wednesday, June 11, 2014

MGOGORO:-MUFTI WA TANZANIA SHAABAN SIMBA AONGOZA BAADHI YA WAISLAM KUVUNJA MILANGO YA MSIKITI MKUU WA IJUMAA TABORA

Baadhi ya waumini wa dini ya kiislamu msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni mjini Tabora wakati wa tukio la kuvunjwa milango ya msikiti huo unaodaiwa kufungwa na baadhi ya viongozi walioondolewa madarakani na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Issa Simba kwa madai ya kukiuka utaratibu wa Baraza kuu la Waislam Tanzania Bakwata,ambapo Mufti aliongoza tukio la kuvunja milango ya msikiti huo jambo ambalo lilipingwa vikali na baadhi ya waumini wanaowaungamkono viongozi waliosimamishwa akiwemo Sheikh mkuu wa mkoa wa Tabora Shaban Salum.
Mara baada ya kuvunjwa kwa msikiti huo huku kukiwa na ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi Mufti Shaban Simba aliingia ndani na kuzungumza na baadhi ya waumini ambapo aliendelea na msimamo wa kumsimamisha Sheikh wa mkoa wa Tabora Shaban Salum hatua ambayo imeendelea kulalamikiwa na idadi kubwa ya waumini wa dini ya kiislam hasa wanaofanya ibada katika msikiti huo wa Ijumaa.
Mufti Shaaban Issa Simba akiwa ndani ya msikiti wa Ijumaa baada ya kuvunjwa licha ya kuwa katika milango ya msikiti huo kulikuwa na hati ya mahakama ya kulalamikiwa kwa Mufti huyo.

Baadhi ya waumini nje ya msikiti walikuwa wakihojiwa na waandishi wa habari ambapo wameendelea kumlalamikia kiongozi huyo mkubwa wa waislam nchini kwa hatua ya kumsimamisha Sheikh wa mkoa wa Tabora jambo ambalo wamedai kuwa ni moja ya hatua ya kuidhalilisha dini ya kiislam kwakuwa suala hilo lingetafutiwa ufumbuzi kwa vikao vya ndani na kwakuzingatia busara zaidi kuliko hali ilivyokuwa

BLATTER: WANAOPINGA QATAR WABAGUZI WA RANGI ASEMA BLATTER

blatter_71b68.jpg
Sao Paulo, Brazil. Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Sepp Blatter amesema madai ya rushwa katika kuipa Qatar uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za 2022 yamechochewa na hisia za ubaguzi wa rangi.
Blatter alisema haya alipokuwa akijibu madai wanayorushiwa baadhi ya wanakamati wa Fifa waliohusika na uamuzi huo, wanaokabiliwa na tuhuma za rushwa.
"Kuna kimbunga kimeelekezewa Fifa tangu iichague Qatar. Inasikitisha sana kwamba yote yamechochewa na hisia za ubaguzi hasa wa rangi," Blatter.
Blatter alisema hayo mjini Sao Paulo, Brazil alipokuwa akizungumza na maofisa kutoka Afrika.
Aliahidi kuwa Fifa itakabiliana na chochote kinachobeba hata chembe ya kibaguzi.
Hata hivyo, Fifa imeamua kufanya uchunguzi wake na imesema taarifa ya uchunguzi itatolewa kati ya Septemba na Oktoba.
Katika kikao chao cha Sao Paulo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) nalo lilitoa cheche zake kwa vyombo vya habari vya kimataifa hasa magazeti ya Uingereza likisema ndiyo yaliyoanza kampeni hiyo dhidi ya Qatar na ya kuchafua jina la shirikisho hilo.
Wametaja suala hilo kuwa ni kampeni iliyojaa chuki na udhalilishaji. Wametishia kuyafungulia kesi magazeti husika.
Mwendesha mashtaka wa zamani wa Marekani, Michael Garcia anayeongoza kitengo cha uchunguzi cha Kamati ya Maadili, ndiye anayechunguza kashfa hiyo.
amekuwa akichunguza utaratibu na vipi nchi zinavyochaguliwa kuandaa kombe hilo na atatoa ripoti yake hapo Julai.
Qatar ilishinda Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani hapo Desemba 2010 ilipochaguliwa na Fifa kama mwenyeji wa Kombe la Dunia 2022.
Qatar imekana vikali kuhusika na vitendo vyo vyote vya rushwa na kusema kuwa ilishinda kihalali

MALAWI IMEANZA KUWATISHA WATANZANIA ASEMA MBUNGE

peter f1df1
Na MABANTANYAU FAMILY
"Kwa kuzingatia uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Malawi, naomba mwongozo wako maana ndege za Malawi sasa zinaingia hadi Tanzania na kuwatia hofu wananchi," alisema Kibona.
Kauli ya mbunge huyo imekuja wakati msimamo rais wa Malawi, Profesa Peter Mutharika kuhusu mzozo uliopo kati ya nchi hiyo na Tanzania kuhusu Ziwa Nyasa ukiwekwa bayana hatakuwa na mjadala kuhusu mpaka wa nchi hizo akidai kuwa Ziwa Nyasa ni la Malawi pekee.
Kibona alisema kwa takriban wiki mbili sasa, ndege hizo zimekuwa zikionekana upande wa Tanzania, lakini hakuna kauli yoyote iliyotolewa na Serikali mpaka sasa.
Katika mwongozo wake, Spika Anne Makinda alisema: "Jambo hili ni umuhimu sana hivyo Serikali ni lazima Serikali ijipange ili kulijibu." Aidha, Naibu Spika Job Ndugai aliongeza: "Hili jambo ni zito na Serikali haiwezi kukurupuka kujibu. Kwanza lazima majibu hayo yamfikie Rais Jakaya Kikwete."
Profesa Mutharika, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Democratic Progressive (DPP), anapinga kuendelea kujadiliana na Tanzania kuhusu nani mwenye haki ya kumiliki Ziwa Nyasa, msimamo aliutoa kwa wananchi wa Chipoko, kando ya ziwa hilo miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu ambao ulimwigiza madarakani.
"Hakuna haja ya kuendelea kujadiliana. Ziwa Malawi ni mali ya Malawi na litaendelea kuwa la Malawi daima," aliwaambia wananchi hao huku akimshutumu mtangulizi wake, Joyce Banda kwamba alikuwa dhaifu kiasi cha kutoa fursa kwa Tanzania kutumia udhaifu huo kutaka kupora ziwa hilo.
Hata hivyo, akizungumza bungeni wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake, waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema Tanzania ilikuwa ikifuatilia kwa karibu uchaguzi wa Malawi na kwamba iko tayari kufanya kazi na serikali yoyote itakayoingia madarakani.
Juhudi za usuluhishi wa mzozo huo zinafanyika chini ya uongozi wa rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano akisaidiwa na rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.