Monday, January 6, 2014

Soma Kwa Makini Majibu ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini zitto

 Mbunge wa Kigoma Kaskazini -Chadema Zitto Kabwe

---
Our Ref: ZZK/12/13 10.12. 2013.
Mh. Katibu MKuu, 
Chama Cha Demokrasia Na Mendeleo
 HSE NO 170, UFIPA STREET, KINONDONI 
S. L. P 31191 Dar es Salaam – Tanzania. 

Rejea barua yako ya tarehe 26 Novemba 2013 yenye kumbukumbu no C/HQ/ADM/KK/08/31 Iliyoelezea maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha tarehe 20-22 Novemba 2013, kiliazimia kwamba niachishwe nafasi zote za uongozi ninazoshikilia katika chama na kwamba Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe dhidi yangu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za 6.5.2(d), ningependa kuwasilisha majibu ya mashtaka hayo kama ifuatavyo; 

1.0 MAELEZO YA AWALI; Napenda kuwasilisha utetezi wangu huku nikiwa napinga utaratibu uliotumika kuandaa na kunifikishia mashtaka husika (Defence Under Protest) kwa sababu zifuatazo; 

1.1. Hatua za kinidhamu ambazo kimsingi ni adhabu zimeshachukuliwa na Kamati Kuu kwa mashtaka haya haya ambayo nimepatiwa. Kama barua yako inavyosema na nanukuu maneno yako “Kamati Kuu kwa kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(d) ya Kanuni za Uendeshaji Shughuli za Chama (‘Kanuni za Uendeshaji’), iliazimia kwamba muachishwe nafasi zote za uongozi mnazoshikilia katika Chama…” (msisitizo ni wangu). Mheshimiwa Katibu Mkuu; Ni wazi kabisa kwamba adhabu ya kuachishwa nafasi zote za uongozi imeshatekelezwa. Kamati Kuu imeshanitia hatiani kwa makosa haya haya ambayo sasa hivi natakiwa nijitetee. Binafsi siamini kwamba kwa utaratibu huu haki itatendeka na inaonekana kutendeka. Ni vigumu sana kusema kwamba haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kujitetea imelindwa wakati tayari adhabu imeshatolewa na chombo kile kile ninachotakiwa kujitetea mbele yake. 

1.2. Kama kiongozi ambaye nimeadhibiwa na Kamati Kuu ninayo haki ya kukata rufaa Baraza Kuu dhidi ya haya yafuatayo; 
1.2.1. utaratibu uliotumika na Kamati Kuu kunivua nyadhifa zote za uongozi. 
1.2.2. sababu zilizotumika kunivua nyadhifa zote za uongozi. 

Mheshimiwa Katibu Mkuu; 


Katiba ya Chama pamoja na Kanuni za Uendeshaji zinatoa HAKI hii ya msingi na UTARATIBU kwa maneno haya; 

Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama; “Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”. 

Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama; “Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wa siku thelathini tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa adhabu”. Mheshimiwa Katibu Mkuu; Kanuni za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa ufuatwe ili kiongozi aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa maneno haya; Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji; “Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la” 

Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji; “Mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabu” Kanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji; “Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo lazima ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi”

Mheshimiwa Katibu Mkuu;

Mpaka tarehe 01/12/2013 siku ambayo nimepokea barua yako ya mashtaka dhidi yangu sijapokea taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu na pia taarifa kamili ya mwenendo wa shauri langu haujawasilishwa Baraza Kuu. Wakati hayo yote hayajafanyika natakiwa kutoa utetezi wangu wa maandishi kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(a) ikisomwa pamoja na Kanuni ya 6.5.6 ya Kanuni za Uendeshaji kwa makosa yaleyale ambayo tayari nimeshaadhibiwa na Kamati Kuu. Ni wazi kabisa kwamba barua yako ya mashtaka ni muendelezo wa hatua au maazimio ya Kamati Kuu kama ilivyoandikwa “Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe….” 

Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

Utaratibu uliotumika na Kamati Kuu sio wa HAKI na ni ukiukaji wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji. Nalazimika kutoa utetezi wangu nikiwa napinga (under protest) kwa sababu kwa Chama ambacho kinasifika kwa kupigania misingi ya utawala bora na utawala wa sheria ni lazima kiheshimu haki za wanachama na viongozi wake pamoja na kufuata utaratibu kilichojiwekea wakati wa kuchukua hatua za kinidhamu. 1.3. Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu kwa nyakati mbalimbali wametoa matamko kwamba tumefukuzwa uongozi na hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yetu kabla hata ya ofisi yako kutoa Mashtaka dhidi yetu. Mheshimiwa Tundu Lissu na Mheshimiwa John Mnyika walitoa matamko hayo wakati wakiongea na Waandishi wa Habari.

Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

Kitendo cha wajumbe hao kutoa misimamo kwa niaba ya Chama au Kamati Kuu ni ukiukwaji wa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa. Ni wazi kabisa kwamba tayari hukumu dhidi yangu imeshapitishwa kabla sijasikilizwa. Sina imani na wajumbe ambao tayari wameonyesha waziwazi misimamo yao kuhusu tuhuma dhidi yangu. 

Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

Kutokana na hayo yote ambayo nimeyataja hapo juu naomba ofisi yako isitishe utekelazaji wa maamuzi au maazimio ya Kamati Kuu mpaka pale ambapo nitakuwa nimepatiwa taarifa ya msingi wa maamuzi ya Kamati Kuu na kuweza kukata rufaa ngazi ya juu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji. Hatua zozote za Kamati Kuu zitaendelea kukiuka Katiba na Kanuni za Uendeshaji. 

Bila kuathiri hayo niliyoyasema; 

1 UTETEZI WANGU DHIDI YA MASHTAKA Mheshimiwa Katibu Mkuu; Kwa ujumla nakanusha na kukataa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwangu kuhusu kinachoelezwa kwamba niliandaa mkakati wa mabadiliko 2013, mimi binafsi sijawahi kushiriki, kuhusika kuandaa au kufahamu kwa namna yoyote ile kinachoitwa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 kama ulivyoainisha kwenye barua yako. 

KOSA LA KWANZA 

Kukashifu Chama kiongozi au mwanachama yeyote wa chama kinyume na masharti ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 

2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia yoyote ile. 

3. Kuhusu kutoa kashfa kwa Katibu Katibu Mkuu wa Chama na Mbunge wa Arusha Mjini Mh. Godbles Lema kama ulivyoainisha kwenye barua yako mimi binafsi sijawahi kutoa kashfa hizo na wala kuhusika kwa namna yoyote ile kwenye maandalizi ya mkakati huo wa mabadiliko.

KOSA LA PILI

Kutokuwa wakweli na wawazi wakati wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) Kinyume na Kanuni ya Uendeshaji 10.1 (vii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilianzisha mtandao wa siri ulioitwa “Mtandao wa Ushindi’ ili kuniwezesha mimi kutwaa madaraka ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia zilizo kinyume na Katiba, Kanuni za Uendeshaji na Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa CHADEMA na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012. 
2. Nakanusha kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kuufahamu unaoitwa mtandao wa ushindi kama ilivyoelezwa na barua yako. 
3. Siku zote nimekuwa mkweli muwazi kwa yale ninayoyaamini na katika kutekeleza majukumu yangu kama kiongozi na mwanachama mtiifu wa CHADEMA. Pia sijashirikiana na kikundi chochote cha majungu au wadanganyifu kama iliyoainishwa kwenye barua yako. 


KOSA LA TATU

Kutoa tuhuma juu ya viongozi wenzenu pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni kinyume na Kanuni ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilitoa tuhuma nzito na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji. 
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nilitoa tuhuma nzito na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa n Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.

KOSA LA NNE

Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii na Kanuni ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote chenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambacho kina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii kwa kutumia waraka unaosemekana kuandaliwa nami. 

2. Mimi binafsi sio mdini, mkabila au mkanda na sijawahi kujihusisha na kikundi au mtu yeyote mwenye tabia hizo.

KOSA LA TANO

Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake na kinyume na Kanuni ya 10.1 (x) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake. 

2. Mimi binafsi sikifahamu kikundi chochote ambacho nashutumiwa kujihusisha nacho. 

KOSA LA SITA

Kutekeleza mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo kinyume na kifungu cha 2(g) cha Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba nimetekeleza au kuhusika katika utekelezaji wa mpango wa kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo. 

