Morogoro. Wakati jamii ikiwa bado haijasahau mateso aliyoyapata mtoto Nasra Mvungi na kusababisha kifo chake, tukio lingine la aina hiyo limetokea katika Kijiji cha Matongola, Tarafa ya Magole Wilaya ya Kilosa, baada ya kubainika mtoto wa miaka sita akiwa amefichwa uvunguni mwa kitanda na kufanyiwa vitendo vya kikatili na mama yake mzazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa taarifa za mateso ya mtoto huyo zilifikishwa Kituo cha Polisi wilayani Kilosa za saa za mchana jana, baada ya uongozi wa kijiji na kata kutoa taarifa na tayari mwanamke huyo amekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Mama aliyefanya ukatili huo anafahamika kwa jina la Sala Mazengo ambaye alimficha ndani mtoto wake aliyefahamika kwa jina la Devota Malole na kumfanyia vitendo vya kikatili ikiwa pamoja na kutompa chakula, wala kumfanyia usafi.
Baada ya kufichuliwa kutoka alipofichwa, mtoto huyo alionekana kuwa dhaifu kiafya kutokana na kukosa lishe pamoja na mazingira aliyokuwa akiishi kutoridhisha, jambo ambalo ni kosa kisheria, pia ukiukwaji wa haki za watoto.
Inadaiwa kuwa tangu mwka 2009 Sala amekuwa akimficha mtoto wake huyo ambaye sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa vipimo na matibabu.
Hata hivyo, mwanamke huyo alipoulizwa alidai kuwa afya ya mtoto wake ilikuwa mbaya tangu alipozaliwa kutokana na magonjwa ya mara kwa mara, pia hali ngumu ya maisha ilichangia kudhoofisha afya ya mtoto huyo.
Alidai kuwa ana watoto sita, pia alikiri kumlaza chini mtoto huyo kutokana na kuwa na kitanda kimoja, ambacho hakiwatoshi watoto hao.
Aliongeza kuwa hata chakula amekuwa akikipata kwa shida kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa kuwa ana mtoto mwingine mdogo.
Kamanda Paulo alisema kuwa mwili wa mtoto huyo umedhoofu kutokana na kufichwa ndani kwa muda mrefu na bado mwanamke huyo hajaeleza sababu za kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto huyo.
“Siwezi kutoa taarifa ya kidaktari, lakini kutokana na afya ya mtoto yule na mazingira tuliyomkuta ni dhahiri alikuwa akipata mateso na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Hata hivyo, uchunguzi zaidi tunaufanya na kwamba taratibu za kumfikisha mtuhumiwa huyo Kituo Kikuu cha Polisi mkoani hapa zinaendelea,” alisema Kamanda Paulo.
Alisema kuwa mpaka sasa bado haijafahamika kama mtoto Davota ni mlemavu au la na kwamba taarifa za afya ya mtoto huyo zitatolewa baada ya madaktari kumfanyia uchunguzi wa kina.
No comments:
Post a Comment