Thursday, May 29, 2014

‘SIJAVURUGA NDOA YA VICKY KAMATA’ Charles

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Sinza jijini Dar es Salaam, Kamata alisema ingawa ndoa hiyo haijafungwa, moyo wake una amani kwa kuwa alimwomba Mungu kuhusu suala hilo kwa muda mrefu na hicho ndicho Mungu alichojibu.PICHA|MAKTABA 
Dar es Salaam. Suala la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata limechukua sura mpya baada ya mzazi mwenza wa mchumba wa mbunge huyo, kukanusha taarifa kwamba alikwenda Dodoma kwa lengo la kuomba msaada kwa viongozi wa Bunge. (FS)

Kauli ya mama huyo imezidisha utata katika sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa hiyo iliyokuwa ifanyike Jumamosi baada ya kutokea habari kuwa mwanamke mmoja alikwenda bungeni mjini Dodoma kutaka kuonana na Spika kwa lengo la kuomba Bunge limsaidie kupata haki yake kabla ya harusi hiyo kufungwa na hivyo kusababisha harusi kutofanyika.
Kamata, ambaye alijizolea umaarufu kutokana na wimbo wake wa “Wanawake na Maendeleo” na baadaye kuingia bungeni katika uchaguzi wa mwaka 2010, alikuwa afunge ndoa na mtu aitwaye Charles Gardiner Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam, lakini haikufanyika kutokana na mbunge huyo kuwa mgonjwa kiasi cha kulazwa hospitali maeneo ya Tabata.
Jana, Kinavi Dadi, ambaye ni mzazi mwenza wa Gardiner, alikanusha kufunga safari hadi Dodoma kwa lengo hilo.
“Ni kweli kwamba Charles ni baba watoto wangu, lakini sijawahi kwenda Dodoma na wala sifahamu chochote kuhusu safari hiyo. Nadhani inatosha,” alisema mama huyo na hakutaka mazungumzo zaidi.
Baadaye kidogo mmoja wa ndugu wa Kinavi, ambaye aliomba asitajwe jina lake gazetini, alikiri ndugu yao kufunga ndoa na Gardiner Juni 2004 na kujaliwa kupata watoto wawili, lakini walitofautiana na baadaye ndoa yao kuvunjwa mwaka 2012.
“Ni kweli kwamba dada yetu alifunga ndoa na Charles, lakini pia ni kweli kwamba walipeana takala halali two years ago (miaka miwili iliyopita), kwa hiyo taarifa kwamba eti amezuia ndoa isifungwe, siyo za kweli na wala huko Dodoma hajawahi kwenda,” alisema.
Alisema taarifa kwamba aliyepata kuwa mke wa Gardiner alikwenda Dodoma kuomba msaada wa Bunge zimewaumiza sana kama familia kutokana ukweli kwamba Kinavi ndiye anayefahamika kuwa mke wa kwanza.
“Ndugu yetu analia sana kutokana na kuumizwa na wale wanaomchafua. Sisi katika familia tumelelewa kwa maadili hivyo Kinavi siyo mtu wa kuzuia ndoa ya Gardiner maana walishatengana, mawasiliano yaliyopo ni yale yanayohusu watoto ambao wana haki ya wazazi wote wawili. Hatujui waliozitangaza hizo habari walikuwa na malengo gani,” alisisitiza.
Bungeni Dodoma
Wakati hayo yakiendelea, habari kutoka bungeni Dodoma zinasema mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wa Gardiner ni ‘feki’ na alikuwa wa kutengenezwa na baadhi ya wabunge kwa lengo la kumtibulia Kamata.
Mpango huo unadaiwa kuwahusisha wabunge wanawake wanne; watatu kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka Chadema ambao awali waliapa kwamba ndoa ya mbunge mwenzao isingefungwa

