Tuesday, May 27, 2014

AMWAGA MACHOZI MAHAKAMANI BAADA YA KUKUTWA NA UNGA

Dar es Salaam. Hatimaye bibi raia wa Nigeria aliyekamatwa na dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA), jana aliangua kilio baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya.
Bibi huyo, Olabis Ibidun Cole (65) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Lagos nchini Nigeria, ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mshtakiwa wa dawa za kulevya mwanamke mwenye umri mkubwa.(Martha Magessa)
Alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.
Mshtakiwa huyo alianza kutoa machozi na kulia kwa sauti ya chini baada ya kesi yake kuahirishwa hadi leo kutokana na kukosekana kwa mkalimani wa lugha yake.
Awali mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi (Inspekta) wa Polisi Jackson Chidunda na baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Frank Moshi alimwambia hatakiwi kujibu chochote na kwamba kama ana maombi ya dhamana atawasilisha Mahakama Kuu.
Hata hivyo, baada ya Hakimu Moshi kumuuliza kama ameelewa, mshtakiwa huyo alijibu kuwa hajaelewa kwa kuwa lugha ya Kiingereza iliyotumika kumsomea mashtaka haielewi vizuri. Hakimu Moshi alilazimika kuahirisha kesi hiyo hadi leo ili aweze kusomewa mashtaka tena baada kupatikana kwa mkalimani anayejua lugha ya Kiyoruba.
Awali, Mkaguzi Chidunda alidai mshtakiwa alikamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroine zenye thamani ya Sh37 milioni.
Chidunda alidai kuwa siku ya tukio saa 9:00 jioni katika uwanja huo alikutwa na gramu 831 za dawa za kulevya aina ya Heroin zenye thamani ya Sh 37milioni.
Mshtakiwa alirudishwa rumande hadi leo kesi yake itakapokuja kwa ajili ya kusomwa. Alikamatwa katika uwanja huo akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

No comments:

Post a Comment