2. Sijatangaza sehemu yeyote kwamba nitagombea nafasi hiyo na pia vile vile sijatekeleza mpango wowote kama ilivyoelezwa kwenye barua yako.

KOSA LA SABA

Kutengeneza makundi au mitandao ya kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikisha ushindi kinyume nakifungu cha 2(d) cha mwongozo wa kuwania uongozi. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kutengeneza, kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote kwa ajili ya kuniwezesha kuwania uongozi ndani ya chama na kujihakikishia ushindi kutwaa Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume na taratibu.

KOSA LA NANE

Kuwachafua viongozi na wanachama wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume nakifungu cha 2(e) cha Mwongozo wa Kuwania Uongozi. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 

2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama Taifa, kiongozi mwenzangu au mwanachama yeyote Yule. 

KOSA LA TISA

Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kinyume na Kanuni ya 10.3(4) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa mkakati wa kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kwa kuwachafua viongozi wakuu wa Chama yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na Katibu Mkuu kwa tuhuma nzito za uongo na kunipamba mimi. 
2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote.

KOSA LA KUMI

Kukashifu Chama au Kiongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume na Kanuni 2(b) ikisomwa pamoja na Kanuni 3(b) ya Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Wabunge. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana kwa kuandaa na kutumia waraka uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013 nilitengeneza mtandao haramu ndani ya Chama na nilitoa kashfa, matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama. 

2. ambao ulikashifu Chama na/au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni. 

3. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nimekashifu Chama au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni kwa njia yoyote ile.

KOSA LA KUMI NA MOJA

Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume na Kanuni ya 3(f) ya Kanuni za mwenendo na maadili ya Wabunge. Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

1. Mimi kama kiongozi wa Kitaifa sijawahi kutengeneza mtandao haramu ndani ya Chama wala kutoa lugha ya matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama. 

HITIMISHO: 

Mheshimiwa Katibu Mkuu; 

a) Nakanusha kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yangu. Mashtaka yote dhidi yangu sio kweli na sijavunja Katiba au Kanuni za Chama. 
b) Naiomba Kamati Kuu ijiridhishe kwa kiasi kinachostahili kuhusu mashtaka yote niliyoshtakiwa nayo kwa kuangalia ushahidi wote uliotolewa au utakaotolewa dhidi yangu. 
c) Utetezi wangu umetolewa bila kupewa nakala ya Waraka unaosemekana nimeuandaa ilhali kukiwa na maelezo kwamba kuna waraka ‘feki’ na waraka ‘original’ ambao umetumika na Kamati Kuu kufikia maamuzi yake. 
d) Ndugu Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kwa maneno yao wenyewe wametamka kwamba hawakunishirikisa na sikushiriki kwenye uandaaji wa waraka ambao ndio msingi wa mashtaka haya. Kamati Kuu inao ushahidi huo.

Wako katika ujenzi wa Chama,

RAISI KIKWETE AONGOZA MAZISHI YA MGIMWA




 Baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri Wakiwa Wanuingiza Mwili wa wa marehemu Dkt. William Mgimwa

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini kitabu cha maombolezo wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Dkt William Mgimwa viwanja vya Karimjee hall jijini Dar es salaam leo january 5, 2014

  Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete, wakitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dkt. William Mgimwa, wakati wa shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, leo mchana. Mwili huo umesafirishwa leo kuelekea Mkoani Iringa kwa maziko

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji mjane wa marehemu na familia yake wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Dkt William Mgimwa viwanja vya Karimjee hall jijini Dar es salaam leo january 5, 2014

 Rais Jakaya Kikwete, akiifariji familia ya marehemu Dkt. William Mgimwa

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na mkewe Mama Zakia Bilala, wakitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal na mkewe Mama Zakia Bilal, wakiifariji familia ya marehemu Dkt. William Mgimwa, wakati wa shughuli za kuaga na kutoa heshima za mwisho zilizofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam

  Mama Maria Nyerere, akitoa heshima za mwisho.

  Spika wa Bunge Anne Makinda, akitoa heshima za mwisho.

  Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana heshima za mwisho

 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, heshima za mwisho.


 Baadhi ya Mawaziri wakiwa katika foleni kuelekea kutoa heshima zao za mwisho.

Mawaziri wakibeba Jeneza lenye mwili wa marehemu Dkt. William Mgimwa wakati likipakiwa kwenye gari tayari kuanza safari ya kuelekea Uwanja wa ndege kuelekea mkoani Iringa kwa maziko.


  Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakiwa katika shughuli hiyo.



  Baadhi ya viongozi wa Serikali waliohudhuria shughuli hiyo

 Baadhi ya Wabunge waliohudhuria shughuli hiyo.Picha na IKULU na Ofisi ya Makamu wa Rais

SOMA MAAMUZI YA KAMATI KUU YA CHADEMA


 Katibu Mkuu wa Chadema Dr Wilbrod Slaa

---
 CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO

 UTANGULIZI 

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea, kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba. 

Kikao hicho cha dharura kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka dhidi ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha, Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya Mahakama Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.
 
MASHTAKA
Watuhumiwa wote watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko, 2013 kama ifuatavyo:

1.   Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;

2.   Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;

3.   Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila kupitia vikao halali vya Chama;

4.   Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;
5.   Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;

6.   Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa Mwongozo wa Chama;

7.   Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;

8.   Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;

9.   Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;

10.                Kukashifu Chama na viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
11.                Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.

UTETEZI WA WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele yake. 

Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi, licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba – alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na Mwongozo wa Chama.

 Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yake”, na kwamba mashtaka hayo sio ya kweli na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama. 

Aidha, licha ya kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!


USHIRIKI WA ZITTO ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO
Itakumbukwa kwamba katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko. 

Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi. Hata hivyo, wakati wa mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba yeye na waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing juu ya Mkakati na kwamba alikuwa anaufahamu.

 Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka. 


Zaidi ya hayo, baada ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006 unaothibitisha kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo alikataa kata kata kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa. 

Kuhusu tuhuma zao kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za matumizi ya fedha ni siri ya viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa mbali mbali za fedha zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao vya Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi Kabwe. 

Zaidi ya hayo, Dr. Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao husika. Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile katika manunuzi hayo na hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya vifaa hivyo.

 Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr. Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu. 

MAAMUZI YA KAMATI KUU
Baada ya kusikiliza utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa Chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa kutumia tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu, Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la ukombozi. 

Kamati Kuu imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa Chama umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu.

 Mkakati huo ulihusisha pia hujuma dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.

Kwa sababu zote hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
1.    Kwamba kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na 

2.    Kwamba, kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe, viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la CHADEMA.

——————————–
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU

Sunday, January 5, 2014

TIMBWILI LA WANACHAMA WA CHADEMA

TIMBWILI LA WANACHAMA WA CHADEMA WAKIMPIGA MWANACHAMA MWENZAO ALIYEKUWA AKIPINGA HOJA ZA ZITTO KABWE MAHAKAMANI


- Dar es Salaam,Tanzania


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeahirisha kutoa hukumu ya kesi iliyofunguliwa jana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Zuberi Kabwe (Chadema), kuhusu ombi la kuitaka Mahakama hiyo kuizuia Kamati Kuu ya Chama hicho, kutomjadili katika kikao ambacho kilipangwa kufanyika leo jijini Dar es Salaam.
Wanachama wa Chadema, wakitwangana nje ya Mahakama Kuu, jijini Dar es Salaam. 

Jaji John Utumwa alisitisha kutoa hukumu hiyo mpaka siku ya Jumatatu saa 4:00 asubuhi.Hata hiyo baada ya Jaji huyo kuahirisha kesi hiyo, nje ya Mahakama hiyo kulikuwa na vurugu kubwa baada ya kundi linalo unga mkono maamuzi ya Chadema kutwangana na kundi linalo muunga Zitto Kabwe. 
Mwanachama wa Chadema, anayepinga hoja za Zitto Kabwe, akimtwanga mfuasi wa Zitto Kabwe. 

Hatua hiyo ilisababisha Askari wa Jeshi la Polisi kuingilia kati, huku wakiungana na upande wa Chadema na kuwatwanga marundi wafuasi wa Zitto waliokuwa na mambango kama ilivyokuwa kwa wenzao wa Chadema.

