Monday, May 12, 2014

VITA VYAZUKA TENA SUDAN KUSINI

Saa chache tu baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa usitishaji mapigano nchini Sudan kusini Malumbano yameibuka .
Sasa Serikali na wapiganaji wa Sudan Kusini wanalaumiana kila upande ukimshutumu mwenzake kuvunja makubaliano hayo yaliyosainiwa ijumaa.
Hata hivyo kiongozi wa waasi Riek Machar anasema bado ameazimia kutekeleza makubaliano hayo licha ya kwamba anasema serikali ya rais Salva Kiir inavunja mapatano hayo.
Machar amesema kuwa majeshi ya UPDF ya Uganda ambayo yamekuwa yakivamia maeneo inayoyadhibiti haijaafiki mkataba uliotiwa sahihi huko Adiss Ababa kati yake na Rais Salva Kiir.(P.T)
Aidha msemaji wa jeshi la serikali, Kanali Philip Aguer, amesema waasi hao wameshambulia maeneo ya serikali katika mji wa Bentiu .
Upinzani umepinga madai hayo.
Machar ameiambia BBC kuwa angetaka mazungumzo zaidi na serikali kuhusu hilo, lakini amesema anafahamu kuwa Rais hana uwezo wa kudhibiti majeshi yote yanayopigana kwa upande mmoja na majeshi ya serikali kama vile majeshi ya Uganda na wapiganaji kutoka Darfur.
Serikali ya Sudan Kusini pia imelaumu upande wa waasi kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano saa chache tuu baada ya mkataba huo kutiwa saini.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalitiwa saini Ijumaa, na yalikusudiwa kumaliza vita vya miezi mitano ambavyo vimeuwa maelfu ya watu na kulazimisha zaidi ya milioni moja kuhama makwao

No comments:

Post a Comment