MAYA ANGELOU AFARIKI DUNIA

Maya Angelou
Maya Angelou, enzi za uhai wake. Picha imepigwa November 3, 1971.
Maya Angelou, mshairi mashuhuri, mwandishi na mtetezi wa haki nchini Marekani amefariki akiwa na umri wa miaka 86.
Angelou aliyepata umaarufu katika miaka ya 1970 kwa kitabu chake cha "I know why the caged bird sing" alifariki huko Winston-Salem katika jimbo la North Carolina nchini Marekani.
Alizaliwa huko St.Louis , Misouri na alilelewa katika jimbo la Arkansas. Baada ya kubakwa akiwa mdogo aliacha kuongea kwa muda wa miaka mitano. Baadae katika maisha yake alifanya kazi mbalimbali kama vile mhudumu wa hoteli, mpishi na pia kondakta kwenye mabasi.
Maya hakupoteza upendo wake wa sanaa, muziki, uigizaji na dansi. Uandishi wake ulianza wakati ambapo mwandishi mmoja maarufu, m-Marekani mweusi James Baldwin aliposikia mambo aliyoyapitia Maya akiwa bado mdogo na kumhimiza aandike kitabu.
Mwaka 1993 aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton alimuomba bi.Angelou aandike shairi lililosomwa katika sherehe za kuapishwa kwa Clinton kuwa Rais wa Marekani

Wednesday, May 28, 2014

DARASA LA SABA KUANZA MTIHANI WA MOKO LEO

Na MABANTANYAU FAMILY
Wanafunzi 3,264 wa Darasa la Saba Mkoani Iringa leo wameanza Mtihani wa Tathimini ya mwaka(MOKO) katika ngazi ya Halmashauri Mkoani humo.
Kwanza Jamii radio ikizungumza  na Afisa Elimu wa Manispaa ya Iringa, Halfani Omari Masukira kwa niaba ya Mkurungezi wa Manispaa, Telesia Mahongo  amesema asubuhi leo hii, mtihani huo utafanyika siku mbili kuanzia tarehe ya leo  28 hadi 29 Mei mwaka huu kwa kufanya mtihani wa masomo matano ikiwemo Kiswahili, Kingereza, Hisabati, Sayansi na Somo la Maarifa ya Jamii.
Masukira amesema, lengo la Mtihani huo ni kuwapima Wanafunzi hao ili kuweza kujiridhisha na kuwaandaa katika kufanya vizuri mtihani wao wa Taifa utakaofanyika Septemba Mwaka huu.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wazazi kuwapa nafasi watoto wao ya kujisomea pamoja na kushirikiana na walimu katika malezi bora ya watoto hao.

Tuesday, May 27, 2014

MSANII BONGO MOVIES 'RACHEL' AFARIKI!


Msanii wa Bongo Movie, Rachel Haule 'Recho' (pichani), amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es slaaam. Habari zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa Bongo Movie, Steve Nyerere, zimesema kuwa Recho alikwenda Muhimbili jana kujifungua ambapo mara baada ya kujifungua mtoto alifariki na yeye hali yake kuwa mbaya, ilibidi ahamishiwe ICU ambako hali ilizidi kuwa mbaya na baadae kufariki dunia

AFYA YA ‘MTOTO WA BOKSI’ YABADILIKA GHAFLA, KULETWA DAR LEO

Morogoro. Hali ya mtoto Nasra Rashid (4) aliyekuwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka minne, imebadilika ghafla juzi na jana kuwalazimu madaktari kumweka katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.(Martha Magessa)
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alisema jana kuwa tatizo kubwa la mtoto huyo ni kubadilika ghafla kwa upumuaji wake na utaratibu unafanyika ili leo asafirishwe kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
"Tunatarajia kumpeleka Muhimbili mapema asubuhi kwa gari maalumu la wagonjwa ili kupata matibabu zaidi," alisema Dk Lyamuya.
Alisema juzi Nasra alikuwa mwenye furaha na mchangamfu lakini jioni yake hali ilibadilika katika mfumo wake wa kupumua.
Alisema kwa msingi huo, uongozi wa hospitali ya mkoa umeamua kumsafirisha kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.
Uchunguzi wa awali wa afya ya Nasra ulibaini kuwa mtoto huyo alikuwa na maradhi ya nimonia (kichomi), mifupa ya miguu na mikono kuvunjika pamoja na utapiamlo.
Watuhumiwa kortini
Katika hatua nyingine, watu watatu akiwamo baba mzazi wa Nasra, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro kujibu mashtaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
Baba wa mtoto huyo Rashid Mvungi (47), mama mlezi wa Nasra, Mariamu Said (38) na mumewe Mtonga Omar (30), walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo jana na kusomewa mashtaka hayo.
Wakili wa Serikali, Sunday Hyera alidai kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Desemba, 2010 na Mei mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.
Alidai kuwa katika kipindi hicho walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na hivyo kumsababishia magonjwa.
Alitaja maradhi yaliyomkumba akiwa ndani ya boksi ni utapiamlo, kichomi na mvunjiko wa mifupa.