Kesi hiyo ilifunguliwa jana na wakili wa Mbunge huyo Albert Msando huku wakili wa Chadema Tundu Lissu akiweka pingamizi,hata hivyo Jaji John Utumwa wa Mahakama hiyo alitupilia mbali mapingamizi yote yaliyowekwa na Tundu Lissu.

Kamanda wa Al Qaeda Afariki

Kamanda wa Al Qaeda Afariki Dunia Akiwa Kizuizini



Majid-Al-Majid

Majid-Al-Majid

MAJESHI ya Lebanon yametangaza kuwa kamanda wa cheo cha juu wa kundi la kigaidi la Al Qaeda katika nchi hiyo Majid Al – Majid amekufa akiwa kizuizini. Kamanda huyo ambaye ni raia wa Saudi Arabia, alikuwa kiongozi wa kundi la Abdulha Azzam ambalo lina uhusiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda, ambalo pia limekuwa likikiri kuendesha mashambulizi ya kigaidi na milipuko ya mabomu kulenga maeneo yanayokaliwa na waumini wa madhehebu ya Shia katika siku za hivi karibuni.
Miongoni mwa mashambulizi waliyokiri kuhusika nayo ni shambulizi katika Ubalozi wa Iran nchini Lebanon. Maofisa wa jeshi wanasema Al Majid amekufa kutokana na maradhi ya figo na kwamba hali yake ilikuwa imezorota kwa muda sasa. Al Majid alikamatwa mwezi uliopita na alikuwa akishikiliwa katika kizuizi cha siri

MAAJABU MKOANI MBEYA

Mwanamke Mkoani Mbeya Ajifungua Watoto Wanne

Mwanamke Mkoani Mbeya Ajifungua Watoto Wanne
Aida Nakawala 25 mkazi wa kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya, hivi karibuni alijifungua watoto wanne  mapacha kwa mkupuo(Quadliplets) katika usiku wa kuamkia Mwaka mpya anaendelea vizuri.
Mwanamke huyo ambaye kwa hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa na watoto wake wote wanne alijifungua majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na watoto wakiwa na uzito wa kawaida tofauti na matarajio ya Wengi.

Muuguzi na msimamizi wa Watoto katika chumba cha Joto Sista Frolence Maisa amesema hali za watoto ni nzuri ambapo mama mzazi anahitaji kupatiwa vyakula vinavyoweza kumuongezea maziwa mengi kutokana na idadi ya watoto aliyonayo.