AMWAGA MACHOZI MAHAKAMANI BAADA YA KUKUTWA NA UNGA

Dar es Salaam. Hatimaye bibi raia wa Nigeria aliyekamatwa na dawa za kulevya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA), jana aliangua kilio baada ya kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya.
Bibi huyo, Olabis Ibidun Cole (65) ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Lagos nchini Nigeria, ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mshtakiwa wa dawa za kulevya mwanamke mwenye umri mkubwa.(Martha Magessa)
Alipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.
Mshtakiwa huyo alianza kutoa machozi na kulia kwa sauti ya chini baada ya kesi yake kuahirishwa hadi leo kutokana na kukosekana kwa mkalimani wa lugha yake.
Awali mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi (Inspekta) wa Polisi Jackson Chidunda na baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Frank Moshi alimwambia hatakiwi kujibu chochote na kwamba kama ana maombi ya dhamana atawasilisha Mahakama Kuu.
Hata hivyo, baada ya Hakimu Moshi kumuuliza kama ameelewa, mshtakiwa huyo alijibu kuwa hajaelewa kwa kuwa lugha ya Kiingereza iliyotumika kumsomea mashtaka haielewi vizuri. Hakimu Moshi alilazimika kuahirisha kesi hiyo hadi leo ili aweze kusomewa mashtaka tena baada kupatikana kwa mkalimani anayejua lugha ya Kiyoruba.
Awali, Mkaguzi Chidunda alidai mshtakiwa alikamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroine zenye thamani ya Sh37 milioni.
Chidunda alidai kuwa siku ya tukio saa 9:00 jioni katika uwanja huo alikutwa na gramu 831 za dawa za kulevya aina ya Heroin zenye thamani ya Sh 37milioni.
Mshtakiwa alirudishwa rumande hadi leo kesi yake itakapokuja kwa ajili ya kusomwa. Alikamatwa katika uwanja huo akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

Monday, May 12, 2014

VITA VYAZUKA TENA SUDAN KUSINI

Saa chache tu baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa usitishaji mapigano nchini Sudan kusini Malumbano yameibuka .
Sasa Serikali na wapiganaji wa Sudan Kusini wanalaumiana kila upande ukimshutumu mwenzake kuvunja makubaliano hayo yaliyosainiwa ijumaa.
Hata hivyo kiongozi wa waasi Riek Machar anasema bado ameazimia kutekeleza makubaliano hayo licha ya kwamba anasema serikali ya rais Salva Kiir inavunja mapatano hayo.
Machar amesema kuwa majeshi ya UPDF ya Uganda ambayo yamekuwa yakivamia maeneo inayoyadhibiti haijaafiki mkataba uliotiwa sahihi huko Adiss Ababa kati yake na Rais Salva Kiir.(P.T)
Aidha msemaji wa jeshi la serikali, Kanali Philip Aguer, amesema waasi hao wameshambulia maeneo ya serikali katika mji wa Bentiu .
Upinzani umepinga madai hayo.
Machar ameiambia BBC kuwa angetaka mazungumzo zaidi na serikali kuhusu hilo, lakini amesema anafahamu kuwa Rais hana uwezo wa kudhibiti majeshi yote yanayopigana kwa upande mmoja na majeshi ya serikali kama vile majeshi ya Uganda na wapiganaji kutoka Darfur.
Serikali ya Sudan Kusini pia imelaumu upande wa waasi kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano saa chache tuu baada ya mkataba huo kutiwa saini.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yalitiwa saini Ijumaa, na yalikusudiwa kumaliza vita vya miezi mitano ambavyo vimeuwa maelfu ya watu na kulazimisha zaidi ya milioni moja kuhama makwao

KURA YA MAONI KATIKA MAJIMBO YA UKRAINE

Katika majimbo ya Donetsk na Luhansk yaliyoko mashariki mwa Ukraine , raia wamepiga kura katika uchaguzi wa kura za maoni usio rasmi ulioandaliwa na makundi yanayounga mkono Urusi .
Waandalizi wa uchaguzi huo katika jimbo la Donetsk wametangaza kile walichosema ni matokeo ya mwisho saa chache kabla ya kufunga vituo vya kupigia kura.
Wanasema karibu asilimia tisini ya watu wamepiga kura ya ndio kuunga mkono azma ya kujitawala katika uchaguzi ulioshirikisha asilimia sabini na tano ya wapiga kura.
Wapiganaji waliifyatua risasi katika eneo moja ambapo kundi lingine la wapiganaji wanaounga mkoni serikali waliripotiwa kufunga baadhi ya vituo vya kupigia kura.(P.T)
Hili lilikua tukio la kipekee.
Kwa jumla shuguli ya upigaji kura katika maeneo mengi ya Donetsk na Luhansk ambayo yako mpakani mwa Ukraine na Urusi.
Hatahivyo waandishi wa BBC waliotembelea baadhi ya vituo wanasema shughuli yenyewe haikufikia viwango vya kimataifa .
Hakukua na orodha ya wapigaji kura na watu walipewa makaratasi ya upigaji kura baada ya kutoa vitambulisho.
Katika kituo kimoja mwanamke mmoja alionekana akipiga kura mara mbili.
Serikali ya Ukraine imeitaja kura hiyo kama usiyohalali lakini Kamishna wa uchaguzi Roman Lyagin amesesitiza kuwa matokeo hayo ni sauti ya raia wenye haki ya kusikilizwa.
Kura hiyo ya maoni imefanyika licha ya wito wa Rais wa Urusi Vladmir Putin kutaka iahirishwe.
Viongozi wa nchi za Magaribi wanamlaumu kwa kusababisha mgawanyiko nchini Ukraine.
Muungano wa Ulaya umesema kura hiyo ya maoni sio halali na unajiandaa kuendelea kuishinikiza Urusi kwa kuongeza vikwazo vilivyowekwa baada ya Moscow kulitwaa eneo la Ukraine la Crimea

DAKTARI BINGWA AFA KWA DENGUE

Dar es Salaam. Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili nchini, Gilbert Buberwa amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa dengue.
Kifo cha Dk Buberwa kinafanya idadi ya watumishi wa afya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo kufikia wawili baada ya muuguzi Hamida Likoti kufariki dunia wiki iliyopita. (J M)
Ugonjwa huo uliolipuka mkoani Dar es Salaam, umezua taharuki kwa wakazi wake kwa sababu hauna tiba na unasababishwa na mbu, Aedes Egyptae, anayeuma mchana na anayeweza kuzaliana katika majisafi yaliyotuama.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Primus Saidia alisema jana kuwa Dk Buberwa alifariki dunia saa saba usiku wa kuamkia jana akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Dk Buberwa alianza kuumwa ugonjwa huo akiwa kazini katika Hospitali ya Temeke na kulazwa na hali yake ilipobadilika, alihamishiwa MNH kwa matibabu zaidi.
"Kadiri siku zilivyozidi kwenda alibainika kwamba viungo vyake muhimu, yaani ini na figo vimeharibika, hivyo alisafishwa figo huku akiwa amelezwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU).
Dk Saidia alikumbusha kuwa virusi vya dengue havina tiba isipokuwa dalili zake ambazo ni homa, kuumwa kichwa na viungo vya mwili – ndizo zenye tiba.
Dk Buberwa alianza kuugua Mei 3, mwaka huu na siku iliyofuata alipelekwa hospitali na mkewe ambako alilazwa ili kupata uangalizi wa karibu wa madaktari wenzake.
Kaka wa marehemu, Wakili Nickson Ludovick alisema: "Tunasubiri ndugu kutoka Bukoba na Musoma kwa mazishi yatakayofanyika hapa Dar es Salaam katika makaburi ya Kinyerezi keshokutwa."
Madaktari, wauguzi walazwa
Dk Malima alisema hadi jana, wafanyakazi tisa wa Hospitali ya Temeke walikuwa wamelazwa kutokana na homa hiyo.
Alisema wafanyakazi hao ni madaktari watano, wauguzi watatu na mtaalamu mmoja wa maabara. "Kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita tumepokea wagonjwa wa dengue waliothibitika 15," alieleza Dk Malima. 

MANCHESTER CITY MABINGWA WAPYA ENGLANAD

http://www.ibn-tv.com/wp-content/uploads/2014/03/Man-City.jpg
Manchester City waifunga West Ham goli 2-0 katika mechi iliyokwisha muda mfupi uliopita. Mashabiki wavamia uwanja kwa furaha ya ubingwa. Matokeo mengine: Liver 2-1 New Castle,Card 1-2 Chelsea, Hull 0-2, Everton South 1-1 Man Utd, Tot 3-0 Villa, Norw 0-2 Arsenal, Fulh 2-2 Crystal, Sunder 1-3 Swan, WBM 1-2 Stoke.