kikosi cha blog ya Mbeya Yetu  Kikiongozwa na Joseph Mwaisango ambacho kilifika kumjulia hali kiliguswa na hali hiyo na kujitolea kamsaada kidogo wa nguo za watoto sabuni  chupa na dishi  hivyo kuwaomba wadau wengine kumsaidia mama huyo ili aweze kuwalea vizuri watoto wake.
 KATIKA hali isiyokuwa ya Kawaida Mwanamke mmoja, Aida Nakawala 25 mkazi wa kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya, hivi karibuni alijifungua watoto wanne  mapacha kwa mkupuo (Quadliplets) katika usiku wa kuamkia Mwaka mpya anaendelea vizuri.
Mwanamke huyo ambaye kwa hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa na watoto wake wote wanne alijifungua majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na watoto wakiwa na uzito wa kawaida tofauti na matarajio ya Wengi.
Kwa mujibu wa Muguuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi aliyemfanyia huduma mwanamke huyo, Grace Konga alisema mzazi huyo ni miongoni mwa wazazi 9 waliojifungua katika Mkesha wa Mwaka mpya huku yeye akivunja rekodi kwa kujifungua watoto wanne kwa njia ya kawaida.
Muuguzi huyo alisema watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito uliotofautiana kwa mtoto  wa kwanza hadi wa
mwisho kuanzia kilogramu 1.6,1.5,1.5  na  2.0 ambapo baada ya kuona hali hiyo ilibidi kumpa rufaa kwa ajili ya msaada zaidi katika Hospitali ya wazazi ya Meta ambapo wapo katika Chumba cha Joto hadi sasa.
Aidha kwa mujibu wa Muuguzi na msimamizi wa Watoto katika chumba cha Joto Sista Frolence Maisa amesema hali za watoto ni nzuri ambapo mama mzazi anahitaji kupatiwa vyakula vinavyoweza kumuongezea maziwa mengi kutokana na idadi ya watoto aliyonayo.
Alisema kwa hivi sasa watoto wananyonya vizuri amb  po maziwa yakipungua kwa mama itahitajika msaada wa maziwa ya Kopo aina ya Laktojeni ili watoto waendelee kupatiwa maziwa kama kawaida na afya zao kuimarika.
Kwa upande wake Mzazi wa watoto hao Aida Nakawala alisema hali yake kiuchumi siyo nzuri kuweza kumudu kuwalea watoto hao na kuongeza kuwa mume wake ni mkulima aliyemtaja kwa jina la Web Simkanda hivyo anaomba msaada wa hali na mali kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema huo ni uzao wake wanne ambapo mtoto wake wa kwanza anaumri wa miaka saba, anayefuata ana miaka miwili na
miezi tisa huku mwingine akiwa amefariki dunia mara baada ya kujifungua kabla  ya uzao huu unaofanya kuwa na watoto Sita.
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa hali kama hiyo ya kujifungua watoto zaidi ya mmoja katika familia yao alisema Mama yake mzazi amewahi kujifungua mapacha wawili tu na hakuna mtu mwingine aliyewahi kuzidisha idadi hiyo ya watoto kama yeye.
Hata hivyo kutokana na kuguswa kwa mahitaji ya binti huyo na wanawe kikosi cha blog ya Mbeya yetu ambacho kilifika kumju ulia hali kiliguswa na hali hiyo na kujitolea kamsaada 
kadogo hivyo kuwaomba wadau wengine kumsaidia mama huyo ili aweze kuwalea
vizuri watoto wake.

SIRI YA MBUNGE WA KIGOMA ZITTO KABWE

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
SIRI za Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kukimbilia mahakamani kuzuia Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA isijadili uanachama wake zimeanza kuvuja.
Habari zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili, zinabainisha kuwa Zitto, aliyevuliwa nyadhifa zote ndani ya CHADEMA mwishoni mwa mwaka jana kwa madai ya kukisaliti na kukihujumu chama, alifikia uamuzi huo baada ya kudokezwa kuwa wajumbe wengi wamedhamiria afukuzwe uanachama.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baadhi ya wajumbe walikuwa wakifanya ushawishi kwa wenzao ili waunge mkono hoja ya kumvua uanachama Zitto pindi wakianza kujadili suala lake.
Inadaiwa kuwa wajumbe hao walichoshwa na vitendo vya mbunge huyo kukiumiza chama na viongozi wakuu katika mikutano aliyoifanya mkoani Kigoma hivi karibuni.
Inadaiwa kuwa wajumbe hao waliona ni heri CHADEMA ikose Jimbo la Kigoma Kaskazini kuliko kuendelea kuwa na Zitto ndani ya chama hicho.
Zitto, inaaminika hana ushawishi mkubwa ndani ya CC kama ilivyo nje, hivyo kumfanya ahahe kujinusuru na kuvuliwa unachama baada ya mwishoni mwa mwaka jana kuvuliwa madaraka yote aliyonayo ndani ya chama.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa kutokana na hofu ya kufukuzwa kwenye chama, Zitto aliamua kwenda mahakamani kuzuia CC isijadili suala lake hadi rufaa aliyoikata mwaka jana katika Baraza Kuu la chama hicho itakaposikilizwa.
Inaelezwa kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini, ni miongoni mwa wajumbe wanaotaka Zitto afukuzwe ili iwe fundisho kwa wanachama wengine wanaokwenda kinyume na taratibu za chama.
Wakati hali ikionekana kuwa tete ndani ya CHADEMA, hatima ya Zitto inatarajiwa kujulikana kesho wakati Mahakama Kuu chini ya Jaji John Utamwa itakapotoa hukumu dhidi ya shauri lililofunguliwa na mbunge huyo.
Juzi, Jaji Utamwa alizuia CC ya CHADEMA kwa muda kujadili uanachama wa Zitto hadi kesho atakapotoa uamuzi wa jambo hilo.
Hata hivyo, tayari suala la Zitto limesababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama ambapo kuna pande mbili kubwa, moja ikiunga mkono uamuzi wa kuvuliwa nyadhifa zote kiongozi huyo, huku nyingine ikipinga.
Pande hizo juzi zilikutana mahakamani zikiwa na mabango yenye ujumbe wa kumpinga Zitto na wengine kumuunga mkono.
Hatua ya Zitto kwenda mahakamani imemuweka katika mazingira magumu ya kuepuka kuondolewa uanachama wake ambapo baadhi ya makada wamekuwa wakimuita msaliti kwa hatua yake hiyo.
Wakati wenzake wakimuona msaliti, Zitto mara kadhaa amekuwa akijinasibu kuwa atapigania uanachama wake ndani ya CHADEMA na hatang’oka hadi atakapoondolewa.
Wajumbe vurugu CC
Wakati suala la Zitto, likionekana kuwagawa baadhi ya wanachama wa CHADEMA, wajumbe wa Kamati Kuu walionekana kuwa na shauku ya kulijadili suala hilo.
Ingawa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alizuia lisijadiliwe kutokana na pingamizi lililowekwa mahakamani, baadhi ya wabunge walitaka kupuuza amri hiyo ya mahakama, lakini walizuiwa.
Mwesiga Baregu na Mabere Marando, inaelezwa walikuwa mstari wa mbele kupinga mjadala wa Zitto kwa maelezo kuwa ni busara chama kikaheshimu uamuzi wa mahakama.
Kilichojadiliwa CC
Mnyika, jana aliwadokezea waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kilichozungumzwa na vikao vya CC.
Alisema CHADEMA itaunganisha nguvu ya kudai haki kwa wananchi wote watakaokosa haki ya msingi ya kupiga kura katika mchakato wa kura ya maoni juu ya katiba mpya.
Aliongeza kuwa hoja hiyo inatokana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutokuwa tayari kuboresha daftari la wapiga kura kwa lengo la kuwapa fursa wananchi kujiandikisha.
Mnyika alisema Kamati Kuu imesikitishwa na Tume ya Uchaguzi kushindwa kutoa kauli juu ya maboresho ya daftari hilo hali waliyoielezea kuwa inadhihirisha hofu ya chama chao kuwa tume hiyo haina uwezo na nia ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata haki ya msingi ya kupitisha katiba waitakayo.
Alisema kutokana na hali hiyo, CHADEMA itafanya mikutano ya hadhara, maandamano na njia nyingine kuhakikisha haki ya msingi ya wananchi kupiga kura inaheshimiwa.
Mnyika alisema pia CHADEMA wamepokea rasimu ya pili ya mabadiliko ya katiba na kwamba katika hatua ya awali wameunga mkono pendekezo la kuwepo serikali tatu wakati mapendekezo mengine yakifanyiwa uchambuzi yakinifu kulinganisha na maoni yaliyotolewa na wananchi.
Alisema pia wameshindwa kuwajadili wanachama wawili wa chama hicho, Dk. Kitilla na Mwigamba kwa sababu wakati wakijadili ajenda za awali walikuwepo nje ya ukumbi wa mkutano, na kwamba muda wa kuwasikiliza ulipofika hawakuonekana katika eneo hilo.
Mnyika alisema Kamati Kuu ilikuwa na uwezo wa kupitia utetezi wao pasipo wahusika kuwepo ndani ya ukumbi wa mkutano, lakini ikaonekana itoe nafasi ya mwisho kwa wanachama hao ili waweze kuhudhuria na kujibu hoja zitakazojitokeza.
Akizungumzia majina ya wajumbe yaliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya uteuzi wa wabunge wa Bunge la Katiba, Mnyika alisema Kamati Kuu imeridhia majina manne yaliyopatikana na kwamba waliangalia sifa na ujuzi wa watu hao katika maeneo mbalimbali ya kijamii na ufahamu wao juu ya katiba.
Aliyataja majina ya watu waliopendekezwa kuwa ni Wakili Marando, Profesa Abdallah Safari, Wakili Method Kimomogoro na Nasra Juma Baruani anayewawakilisha wanawake